Mtanzania anayedaiwa kuhusika katika shambulizi la kigaidi lililoua watu 148 katika Chuo Kikuu cha Garissa – Kenya, Rashid Charles Mberesero, jana alifikishwa mahakamani na kuwekwa kizuizini kwa mwezi mmoja wakati polisi wakiendelea kukusanya ushahidi dhidi yake.
Mtuhumiwa
huyo ambaye pia anafahamika kwa jina la Rehani Dida alirejeshwa Nairobi
kutoka Garissa alikopelekwa awali kwa ajili ya kuhojiwa baada ya kukiri
kujihusisha na kundi la Al- Shabaab.
Mahakama jijini
Nairobi ilisema jana kuwa mtuhumiwa huyo ambaye hakutakiwa kujibu tuhuma
hizo na wenzake wanne watalazimika kuwa chini ya uchunguzi mkali wa
polisi kwa kipindi cha mwezi mmoja na baadaye wanaweza kusomewa mashtaka
ya kuhusika katika shambulizi hilo lililoua watu hao, wengi wao wakiwa
ni wanafunzi.
Haikufahamika mara moja sababu za
kuamuliwa kuwekwa kizuizini kwa muda huo mbali ya taarifa kueleza kuwa
‘watashikiliwa na polisi tena katika kituo cha siri’.
Mwendesha
Mashtaka, Daniel Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa Mtanzania huyo
ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano, alikuwa amepanga safari ya
kuelekea Somalia kwa ajili ya kujiunga na makundi ya kigaidi.
Watuhumiwa hao ni kati ya 14 waliotiwa mbaroni hivi karibuni baada ya shambulizi hilo la kigaidi.
Mahakama hiyo pia imewaamuru washukiwa wengine kuendelea kushikiliwa na polisi kwa muda wa siku tano hadi 15.
Awali,
Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa polisi walikuwa wakifuatilia kwa
karibu uhusiano baina ya wale waliofanya shambulizi hilo na
mfanyabiashara mmoja anayemiliki hoteli mjini Garissa. Inasemekana kuwa
watu waliotekeleza shambulio hilo walikuwa wamelala katika hoteli hiyo.
Hakula chakula cha shule
Wanafunzi
wa Shule ya Sekondari ya Kigwe, mkoani Dodoma alipokuwa akisema
Mberesero baada ya kufaulu kutoka Gonja, wamesema hakuwahi kula chakula
chochote shuleni kwa kipindi cha mwezi mmoja aliokaa akisubiri
kuhamishwa na kubadilishiwa mchepuo wa masomo.
Wakizungumza
na mwandishi wetu shuleni hapo jana, wanafunzi wa kidato cha tano,
Yoram James na Thomas Godwin, walisema siku zote alizoishi shuleni hapo
alikuwa akila kwa mama lishe jirani na shule hiyo.
“Lakini alikuwa na mkarimu kwetu wakati mwingine alikuwa akitununulia maandazi ya kunywea chai,” alisema Yoram.
Hata hivyo, walisema kutokana na upole wake, jinsi anavyoongea na kutumia muda mrefu msikitini, walimpa jina la Ustaadhi.
“Alikuwa akienda mjini mara kwa mara, nadhani alikuwa akiomba ruhusa kwa walimu au alikuwa akitoroka,” alisema Thomas.
Thomas alisema Rashid alikuwa akipenda kucheza mpira wa miguu kwa hiyo alitenga muda wake kwa ajili hiyo.
Uhamisho wake
Mkuu
wa Shule hiyo, Ramadhan Bakari alisema ofisi ya elimu mkoa ilituma
taarifa ya kuwataka wanafunzi wanaopenda kubadilisha mchepuo kuandika
barua ya maombi.
“Rashid alikuwa ni miongoni mwa
wanafunzi watano walioomba kubadilishiwa mchepuo kutoka Sanaa kwenda
Sayansi, walikubaliwa wanne akiwamo yeye,” alisema Bakari.
Hata hivyo, mwalimu huyo alisema Rashid alikuwa akihangaika ahamishiwe Shule ya Sekondari ya Bihawana, tangu aliporipoti Kigwe.
“Hatuwezi kuzungumza kuhusu tabia zake maana hapa hakuishi siku nyingi, alikuwa kama yuko njiani,” alisema.
“Aliondoka hapa shuleni kwenda Bihawana Agosti 19, mwaka jana baada ya taratibu kukamilika,” alisema.
Uvumi wasambazwa
Hofu
imetanda katika maeneo mbalimbali baada ya kusambazwa ujumbe kwenye
simu na mitandao ya kijamii ukidaiwa kutolewa na Umoja wa Mataifa (UN)
kutahadharisha watumishi wake waepuke kukaa katika makundi makubwa na
mikusanyiko katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha leo kuepuka
mashambulizi ya kigaidi.
Hata hivyo, Msemaji wa UN, Usiah Ledama alikanusha umoja huo kuhusika na ujumbe huo akisema ni feki na hauna ukweli wowote.
Kaimu
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Diwani Athumani alisema
hata kama ujumbe huo ni feki, bado Jeshi la Polisi linachukua tahadhari
kuhakikisha Taifa linakuwa salama.
“Huo ujumbe uwe feki
au wa kweli, lazima tuchukue tahadhari, Tanzania si kisiwa, tutakuwa
salama kwa asilimia 100, kwa hiyo ulinzi unaimarishwa,” alisema.
Alisema
ni lazima kila mtu awe mlinzi wa mwenzake na ahakikishe kuwa anakuwa
mzalendo kwa kutoa taarifa zozote ambazo anadhani zitalisaidia Jeshi la
Polisi katika ulinzi.