https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    SERIKALI KUPELEKA BUNGENI MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA

    *Una sehemu 14 ikiwemo ya Mahakama ya Kadhi
    WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itawasilisha Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wenye sehemu 14 likiwemo suala la Mahakama ya Kadhi.

    Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, jana jioni (Jumatano, Machi 11, 2015) Waziri Mkuu alisema
    Serikali inakusudia kuwasilisha muswada huo kwenye mkutano ujao wa
    Bunge unaotarajiwa kuanza Jumanne ijayo, (Machi 17).

    Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasihi Watanzania waondoe hofu iliyoenezwa
    na tetesi kwamba muswada huo una lengo la kuiingiza mahakama hiyo
    kwenye Katiba Inayopendekezwa na kuwataka wazipuuze tetesi hizo.

    “Hakuna ukweli wowote kwenye jambo hilo kwa sababu Bunge la Katiba
    lilikwishavunjwa na Bunge lijalo halina mamlaka ya kufanya hivyo. Hili
    ni Bunge la sasa haliwezi kubadili maamuzi ya awali… Jambo hili halina
    ujanjaujanja au njama zozote za kuliingiza Kwenye Katiba
    Inayopendekezwa,” alisema.

    “Hizo ni hofu za kweli zilizosambaa na inategemea jinsi mtu
    alivyoelewa suala zima. Kikubwa ni kutambua kwamba Mahakama ya Kadhi
    zimekuwa zinafanya kazi hapa nchini tangu mwaka 2012 lakini kwa
    kuendeshwa na wao wenyewe na siyo Serikali,” alisema.

    Alisema kinachoombwa kwenye marekebisho hayo ya sheria ni kutambuliwa
    kwa maamuzi yanatolewa na Mahakama ya Kadhi pindi yanapofikishwa
    kwenye vyombo vya umma au taasisi za Serikali. “Sehemu ya tano ya
    muswada huo ndiyo inaongelea Mahakama ya Kadhi. Na mapendekezo yao
    yanaomba maamuzi yanayotolewa kuhusu ndoa, mirathi au talaka
    yanapokuja kwenye taasisi nyingine yaheshimiwe,” alifafanua Waziri
    Mkuu.

    Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema: “Kuna mama mmoja alipewa talaka na
    katika maamuzi ya talaka ile, alipaswa kupewa nyumba. Alipokwenda kwa
    Kamishna wa Ardhi ili abadilishe jina kutoka majina ya awali na kuwa
    la huyo mama akaulizwa haya maamuzi yametolewa wapi, sisi
    hatuyatambui… hili lilileta usumbufu mkubwa kwa wahusika.”

    Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu alisema kwa mara ya kwanza, suala la
    Mahakama ya Kadhi liliibuliwa mwaka 1998 na Bw. Augustine Lyatonga
    Mrema na Bw. Yusuph Ramia (marehemu) ambao walitaka Bunge lijadili
    hoja yao ya kutaka Serikali ianzishe mahakama hiyo.

    “Bunge liliunda Kamati iliyoongozwa na Bw. Arcado Ntagazwa na baada ya
    mjadala mrefu halikufikia tamati. Serikali ikalifuatilia lakini pia
    haikufikia mwisho. Mwaka 2005 likaingizwa kwenye Ilani ya Chama cha
    Mapinduzi na Chama kikaitaka Serikali ifuatilie kuona tatizo ni nini.”

    “Kwenye mkutano wa Bunge la Bajeti, tarehe 30 Juni 2009, Waziri wa
    Katiba na Sheria ndiye alikuja na hiyo hoja na kuahidi kuifuatilia
    Reinstatement Act ya mwaka 1964 sura ya 375 na kuona Serikali itafanya
    nini katika suala hilo.”

    “Wakati huo ndiyo nilikuwa nimeteuliwa Uwaziri Mkuu kwa hiyo nikaanza
    nalo kwa kuunda timu ya viongozi wa dini ili tulijadili kwa kina suala
    hili kwani kama Serikali kuna masuala ambayo inaamini ni lazima
    iendelee kuyasimamia na kubwa likiwa ni amani na utulivu wa nchi
    yetu,” alisema.

    Alisema katika vikao hivyo walikubaliana kwamba kuendelea kudai suala
    hilo liingizwe kwenye Katiba haikuwa sahihi kwa sababu ni suala la
    imani zaidi na kwa msingi huohuo, walikubaliana kwamba zianzishwe na
    wao wenyewe na kisha wazipangie majukumu ni nini zitafanya.

    “Tulikubaliana kwamba mahakama hizo zisiguse masuala ya jinai bali
    zihusu masuala ya binafsi tu ambayo ni ndoa, talaka, mirathi, malezi
    ya watoto na wakfu. Tulisema jambo hili liwe ni la hiari na lisiwe la
    lazima,” alisema.

    “Msingi wa mjadala ulikuwa mahakama hizi zisiwe kama Mahakama ya Ardhi au Mahakama ya Biashara kwamba mishahara na ofisi zao vigharimiwe na Serikali, hapana… kwa hiyo fikra kwamba Serikali ilikuwa inakataa kuzianzisha hazikuwa sahihi. Ndiyo maana Waislamu walikubali
    kuziansisha kwa hiari yao wenyewe na kwa gharama zao wenyewe,”
    alisema.

    “Nimeongea na Kadhi Mkuu hivi majuzi akaniambia kwamba hadi sasa
    mahakama hizo zimekwishaamua kesi zisizopungua 2,000 na zisizozidi
    3,000.”

    Akielezea juhudi za kukutana na wadau wa pande zote mbili, Waziri Mkuu
    alisema Februari 3, mwaka huu alikutana na Kamati ya Amani ya Mkoa wa
    Dar es Salaam yenye wajumbe 25 ambao ni Waislamu na wajumbe 25 ni
    Wakristo lakini katika kikao hicho walihudhuria wajumbe 55.

    “Wao walijadiliana peke yao, kisha wakakutanisha pamoja na mimi
    nikapewa majumuisho ya mkutano huo. Lakini wakashauri kwamba uitishwe mkutano mkubwa zaidi wenye wadau kutoka nchini nzima ili nao wajadili suala hili. Ndipo Machi 3, mwaka huu nikakutana na Kamati ya Maadili na Haki za Binadamu iliyokuwa na wajumbe 55 wa taasisi tofauti za
    Kiislamu na wajumbe 34 wa Madhehebu ya Dini ya Kikristo.”

    “Mkutano ulikuwa mkali na ubishani mwingi wengine wakidhani kwamba
    wameitwa kushiriki kikao hicho ili kubariki suala la Makahama ya Kadhi
    liingizwe kwenye Katiba inayopendekezwa lakini hatimaye, tulielewana
    na kufikia muafaka juu ya marekebisho yanayotarajiwa,” alisema.

    IMETOLEWA NA
    OFISI YA WAZIRI MKUU,
    2 MTAA WA MAGOGONI,
    S.  L. P. 3021,
    11410 DAR ES SALAAM
    ALHAMISI, MACHI 12, 2015.
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SERIKALI KUPELEKA BUNGENI MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top