
HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA
MAMBO YA NDANI YA NCHI, MHE. GODBLESS LEMA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI
MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA
USIMAMIZI NA UDHIBITI WA SILAHA NA RISASI YA MWAKA 2014 (THE FIREARMS
AND AMMUNITION CONTROL ACT, 2014)
Inatolewa chini ya Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013
__________________________
UTANGULIZI Mheshimiwa
Spika, Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu, familia yangu na viongozi wangu
wa chama na wananchi wa Jimbo langu. Nawashukuru pia maadui zangu kwa
dhati kwani uadui wao, hila zao, na mbinu zao chafu dhidi yangu
zimeendelea kuiimarisha imani yangu na tumaini langu siku hadi siku,
katika vita hii muhimu tunayopigana ya kulikomboa taifa hili.
Mheshimiwa Spika,Muswada
huu wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi unaletwa
katika Bunge lako tukufu wakati ambapo nchi hii iko katika mtanziko
mkubwa ambapo matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yamekithiri; mauaji
ya raia kwa kutumia silaha za moto yameongezeka; matukio yenye sura ya
ugaidi ya utekaji na utesaji yameshuhudiwa hapa nchini, matukio ya
uvamizi na uporaji wa silaha katika vituo vya polisi yanashamiri na
uhamiaji haramu umekuwa ukiongezeka pia kwa kasi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Ni
ukweli usiopingika kwamba matukio yote haya yametokea huku kukiwa na
sheria ya Usimamizi wa Silaha na Risasi ambayo itafutwa na muswada huu
kama utapitishwa na Bunge. Hii ni dhahiri kwamba tatizo kubwa la nchi
hii sio sheria na matumizi yake, bali ni uongozi uliokosa fikra chanya
na utu katika kutawala.
Ndio maana leo, Serikali
inafikiri kupambana na janga la Mauaji ya Albino ni kuwatenga Albino na
jamii kutoka kwenye makazi yao ya kawaida wakati tatizo la msingi ni
imani potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaamini kwamba; huwezi kuipinga imani kwa kutumia silaha
isipokuwa kwa habari njema (imani inayojali utu) kuwafikia watu wote.
Mheshimiwa Spika,Pamoja
na nia njema ya Serikali ya kuleta Muswada huu, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaamini kwamba, kama Serikali itajali utu, usawa, haki na demokrasia ya
kweli pengine hakungekuwa na hofu ya matumizi mabaya ya silaha miongoni
mwa wananchi na hivyo kusingekuwa na na haja ya kuleta sheria za
kudhibiti silaha na kuweka masharti magumu kwa wananchi kumiliki silaha,
hasa kipindi hiki ambacho kumekuwa na matukio mengi ya kigaidi, ya
uvamizi, utekaji na utesaji ambapo kimsingi wananchi wanahitaji ulinzi
wa Serikali na ulinzi binafsi zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Mheshimiwa Spika,Taifa
linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ifikapo
Oktoba mwaka huu wa 2015. Matumizi bora ya sheria za kulinda amani
nchini ni muhimu sana wakati huu. Lakini mambo muhimu na ya msingi
yakipuuzwa amani inaweza kutoweka licha ya sheria ngumu za udhibiti
ikiwemo ya udhibiti wa silaha kuwepo: Masuala hayo ni kama yafuatayo:
i. Kuchezea haki ya mwananchi kujiandikisha kuwa mpiga kura:
Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inasisitiza kwamba, mzaha katika jambo hili hautavumilika.
Aidha, ijulikane kwamba wananchi watakapotambua kuwa hawawezi kuwapata
viongozi wao wanaowataka kupitia sanduku la kura, basi wanaweza kutafuta
haki yao kwa njia nyingine hali ambayo inaweza kuliingiza taifa katika
machafuko kwani haki haiombwi ila inadaiwa.
