Jeshi la
polisi mkoa wa Morogoro limeanza kufanya oparesheni ya kuwatafuta
watuhumiwa waliohusika na mauaji ya watu watatu wakiwemo wakulima
wawili na mfugaji mmoja, kufuatia mapigano yaliyozuka kati ya wakulima
na wafugaji katika bonde la matembele linalounganisha kijiji cha
Mabwegere na Mbigiri wilayani kilosa mkoani Morogoro.
Mkuu wa wilaya ya Kilosa Elis Tarimo akizungumzia tukio hilo wakati
alipotembelea majeruhi katika hospitali ya mission St Joseph Dumila
amesema mauaji hayo hayatavumilika na jeshi la polisi litahakikisha
linawakamata waliohusika na tukio hilo.
Tarimo amewataja waliofariki dunia kuwa ni Joseph Peter (26)
mkulima, Rajabu Selemani (55) mkulima na Kaduru Kashu (30) mfugaji na
wengine wamelazwa hospitalini hapo huku mmoja akihamishiwa katika
hospital ya mkoa wa Morogoro.
Kufuatia tukio hilo mkuu wa wilaya ya Kilosa Elias Tarimo ametupia
lawama Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuchelewa kuleta
wasuluhishi wa mgogoro huo kama serikali ilivyoahidi kwa lengo la
kuhakiki upya mipaka ya vijiji ili kuondoa migogoro ya wakulima na
wafugaji, iliyodumu kwa muda mrefu.
Nao majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Mission Joseph Dumila
wamelalamikia serikali kushindwa kumaliza tatizo la migogoro ya
wakulima na wafugaji.Nae muuguzi wa zamu Melania Shayo amesema wakulima
wawili walifariki dunia wakati wakipatiwa matibu na kukiri kupokea
maiti moja ya mfugaji aliyeuwawa wakati wa mapigano hayo.
Mapigano haya yamekuja siku chache baada ya nyumba 41 kuchomwa moto
zikiwemo za wakulima na wafugaji kufutia mgogoro wa ardhi katika kijiji
cha mabwegere wilayani kilosa, ambapo mkuu wa wilaya aliwakutanisha
wakulima na wafugaji kwa lengo la kumaliza mgogoro huo lakini hata hivyo
mkutano huo uligubigwa na mivutano na wafugaji kuondoka kabla ya
mkutano kumalizika..