HATIMAYE Jumatatu ya wiki hii dunia ilishuhudia ndege inayotumia
nguvu ya jua ikifanya safari yake kuzunguka dunia kwa mara ya kwanza
katika historia ya dunia.
Ndege hiyo iliyopewa jina la Solar Impulse-2, ilianzia safari yake
Abu Dhabi, Umoja wa Falme ya nchi za Kiarabu kuelekea Muscat nchini Oman
na baadaye itaendelea na safari zake kuzunguka dunia hadi China.
Ikiwa
na rubani wake, Andre Borschbeg, ambaye pia ni mhandisi na
mfanyabiashara, ndege hiyo ilikanyaga ardhi ya Oman bada ya masaa 12 ya
kuruka hewani.
Inakadiriwa kwamba miezi mitano baadaye ndege hiyo inatazamiwa kwenda
bara moja hadi jingine ikikatiza katika Bahari kuu za Pacific na
Atlantic. “Na hakika tumefanikiwa.
Solar Impulse imetua ardhini,”
alisema rubani baada ya ndege hiyo yenye rubani mmoja kukanyaga lami.
Ndege hiyo pia ina vifaa kadhaa vya kujiokolea ikiwa ni pamoja na
kumwezesha mtu aliyejiokoa kukaa baharani kwa muda hadi atakapookolewa.
Borschberg atakuwa anafanya kazi ya kurusha ndege hiyo sambamba na
mwenzake, raia wa Uswisi, Bertrand Piccard.
Ndege hiyo inatazamiwa kuwa
na vituo kadhaa duniani kwa ajili ya kupumzika na kufanya matengenezo
muhimu kama yatahitajika na pia kusambaza kampeni ya kuhamasisha
tekonolojia isiyoharibu mazingira, kwa maana ya zile zisizotumia mafuta.
Kabla ya kuruka Angani, Borschberg aliiambia BBC: “Nina uhakika
kwamba tuna ndege nzuri na maalumu ambayo itatuvusha kwenye bahari
nyingi kuu.
“Tunaweza kuruka kwa siku tano, usiku na mchana mfululizo na
itakuwa ni changamoto kubwa, na miezi miwili ijayo tutaruka kwenda
China ili kujifunza zaidi na kufanya maandalizi muhimu,” anasema.
Safari ya Jumatatu kwenda Oman ilikuwa ni ya km 400 na kuchukua saa
12 kwa kuwa ndege hiyo haina kasi kama zile zinazotumia mafuta.
Wazo la
kutengeneza ndege hiyo linakwenda sambamba na imani kwamba matumizi ya
vifaa vinavyotumia nguvu ya jua vitakuwa vingi duniani ifikapo mwaka
2050 ambapo matumizi ya vifaa vya mafuta vinavyochangia kuharibu tabaka
la hewa la dunia yatakuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Inatazamiwa kwamba vifaa vya umeme jua vitakuwa vimeshuka sana bei
kufikia muda huo kwani kwa sasa vifaa vingi vya umeme jua (solar)
vimeshuka bei kwa asilimia 70 na vinatazamiwa kuzidi kushuka.
Benki ya
Holland inaamini kwamba umeme wa nguvu ya jua utakuwa rahisi kadri
teknolojia inavyozidi kuimarika na kufikia mwaka 2020 bnki hiyo inaamini
umeme jua utakuwa rahisi sawa na umeme wa gesi.
Nchini Uingereza, kampuni ya kutengeneza vifaa vya umeme jua inaamini
kwamba baada ya miezi 18 ijayo inaweza kupambana kwenye soko na vifaa
vya kuzalisha umeme kwa upepo.
Kadhalika inaamini kwamba miaka michache
baadaye ‘itakula sahani moja’ na umeme wa gesi kwa upande wa urahisi wa
bei. Nchini Marekani kwa sasa kazi zinazotokana na umeme jua zimeanza
kuzidi kazi zinazotokana na makaa ya mawe.
Mapunduzi katika matumizi ya vifaa vya umeme jua yameimarika baada ya
serikali za nchi nyingi kuweka ruzuku kwenye uitengenezaji wa vifaa
hivyo, hatua ya makamuni mengi kuwekeza kwenye eneo hilo.
Ongezeko la
umeme jua linachukuliwa kama hatua muhimu katika kupambana na matatizo
ya mabadiliko ya tabianchi.