Aidha, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inatoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili waweze kuamua
nani atakuwa kiongozi wao kwenye uchaguzi Mkuu unaokuja. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inamkumbusha kila mwananchi atambue kwamba “Kura yako
ni Maisha yako, Nenda Kajiandikishe Sasa”
ii. Kufanya Mzaha na uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi:
Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaionya Serikali kutofanya Mzaha na jambo hili kwani linaweza
kuiingiza nchi katika machafuko makubwa. Mheshimiwa Spika, Viongozi wa
nchi hii wamekuwa wakifanya mizaha kuhusu maisha ya wananchi kwa mambo
mengi, yakiwemo ufisadi uliokithiri. Kwa mfano wewe mwenyewe Mheshimiwa
Spika, uliwahi kumwomba Mheshimiwa Andrew Chenge kutoa mwongozo wa
kutengeneza maazimio ya Bunge kuhusu watuhumiwa wa wizi wa fedha za
Escrow wakati yeye mwenyewe alikuwa ni mtuhumiwa.
Huu ni mzaha mkubwa ambao
kwa tafsiri inaonyesha kwamba watawala wanawaona watanzania kuwa ni
wajinga. Kambi Rasmi ya Upinzani inaonya kuwa mizaha kama hii ikiletwa
kwenye suala la uwepo wa tume huru ya uchaguzi, taifa hili linaweza
likasambaratika. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Tume
Huru ya Uchaguzi, si kwa sababu inataka kushinda uchaguzi bali ni kwa
sababu inataka kujenga na kulinda Imani ya Mpiga Kura ili kulinda amani
ya nchi yetu”.
iii. Matumizi ya Kisiasa ya Jeshi la Polisi:
Mheshimiwa Spika, kwa
vile imethibitika pasipo shaka yoyote kwamba Polisi mkatili na mkorofi
dhidi ya Upinzani anapandishwa cheo, ni dhahiri kwamba kitendo hiki
kimejenga msingi (precedence) wa polisi kuwaonea, kuwadhalilisha na
kuwafedhehesha viongozi wa Upinzani kwa matarajio kwamba watapongezwa na
kupandishwa vyeo na Serikali.
Mheshimiwa Spika,Kambi
Rasmi ya Upinzani imepigia kelele sana suala hili la matumizi mabaya ya
Jeshi la Polisi ya kulinda maslahi ya kisiasa ya watawala kwa miaka
yote. Viongozi, wanaharakati na wananchi wanaounga mkono mageuzi
wamepita kwenye bonde la uvuli wa mauti kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika,
Hatukuonewa kwa sababu sisi ni wanyonge, ila ni kwa sababu tumeendelea
kuwa wavumilivu. Nina mashaka kama uvumilivu huo utandelea kuwepo kama
uonevu na ukandamizaji utaendelea.
Mheshimiwa Spika,
Mwenyezi Mungu, pamoja na upole wake, ukarimu wake, upendo wake, rehema
zake kwa watu wote lakini bado ametenga Jehanamu kwa watenda dhambi
ambao amewaumba yeye mwenyewe. Tusisubiri wananchi wachoke kuvumilia,
bali hekima ya Mungu ituongoze ili kuliepusha taifa letu na majanga ya
uvunjifu wa amani pindi watu watakapokosa uvumilivu wa mateso.
iv. Ulinzi wa Raia na Mali zao:Mheshimiwa Spika,
Kukosekana kwa ulinzi na
usalama wa raia na mali zao kunaweza kuliingiza taifa katika machafuko.
Matukio ya kuuwawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi – Albino, mauaji ya
vikongwe na wanawake kutokana na imani za kishirikina yamekithiri sana
katika nchi yetu licha ya kuwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
Hali hii imefanya
wananchi kukosa imani na Serikali kwa kuwa bado yanaendelea licha ya
kampeni nyingi kutoka kwawanaharakati mbalimbali kupinga mauaji ya
Albino. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitahadharisaha Serikali
kutodharau kundi la Albino kuwa ni dogo na kutolipatia ulinzi wa
kutosha.
Mheshimiwa Spika,Baada ya
utangulizi huo, sasa naomba nijielekeze kwenye muswada wa Sheria uliopo
mbele yetu unaohusu Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi.
Mheshimiwa Spika,Matukio
yote niliyoyataja hivi punde, ni matukio ambayo kwa kiasi kikubwa
yamedhoofisha hali ya usalama hapa nchini. Hivyo, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaona kwamba muswada huu umekuja wakati muafaka kwa
kuwa matukio niliyoyataja hapo juu ambayo yamekuwa yakiongezeka hapa
nchini, ni matukio ambayo utekelezaji wake unahitaji silaha. Na kwa kuwa
matukio hayo ni ya kihalifu, ni dhahiri kwamba hata silaha
zinazotumika, hazina uhalali.
