https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    SIMBA SC VS AZAM FC; MBINU ZITATOA MSHINDI……

    SIMBA_v_AZAM-FILEminimizer
     Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
     Itakuwa ‘ bonge ya gemu’  jioni hii katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara, Vodacom Premier league, Azam FC dhidi ya mabingwa mara 19 wa zamani ambao wanasotea nafasi mbili za juu kwa msimu wa tatu sasa, Simba SC. Azam FC inaongoza ligi kabla ya michezo ya Jumapili hii wakiwa na pointi 20 itaingia uwanjani ikiwa imetoka kushinda michezo miwili mfululizo ugenini dhidi ya Stand United 0-1 Azam FC, Kagera Sugar 1-3 Azam FC.

     Simba chini ya Goran Kopunovic imeshuka dimba mara moja na kupata ushindi wa pili msimu huu kufuatia ushindi wa Ndanda FC 0-2 Simba SC katika uwanja wa Nang’wanda  wiki iliyopita. Simba wananing’inia katikati ya msimamo wakiwa na pointi 12 wanahitaji ushindi ili kupunguza gepu la pointi na viongozi hao.Kitendo cha kupoteza mchezo huo itakuwa ni sawa na kujiondoa katika mbio za ubingwa, kwani licha ya kuwa nyuma kwa mchezo mmoja, kitendo cha kuwaruhusu Azam kushinda itawafanya Simba kuwa nyuma ya pointi 11 dhidi ya mabingwa hao watetezi.
     SI MECHI YA KIPIMO CHA UBINGWA, LAKINI……
    Mabadiliko yote ya uchezaji katika kikosi cha Simba yametajwa kuletwa na kocha, Goran ambaye tangu alipoanza kazi klabuni hapo mwezi uliopita, ameisaidia Simba kushinda michezo yote saba ya kimashindano ikiwemo kushinda ubingwa wa Mapindu Cup huko Visiwani Zanzibar. Goran ameiongoza Simba dhidi ya timu za Bara katika michezo miwili. Mchezo wa kwanza ulikuwa ni ule dhidi ya Mtibwa Sugar 0-0 Simba SC katika fainali ya michuano hiyo ya Mapinduzi. Simba ilishinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.
     Mchezo wa pili wa Goran dhidi ya timu za Bara ni ule wa ligi kuu waliopata ushindi ugenini dhidi ya Ndanda FC wiki iliyopita. Kiuchezaji Simba imeonekana kuimarika kiasi cha kufufua matumaini ya mashabiki wake kuwa huenda wakarudi katika nafasi mbili za juu ambazo hutoa wawakilishi wa nchi kaika michuano ya Afrika upande wa vilabu. Msimu uliopita Simba ilipoteza michezo yote dhidi ya Azam FC na pointi hizo sita ziliwasaidia Azam kufikia ndoto na kutwaa ubingwa wa kwanza wa ligi kuu Bara. Je, Simba imeimarika kweli?
     Azam ilianza msimu kwa spidi ya chini ikiwemo kupoteza michezo miwili mfululizo dhidi ya JKT Ruvu  1-0 Azam FC, Ndanda FC 1-0 Azam FC vipigo ambavyo viliambatana na sare dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons. Simba pia walianza kwa mwendo wa kusuasua, sare sita mfululizo, kabla ya ushindi wa kwanza katika raundi ya saba, Simba SC 1-0 Ruvu Shooting, kisha kichapo Simba SC 0-1 Kagera Sugar katika raundi ya nane, imezinduka dhidi ya Ndanda  FC huku vijana wa Goran wakicheza michezo saba pasipo kuruhusu goli langoni mwao.
     Kipimo zaidi cha malengo yao mapya ni mchezo wa leo, kama ushirikiano wa Kipre Tchetche, Didier Kavumbagu na Brian Majwega hautazalisha goli lolote kwa kuthibitiwa na safu ‘ kabambe’ ya ulinzi chini ya nahodha mpya wa timu kijana Hassan Isihaka, 20, Murisheed Juuko, Hassan Kessy na Mohamed Hussein bila shaka Goran anaweza kuwa sababu kubwa ya mafanikio. Lakini bado kuna safari ndefu ambayo Goran na vijana wake wanayo kwanza ni kuwazima mabingwa watetezi waliorudi katika ‘ mwendo wa ushindi’.
     Frank Domayo atacheza mchezo wake wa kwanza mkubwa baada ya miezi takribani saba, lakini ni mchezaji kijana mwenye uzoefu mkubwa, mara nyingi ameshiriki kiuhakika katika mipambano ya Simba na Yanga SC. Kiungo huyo maarufu kwa jina la ‘ chumvi’ alifunga bao pekee katika ushindi dhidi ya Stand United na akashiriki katika upishi wa moja ya mabao matatu ya Azam katika ushindi dhidi ya Kagera Sugar. Sasa ndiye kiungo-namba-8 wa Azam atakutana na ‘ mtu mbishi’, nahodha msaidizi Jonas Mkude.
    Sehemu hii ya kaikai ya uwanja itakuwa na ushindani mkubwa, baada ya kutokea benchi na kutengeneza moja ya mabao mawili ya timu yake dhidi ya Ndanda FC, Mganda, Simon Sserunkuma anatazamiwa kuanza sambamba na Mkude na Said Ndemla katika eneo la kiungo upande wa Simba. Kipre Bolou ambaye urejeo wake katika mchezo dhidi ya Kagera siku ya Jumanne kumeifanya safu ya kiungo ya Azam kuwa na nguvu. Himid Mao anaweza kuanza mahala kwa Mudathir Yahya. Salum Abubakary Hajaonekana katika michezo kadhaa sasa ni kiungo ambaye huwasumbua sana Simba. Kila timu itakuwa na nafasi ya kutawala mchezo, timu itakayokuwa na mbinu bora inaweza kushinda.
     Kocha wa Azam FC, Joseph Omog anahaha kuziba ‘ nyufa’ katika ngome. Shomari Kapombe atakuwa akicheza kwa mara ya kwanza dhidi ya timu yake ya zamani atakutana na Danny Sserunkuma ambaye licha ya kucheza katika eneo la ushambuliaji hupendelea kucheza pembeni upande wa kushoto, huko hutulia na mpira na kushambulia kwa kasi. Danny atahitaji spidi
     Mchezo huu ni kipimo kwa safu ya ulinzi ya wawakilishi hao wa Tanzania katika klabu bingwa Afrika, kwani wanakutana na safu ya mashambulizi yenye kasi na uwezo wa kumiki mpira. Licha ya uwepo wa Danny, Emmanuel Okwi anataraji pia kuanza sambamba na Ramadhani Singano katika wingi ya kulia. Omog anaweza kuwatumia Kapombe upande wa kulia, Erasto Nyoni katika beki-3, Paschal Wawa na kaimu nahodha Aggrey Morris.
     Azam wamekuwa na tatizo katika ngome, mipira ya krosi, kona na faulo imekuwa ikiwagharimu sana kama wataziba nyufa za kupitishwa mipira kutokea pembeni mwa uwanja wanaweza kufanikiwa kushinda, lakini bahati mbaya Simba hutumia krosi za chini ambazo ni hatari kwa walinzi wasio na utulivu. Nani msindi? Timu itakayokuwa na mbinu bora inaweza kushinda mchezo huu. Azam wanauwezo wa kufunga mabao mawili, Simba wataweza?. Danny tayari amefunga bao katika mchezo wake wa pili wa ligi kuu, anaweza kufunga tena leo.

    Credit Shafiidauda
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC VS AZAM FC; MBINU ZITATOA MSHINDI…… Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top