Siku tisa
baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza kumvua
uanachama, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe jana alitinga bungeni
na kufanya kikao cha siri na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa zaidi ya
saa moja.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka kwa watu walio karibu naye, mbunge huyo
alipanga kuaga wabunge jana asubuhi baada ya kumalizika kwa kipindi cha
maswali na majibu, lakini baadaye alilieleza gazeti hili kuwa
atazungumzia hatima ya ubunge wake leo.
Mbunge
huyo ambaye pia jana alichangia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Udhibiti
wa Ajira za Wageni wa Mwaka 2014, alipowasili bungeni wabunge wengi
walidhani angewaaga kutokana na taarifa zilizosambaa mjini hapa juzi
kuwa angetumia siku ya jana kuaga lakini hakufanya hivyo.
Akizungumzia
hali hiyo Zitto alisema: “Kuhusu mimi kuaga bungeni we subiri tu. Kama
jambo hilo lipo litakuwepo tu. Ila kwa sasa, nimeitwa na Spika Makinda
na ndiyo nakwenda kuzungumza naye.”
Aliongeza,
“Si unaniona bwana, nimekuja bungeni na kama nisingekuwa mbunge
nisingekuja. Nitazungumza tu, ila kwa sasa ngoja tuone mambo
yatakavyokwenda.”
Hata
hivyo, habari kutoka kwa watu walio karibu na Zitto zililieleza gazeti
hili kuwa mbunge huyo atatoa kauli leo baada ya kushauriana na spika wa
sasa, spika aliyepita, Waziri Mkuu wa sasa, waziri mkuu aliyepita,
aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Chadema, Said Arfi na washauri wake wa
karibu kuhusu suala hilo.
Zitto
alipoulizwa kuhusu hilo, alisema, “Aliyekueleza yuko sahihi, nitaongea
kesho (leo) jioni kabla ya Bunge kuahirishwa ili kuweka wazi msimamo
wangu kuhusu kinachoendelea kwenye ubunge wangu.”
Chadema
ilitangaza kumvua Zitto uanachama siku tisa zilizopita, saa chache baada
ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kutupa shauri lake alilofungua
akitaka chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho
kumpa nyaraka za vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote.
Awali,
Mahakama hiyo ilitoa amri ya muda ya kuizuia Chadema kumjadili na
amedumu kwenye nafasi ya ubunge chini ya zuio hilo kwa takriban mwaka
mmoja.
Iwapo
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itapokea taarifa ya kuvuliwa kwake
uanachama na kumjulisha Spika, Zitto atakuwa amepoteza kiti hicho.
-MWANANCHI