Hivyo sheria bora
itakayoweka udhibiti na usimamizi wa matumizi ya silaha hapa nchini
inaweza kufanikiwa kupunguza matukio ya kihalifu ikiwa itatungwa kwa nia
njema ya kulinda usalama wa raia wote na sio kwa lengo la kukandamiza
kundi fulani la watu ili kukidhi matakwa ya kisisasa ya kundi la watu
wachache.
MAONI NA MAPENDEKEZO YA JUMLA
Mheshimiwa Spika,Kabla
sijaanza kuchambua vifungu vya muswada huu, naomba nitoe maoni ya jumla
ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu utekelezaji bora wa muswada
huu pindi utakapokuwa sheria kama ifuatavyo:
i. Serikali iimarishe
ulinzi wa raia na viongozi sambamba na matumizi ya Sheria ya usimamizi
na udhibiti wa silaha na risasi. Itakuwa haina maana sana kuweka sheria
ya usimamizi na udhibiti wa silaha na risasi kama wananchi na viongozi
watakuwa hawana ulinzi dhidi ya watu wanaotumia silaha kwa malengo ya
kihalifu.
Mheshimiwa Spika, mpaka
sasa ninapowasilisha maoni haya ya Kambi ya Upinzani kuhusu muswada huu,
wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawana ulinzi wa
Serikali. Ni ajabu kwamba Mbunge ambaye kimsingi kazi zake zinamfanya
awe na maadaui ambao ni wahalifu na mafisadi anakuwa hana ulinzi wowote
wa serikali.
Kwa mfano maisha ya Mhe.
David Kafulila aliyeibua sakata la wizi wa Escrow na kusababisha
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mawaziri kufukuzwa kazi yako hatarini
kwa kuwa hana ulinzi wowote. Lakini wakuu wa Wilaya ambao kazi zao ni
kupokea mwenge, kusoma taarifa za UKIMWI na njaa wilayani na kupokea
wageni wa kitaifa wana ulinzi majumbani mwao.
Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka tukio la kuvamiwa na kuchomewa nyumba kwa
wabunge wenzetu. Wabunge hawa wangekuwa wamepatiwa ulinzi wa polisi
wenye silaha yamkini uvamizi ule ungeweza kuepukika.
Kwa mantiki hii Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuanzia sasa kutoa ulinzi
kwenye nyumba za wabunge na viongozi wengine wanaostahili huduma hiyo
kama ambavyo Serikali ya Kenya imefanya kwa wabunge na viongozi wake.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutofanya ubaguzi wa
ki-ulinzi kwa viongozi katika mihimili mitatu ya Dola (yani Serikali,
Bunge na Mahakama).
ii. Wabunge wote na
viongozi wote wenye hadhi ya kidiplomasia (Diplomats) wawe na sifa za
moja kwa moja (direct entitlement) za kumiliki silaha kwa ajili ya
kujilinda mara tu wanapopata hadhi hiyo ya kidiplomasia.
Utaratibu wa
kuwatambulisha kwa msajili wa Silaha ili kupatiwa leseni ya umiliki wa
silaha ufanywe na taasisi wanazozitumikia. Lengo hapa ni kuepusha
mlolongo mrefu wa kuwajadili viongozi walioaminiwa na wananchi walio
wengi (kama Rais na wabubunge) au viongozi walioaminiwa kwa kiwango cha
juu na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadiliwa na ngazi za chini za
uongozi katika vitongoji na mitaa kama ambavyo sheria ya sasa
inavyoelekeza.
Kitendo cha kuruhusu
viongozi wakuu walioaminika kujadiliwa na ngazi za chini kama wana sifa
au hawana sifa za kumiliki silaha ni udhalilishaji wa itifaki
(humiliation of protocol)
iii. Ulinzi na Usalama ni
pamoja na kutambua hadhi na Itifaki.Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kutambua hadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa ambao si
wabunge lakini vyama vyao vina uwakilishi Bungeni na kuwapa hadhi ya
kidiplomasia. Mheshimiwa Spika haiingii akilini kuona kiongozi wa
Kitaifa kama Profesa Ibrahim Lipumba ambaye chama chake kina wabunge
wengi bungeni na kinaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar
anakuwa hana hadhi ya ki-diplomasia.
