Meneja
Mawasiliano wa Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) Innocent Mungy
(Kulia) akiongea na wadau wa Sanaa (hawako pichani) wakati akiwasilisha
mada kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa wasanii kwenye
Jukwaa la Sanaa lililofanyika Jumanne ya wiki hii makao makuu ya Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) Ilala, Sharif Shamba. Kushoto ni Mwanasheria
wa BASATA Deogratius Nchimbi.
Mwanasheria
wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Deogratius Nchimbi (Kushoto)
akiongea jambo na wadau wa Sanaa (hawako pichani) mapema wiki hii wakati
akihitimisha mjadala kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa
wasanii uliowasilishwa na Meneja Mawasiliano wa mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) kupitia programu ya Jukwaa la Sanaa ya Baraza hilo
kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala, Sharif Shamba jijini Dar es
Salaam.
Mmoja
wa wadau wa Jukwaa la Sanaa akiuliza swali kwa Meneja mawasiliano wa
TCRA juu ya athari za sheria mpya ya mitandao ya kijamii kwa wasanii na
waandishi wa habari.
Sehemu ya wadau wa Sanaa waliohudhuria programu ya Jukwaa la Sanaa ya Baraza la Sanaa la Taifa mapema wiki hii.
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) na mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA)
mapema wiki hii wamelaani matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii
miongoni mwa wasanii wakati wa programu ya Jukwaa la Sanaa iliyofanyika
makao makuu ya Baraza hilo yaliyoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es
Salaam.
Akiongea
wakati akiwasilisha mada iliyohusu ‘Matumizi sahihi ya mitandao ya
kijamii kwa wasanii’, Meneja mawasiliano wa TCRA Innocent Mungy alisema
kuwa wasanii ni kioo cha jamii hivyo kwa namna yoyote ile hawapaswi kuwa
sehemu ya uharibifu wa jamii inayowazunguka au kuharibu wajihi
(taswira) yao kwa jamii yao.
“Unapokuwa
kioo cha jamii, unategemewa kuishi kwa kuwa mfano katika jamii yako.
Vijana wengi wanaiga kutoka kwa wasanii ambao ni maarufu. Tunatarajia
wasanii wawe mfano kwao” alisisitiza Mungi.
Aliongeza
kwamba, msanii anapotumia mitandao ya kijamii kwa kuweka picha chafu,
zisizo na maadili au kitu chochote kisicho na staha ni kuchafua wajihi
wake mbele ya jamii na hili linampotezea fursa nyingi za kibiashara na
kiuchumi maana hakuna kampuni au asasi itakayopenda kufanya kazi na
msanii mwenye sifa mbovu.
“Wasanii
wanapotumia hovyo mitandao ya kijamii wanachafua wajihi wao katika
jamii. Wanajikosesha fursa za kimapato. Mfano; mfanyabiashara anapotaka
kutangaza shule yake ya watoto wa awali hawezi kutumia msanii mwenye
wajihi mchafu na unaoharibu watoto” aliongeza Mungy.
Alizidi
kueleza kwamba wasanii hawana budi kutumia mitandao hii ya kijamii
hususan facebook, twitter, instargram, u-tube na kadhalika katika
kujitangaza na kuuza kazi zao na zaidi kutenga muda mwingi kutumikia
jamii.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa na Masoko wa BASATA,
Vivian Shalua alisema kwamba Baraza hilo muda wote limekuwa likisisitiza
maadili mema miongoni mwa wasanii maana vijana wengi huwaangalia kama
mfano katika maisha yao.
“Kila
mara BASATA limekuwa likisisitiza maadili kwa wasanii wote. Kazi hii ni
ngumu na inataka wadau wote kushiriki katika kunyoosha maadili ya
wasanii na vijana kwa ujumla” alimalizia Shalua