Ndege zinazotumia nguvu ya jua zimeshatokea nchini Marekani ya kwanza
ilipaa angani mwaka 2013 lakini ndege yenye kiwango cha kukatiza masafa
ndio sasa imezinduliwa Jumatatu ya wiki hii ikiwa na uwezo na kubwa
kuliko Solar Impulse-1. Modeli hii mpya ina bawa lenye urefu wa mita 72,
ambalo ni kubwa kuliko jumbo jet 747.
Hata hivyo bawa hili lina uzito wa tani 2.3 pekee. Ndege hii ilikuwa
na paneli 17,000 zilizopangwa kwenye mabawa, ambazo hufanya kazi ya
kupeleka umeme kwenye betri maalumu inayowezesha ndege hii kutembea
usiku mzima bila kuishiwa nguvu.
Kuiwezesha ndege kuruka usiku kusiko na
jua litakuwa jambo muhimu pia kama kuna hitaji la kwenda masafa marefu
na kukatiza bahari kuu za Pacific na Atlantic na hasa ikizingatiwa
kwamba kasi ya ndege hii si kubwa kulinganisha na zinazotumia mafuta.
Andre Borschberg, mhandisi na rubani wa zamani wa ndege za kijeshi
amekuwa kwa muda mrefu akifanya biashara ya teknolojia ya kompyuta.
Rubani mwenzake, Bertrand Piccard, anakumbukwa zaidi na wengi kuhusu
uwezo wake wa kurusha mabaluni angani.
“Niliwa na ndoto hii miaka 16 iliyopita ya kuruka hewani bika kutumia
mafuta na sasa imewezekana,” anasema Borschberg. Wazo la Borschberg la
kuruka hewani na ndege isiyotumia mafuta lilikuwa sana na wazo la
mtaalamu wa kuruka kwa parachuti, Piccard, ambaye naye alikuwa na wazo
kutuka hewani na ndege isiyotumia mafuta.
Piccard alipata wazo hilo mwaka 1999 alipokuwa na ziara ya kuzunguka
dunia kwa mara ya kwanza kwa kutumia parachuti.
Akiwa katika safari hiyo
aliona jinsi jua lilivyoangaza na kuhisi kuwa nguvu ya jua inaweza
kukamilisha ndoto yake ya kuruka angani kwa kutumia chombo ambacho
hakitumii mafuta wala kuchafua kuchafua anga.
Borschberg na Piccard waliungana na kuanza kutekeleza mawazo yake kwa
vitendo jambo lililofanikisha kupatikana kwa ndenge hiyo inayoweka
alama ya mafanikio makubwa ya kutumia maarifa katika karne ya 21 na
kuendelea kuboresha utaalamu wa kutengeneza ndege ili kuwaenzi
wanasayansi wa zamani.
“Ndege ya kwanza iligunduliwa mwaka 1903 na Marekani Orville na
Wilber mwaka 1903 lakini hawakujua kuwa ipo siku ndege itakuwas uwezo wa
kuvuka Bahari ya Atlantic na kwenda masafa marefu.
Hata hivyo mwaka
1927 mwanasayansi Charles Lindbergh aliendeleza wazo hilo na kutengeneza
ndege aliyoruka nayo kutoka New York hadi Paris,” Borschberg alisema.
Aliendelea kusema, “ni matarajio yetu kuwa mradi wa Solar Impulse
utakuwa alama ya dunia na kujenga uelewa kuhusu matumizi yetu ya
nishati.” Mradi huo wa kutengeneza ndege inayotumia nishati ya jua
umejumuisha watu zaidi ya 70 wahandisi 50, madaktari, wataalamu wa
uboharia na wanasayansi wa kompyuta.
Pamoja na mafanikio makubwa yaliyofikiwa Borschberg anasema hatarajii
kuwa ndege za biashara zitatumia nishati ya jua katika siku za hivi
karibuni kwa kuwa unahitajika utaalamu mkubwa na fedha nyingi kuwekeza
katika mradi huo.
“Nishati ya jua inaweza kuwa chanzo cha nishati cha
nyongeza, lakini bila ya kuwa na ugunduzi mkubwa sioni jambo hilo
likitokea,” Borschberg alisema.
Hata hivyo Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga, ambacho
kinawakilisha ndege zote za biashara 230, kina lengo la kuzalisha ndege
zisizozalisha gesi ya kaboni ifikapo mwaka 2050.
Makala haya yameandikwa kutumia vyanzo mbalimbali vya habari kwa mtandao kompyuta.