Kwa upande mwingine
inashangaza kuona kiongozi wa kitaifa kama Dkt. Wilbroad Slaa ambaye
chama anachokiongoza kinaunda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia
anakuwa hana hadhi ya kidipolmasia wakati wabunge walioko chini yake
wana hadhi hiyo.Mheshimiwa Spika, viongozi wakuu wa vyama vya siasa
vyenye uwakilishi mkubwa bungeni ni viongozi wa Serikali watarajiwa.
Hivyo kupuuza itifaki na
ulinzi wao ni kuiweka nchi katika mtanziko na mashaka. Hili si jambo
ambalo mnaweza kuliunga mkono kwa sasa lakini ni jambo muhimu kwenu
kuelewa.
MAONI NA MAPENDEKEZO YA VIFUNGU MAHSUSI
Mamlaka ya Msajili wa Silaha
Mheshimiwa Spika,Mamlaka
na majukumu ya Msajili wa Silaha yametolewa chini ya kifungu cha 8(2)
cha muswada huu wa sheria ya usimamizi na udhibiti wa silaha. Lakini
kifungu hicho, hakijatoa mwongozo au mipaka ya utekelezaji wa majukumu
ya Msajili wa Silaha. Matokeo yake ni kwamba katika maeneo mbalimbali ya
sheria hii, Msajili amepewa mwanya mkubwa wa kuamua anavyotaka
(discretion).
Kwa mfano kifungu cha 17
(1) na (2) kinampa Msajili wa Silaha mamlaka ya kutoa kibali cha
kumiliki silaha kwa mtu yeyote kwa kipindi ambacho ataamua yeye mwenyewe
na kuweka masharti ya kibali hicho yeye mwenyewe. Aidha, Msajili
anaweza katika muda wowote kufuta kibali cha umiliki wa silaha.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inamtazamo kwamba, ni bora zaidi masharti ya utoaji
kibali cha muda, masharti ya muda au kipindi ambacho kibali hicho
kitakoma na masharti ya kufuta kibali yakawekwa na sheria na sio
kutegemea utashi wa Msajili wa Silaha. Kwa kufanya hivyo, mianya ya
rushwa au upendeleo au uonevu wa aina yoyote katika utekelezaji wa
majukumu ya Msajili wa silaha inaweza kuzibwa na kuepukwa.
Watu wasio na Sifa ya Kumiliki Silaha
Mheshimiwa Spika,Katika
kifungu cha 26(1) cha muswada huu ipo orodha ya mambo au tabia
zinazoweza kumkosesha mtu sifa ya kumiliki silaha. Miongoni mwa tabia
hizo ni pamoja na Ukorofi. Kwa kuwa tafsiri ya neno ukorofi ni
subjective , na kwa kuwa kila mtu anaweza kutafsiri ukorofi kwa namna
yake, hivyo msajili wa Silaha anaweza kuwa na tafsiri yake ya ukorofi
kutokana na hisia zake na kumnyima mtu leseni ya kumiliki silaha kwa
kisingizio kwamba mtu huyo ni mkorofi.
Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inashauri kwamba neno ukorofi litafsiriwe na sheria hii ili
kuondoa mkanganyiko wa tafsiri pindi sheria hii itakapoanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, Kifungu
26(2) cha muswada huu kinaeleza kwamba endapo msajili wa silaha
ataridhika kwamba kuna sababu za msingi za kuamini kwamba mtu hana sifa
ya kumiliki silaha, atatoa notisi ya maandishi akimtaka mtu huyo kufika
mbele yake katika muda na sehemu iliyotajwa katika notisi hiyo ili
kuonyesha ni kwa sababu gani asitangazwe kuwa hana sifa ya kumiliki
silaha. Aidha, ikiwa mtu aliyepewa notisi hiyo atashindwa kuhudhuria
katika muda na sehemu iliyotajwa katika notisi, Msajili wa silaha
atamtangaza mtu huyo kuwa hana sifa ya kumiliki silaha.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kwamba kifungi hiki kina mapungufu.
