Katika umri wa miaka 29 mshambulizi, Mussa Hassan Mgosi bado ana safari ndefu katika maisha ya soka la ushindani. Mgosi ambaye kwa msimu wa pili sasa yuko ametulia katika klabu ya Mtibwa
Sugar ya Turiani, Morogoro ambayo alijiunga nayo, Agosti, 2013 baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa muda mfupi na JKT Ruvu ya Pwani.
Katika mchezo wa robo fainali ya michuano inayoendelea ya Mapinduzi Cup huko Zanzibar kati ya Mtibwa na Azam FC, Mgosi alionesha uwezo mkubwa, alikuwa mwenye nguvu, akili na uwezo wa kukimbia hata mbele ya wachezaji wanne wa Azam. Shomari Kapombe ambaye alicheza katika nafasi ya beki wa kulia upande wa Azam alikutana na wakati mgumu kumkabili,
Mussa mshambulizi wa zamani wa Simba SC na Darling Club Motema Pembe ya DR Congo. Moja kati ya mechi za kukumbwa sana kwa mashabiki wa soka nchini ni ile iliyowahusisha mahasimu wa kandanda nchini Yanga na Simba, Agosti 18, 2010 kati Ngao ya Jamii ( yanga ilishinda mchezo huo kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 3-1). Shadrack Nsajigwa ‘ Fusso’ wakati huo alikuwa ndiye mlinzi bora wa kulia nchini lakini alikumbana na ‘ fedheha’ kubwa baada ya kupigwa ‘ chenga kali ya mwili’.
Mgosi akitumia zaidi mguu wa kulia alimsogelea kwa kasi, Nsajigwa kisha akayumbisha mwili ndani ya uwanja kisha akausogeza mpira upande wa kushoto na kufanya kitendo cha haraka, kunyumbulika na kukimbia kwa kasi. Nsajigwa akajikuta ameachwa na alipogeuka, Mgosi alikuwa hatua tano zaidi yake akaanza ‘ kuunga tera’ bila mafanikio.
Sikushangaa kumuona kijana ( Kapombe) akitaabika kumkamata Mgosi katika mchezo ambao ulishuhudia Mtibwa ikiwaondoa Azam kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 7-6. Mtibwa iliishinda pia Polisi kwa changamoto ya mikwaju ya penalti katika nusu fainali na sasa watacheza na Simba katika mchezo wa fainali.
Akiwa baba wa watoto wawili, ( Hassan 12, Laylat 5) anakiri wazi kuwa Simba ndiyo klabu iliyomkomaza kisoka na kumpa umaarufu lakini amekuwa mwenye furaha licha ya kuwa nje ya timu hiyo kwa miaka minne sasa baada ya kuondoshwa ‘ kimizengwe ‘ klabuni. Mgosi alikuwa ni mmoja ya wachezaji nyota ambao walituhumiwa kuikosesha Simba ubingwa wa Tanzania msimu wa 2010/11.
Aliondoka na kujiunga na Motema Pembe kabla ya kurejea nchini kujiunga na JKT Ruvu mwanzoni mwa mwaka 2013. Imezoeleka kusemwa kuwa wachezaji ambao huondoka katika klabu za Simba na Yanga ‘ wamekwisha’, ndiyo lakini si wote. Wengi huachwa kwa sababu zisizo za kimpira. Mgosi alilazimishwa kuondoka Simba na uongozi uliopita ambao ulishindwa kufanya jitihada kuhakikisha timu hiyo inatetea ubingwa wake licha ya kuwa juu ya msimamo kwa tofauti ya pointi sita zikiwa zimesalia mechi tatu msimu kumalizika.
Simba ilijaribu kumrudisha mchezaji huyo mwezi uliopita katika usajili wa dirisha dogo, lakini wakaambiwa wazi waende klabuni Mtibwa wakatoe fungu la usajili kwa kuwa yuko ndani ya mkataba na timu hiyo. Pia aliwaambia viongozi anahitaji kupewa fedha nyingi kuliko mchezaji yoyote nchini. Misimu sita mfululizo aliyoichezea Simba bila shaka amejifunza mengi. Hakuwa na sababu ya kuicha Mtibwa timu iliyompandisha thamani kwa mara nyingine wakati ambao alionekana si mchezaji bora tena. Alifunga dhidi ya Simba na Yanga msimu uliopita, na mabao yake matatu msimu msimu huu, magoli mawili amefunga dhidi ya Yanga na Simba.
Mgosi ni mchezaji ambaye jobo la ufundi la CAF, Shirikisho la soka Afrika lilimteua katika kikosi bora cha CHAN, 2009, Ivory Coast kutokana na uwezo wake mkubwa uwanjani. Uzoefu wake wa miaka 11 katika ligi kuu Bara umeonekana kuisaidia sana timu hiyo msimu huu. Alimfunga bao la ‘ tobo’ mlinda lango wa Simba, Manyika Peter Manyika, Novemba, 2014 baada ya kumdanganya kipa huyo chipukizi na kukubali kutanua miguu na hivyo kutoa mwanya kidogo kwa mshambulizi huyo kupitisha katika mazingira pekee yaliyopatikana na kufunga bao la kusawazisha katika mchezo uliomalizika, Mtibwa 1-1 Simba.
Kama wachezaji wazoefu wataendelea kushindana na vijana kama wafanyavyo, Mgosi, Vicent Barnabas, Shaaban Nditti, Said Mkopi, Malegesi Mwangwa, Abuu Mtiro na wengineo bila shaka ushindani na ubora fulani utapanda katika soka nchini. Ni wachezaji wenyewe kukubali kucheza kwa namna ya kujituma, nidhamu, na moyo wa kuhitaji mafanikio kokote pale wanapocheza.
Musa Hassan Mgosi huyu wa sasa si yule aliyetokea benchi na kwenda uwanjani kukomboa mabao mawili dhidi ya SC Villa katika mchezo nusu fainali ya Tusker Cup, 2005 katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, huyu ni Mgosi mwenye uzoefu zaidi, ubora zaidi, mbinu zaidi na usongo uleule. Ligi kuu Bara inawahitaji wachezaji kama yeye, walio tayari kukubali kucheza kwa dhati wakiwa nje ya klabu za Simba na Yanga.