Mapungufu hayo ni pamoja na muda wa kufika mbele ya msajili kutowekwa na
sheria na badala yake kuachwa katika utashi (discretion) ya msajili wa
silaha; na sharti la kufika mbele ya msajili wa silaha mwenyewe
kujieleza kama mtu ana sifa ya kumiliki silaha iwapo kuna mashaka juu
yake.
Kambi Rasmi ya Upinzani
inashauri kwamba muda wa kufika mbele ya msajili uwekwe na sheria ili
kuziba mwanya wa uonevu unaoweza kutumika kwa kuweka muda mfupi ili
mtuhumiwa ashindwe kufika katika muda huo na kutangazwa kuwa hana sifa
ya kumiliki silaha. Aidha, sharti la kufika mbele ya Msajili mwenyewe
liondolewe na badala yake sheria iweke wasajili wasaidizi katika mikoa
ili kupunguza adha na ghrama za kusafiri kumfuata msajili wa Silaha
mmoja ambaye kwa vyovyote vile ofisi yake itakuwa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, Kifungu
cha 26(3) kinasema kwamba cheti cha kuonyesha uwezo, leseni na kibali
kilichotolewa kwa mtu aliyetangazwa kuwa hana sifa ya kumiliki silaha
vitapoteza uhalali wake kuanzia tarehe ya kutangazwa huko. Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inahoji, ni kwa nini Serikali itoe cheti cha
kuonyesha uwezo, leseni na kibali kwa mtu ambaye hana sifa?
Nasema hivi kwa sababu
ikiwa Serikali itakuwa makini tangu mwanzo mtu anapoomba leseni au
kibali cha kumiliki silaha basi uwezekano mtu huyo aliyekidhi vigezo
tangu mwanzo vya kumiliki silaha kupoteza sifa na kutangazwa kuwa hana
sifa utakuwa ni mdogo sana vinginevyo awe amekuwa kichaa ghafla.
Mheshimiwa Spika, Kifungu
cha 26(4) kinasema kwa pia kwamba mtu aliyetangazwa kuwa hana sifa ya
kumiliki silaha, basi atasalimisha katika kituo cha Polisi haraka
iwezekanavyo cheti cha kuonyesha uwezo, leseni na vibali vilivyotolewa
kwake na silaha pamoja na risasi zilizo katika umiliki wake.
Mheshimiwa Spika,Kambi
Rasmi ya Upinzani inaona kwamba huu unaweza kuwa ni uporaji wa hila wa
silaha za wananchi kwa kutumia sheria, kwa kuwa muswada huu haujatamka
ni hatua gani zitafuata baada ya mtu aliyetangazwa kuwa hana sifa za
kumiliki silaha atakaposalimisha silaha yake na nyaraka za umiliki
katika kituo cha polisi. Sheria hii ikiachwa kama ilivyo inaweza
kutumika kwa kulipiza visasi au kutekeleza maelekezo yenye nia mbaya.
Utoaji wa silaha na risasi kutoka katika ghala la umma au kituo cha Polisi
Mheshimiwa Spika, Kifungu
cha 29(1) cha muswada huu kinaeleza kwamba silaha au risasi
zilizohifadhiwa katika ghala la umma, kituo cha polisi au sehemu
nyingine yoyote iliyoelezewa na Msajili hazitatolewa humo isipokuwa kwa
kibali kilichosainiwa na msajili. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kuwe
na ugatuzi wa madaraka ili kibali cha kuondoa silaha katika ghala la
umma au sehemu nyingine yoyote kiweze kusainiwa na Wakuu wa Polisi wa
Mikoa hasa pale kunapotokea dharura mfano ujambazi, uasi, wanyama hatari
nk.
Masharti kwa Wauzaji wa Silaha
Mheshimiwa Spika,Kifungu
cha 33 cha muswada huu kinampa Waziri mamlaka makubwa ya kutunga kanuni
zitakazoweka masharti ya utoaji wa kibali cha muuzaji wa silaha,
masharti kuhusiana na eneo la biashara la muuzaji, masharti ya kutolewa
upya kwa kibali cha muuzaji na masharti ya kusitishwa, kufutwa kwa muda
kwa kibali cha muuzaji wa silaha.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inapendekeza masharti hayo yatajwe na sheria ili
kuziba mwanya wa Waziri kutumia madaraka yake vibaya kwa kuweka masharti
kandamizi au ya upendeleo kwa baadhi ya makundi ya wauzaji wa silaha.
Upekuzi na Ukamataji wa Silaha
Mheshimiwa Spika, Kifungu
cha 54 cha muswada huu kinasema kwamba “Hakuna mashtaka au hatua zozote
za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya Msajili au mtu mwingine yeyote
aliyeidhinishwa anayetekeleza majukumu yoyote chini ya sheria hii kwa
lolote atakalolitenda wa nia njema”
Mheshimiwa Spika, Hakuna
utendaji bora usiokuwa na mipaka. Kifungu hiki kinaweza kutumika vibaya
kwa kuwa kinatoa mwanya mkubwa kwa Msajili au afisa yeyote
aliyeidhinishwa kupekua au kukamata silaha kufanya jambo lolote hata
kama ni ovu kwa kisingizio cha “nia njema. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani
inapendekeza kwamba sheria hii imtake msajili au afisa aliyeidhinishwa
kuzingatia kanuni na taratibu za upekuzi na ukamataji, kwani kumiliki
silaha kihalali sio kosa la jinai hivyo upekuzi na ukamataji uzingatie
taratibu za kisheria hasa kwa wale wanaomiliki silaha kihalali.
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya marekebisho ya baadhi ya vifungu yataletwa katika jedwali
la marekebisho wakati wa Kamati ya Bunge zima.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Imekuwa
ni desturi kwa Serikali zilizoko madarakani kuleta miswada ya sheria
kwa ajili ya kulinda maslahi yake yenyewe bila kujali maslahi mapana ya
wananchi na taifa kwa jumla. Aidha, imekuwa ni desturi sheria nyingi
kupitishwa haraka hara bila kupata maoni ya wadau wengi jambo ambalo
husababisha sheria nyingi kupingwa kabla hata hazijaanza kutumika. Mfano
halisi ni Muswada huu kutoshirikisha wadau ipasavyo. Wadau wengi
walilalamika mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kwamba
hawakushirikishwa kabisa katika mchakato wa kuandaa muswada huu.
Kambi Rasmi ya Upinzani
inaihoji Serikali ni kwa nini inapuuza wadau katika sheria muhimu kama
hii? Je, Serikali haioni kuna athari kubwa kiulinzi na kiusalama kwa
kutowashirikisha wadau wakubwa wa silaha na risasi kama vile makampuni
ya ulinzi binafsi, na wafanyabiashara wakubwa wa silaha hapa nchini?
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza tena kwamba Amani na utulivu wa
nchi hii hautategeme tu uwepo wa sheria ya udhibiti na usimamizi wa
silaha na risasi bali uongozi unaozingatia misingi ya utawala bora,
haki, usawa, ukweli na usitawi wa jamii nzima kwa jumla. Aidha, ugumu wa
maisha unaosababishwa na umasikini uliokithiri kutokana na mfumuko wa
bei, elimu duni, maradhi, ukosefu wa ajira, ukosefu wa maji safi na
salama nk. ni viashiria vikubwa vya uvunjifu wa amani kuliko silaha na
risasi ambazo Serikali inafanya bidii kubwa kutungia sheria.
Mheshimiwa Spika,Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni bado inaitaka Serikali kukumbuka na kuzingatia
barabara masuwala manne muhimu iliyotahadharisha yasichezewe au
kufanyiwa mzaha kwani yanaweza kuliingiza taifa katika machafuko.
Masuala hayo ni kuchezea
haki ya mwananchi kujiandikisha kuwa mpiga kura, Kufanya Mzaha na uwepo
wa Tume Huru ya Uchaguzi, Matumizi ya Kisiasa ya Jeshi la Polisi na
Ulinzi wa Raia na Mali zao hususan ulinzi wa watu wenye ulemavu wa ngozi
(Albino).
Mheshimiwa Spika,Baada ya kusema hayo, kwaniaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba kuwasilisha.
Godbless Jonathan Lema (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
19 Machi, 2015

