WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imeanzisha Kurugenzi ya Wauguzi na Wakunga katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili kwenye utoaji wa huduma kwa umma.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Mei 5, 2015), wakati akizungumza wauguzi na wakunga pamoja na wakazi wa mkoa wa Mara kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mkendo, mjini Musoma.
“Nina taarifa kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha (2015/2016), Kurugenzi hiyo itakuwa na bajeti yake yenyewe itakayotumika kuboresha huduma za wauguzi na wakunga nchini. Haya yote yanafanyika kwa kuwa Serikali inatambua na kuthamini shughuli za wauguzi na wakunga hapa nchini,” alisema.
Alisema mafanikio yaliyofikiwa ya kupunguza vifo vya watoto na vifo vya wanawake yamechangiwa na kazi nzuri zinazofanywa na wakunga licha ya kuwa kada hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi.
Alisema ili kukidhi mahitaji ya wakunga nchini, Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na fani ya uuguzi na ukunga. Akitolea mfano, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2009 tulikuwa na wanafunzi wa uuguzi na ukunga 617 wa ngazi ya Cheti na 925 wa ngazi ya Diploma. Kufikia mwaka 2014 idadi hiyo iliongezeka kufikia wanafunzi 2,566 wa Cheti sawa na ongezeko la asilimia 315 na wanafunzi 2,294 wa Diploma sawa na ongezeko la asilimia 141 katika kipindi cha miaka mitano.”
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhara hiyo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi Jamii, Dk. Stephen Kebwe alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika ambazo zimeweza kupunguza vifo vya watoto na kuvuka Malengo ya Milenia.
Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wanaume wa mkoa huo na wanaume wote nchini kukubali kutumia njia za uzazi wa mpango ili wawasadie wenza wao kuwa na afya imara. Pia aliwataka waachane na dhana potofu za mitaani bali wafuate tiba na huduma sahihi uzazi wa mpango kwenye vituo vya afya.
“Inashangaza kuona baadhi ya wanaume wanawaacha wake zao eti kwa sababu hawazai, lakini wakiwaacha baada ya muda unasikia yule mama amepata ujauzito, hapo kosa ni la nani?” aliuliza.
“Pia ninawasihi akinababa waachane na dhana potofu kuhusu njia ya kufunga kizazi. Ninawahimiza washiriki njia hii ya kufunga kizazi wanaposhauriwa kufanya hivyo kwa sababu kufunga ule mrija hakumuondolei mwanaume hadhi ya kufanya tendo la ndoa, bado inawezekana hata baada ya kufunga mrija,” alisisitiza.
Mapema, akitoa salamu kwenye maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkazi wa taasisi ya Mama Ye, Bw. Craig Ferla aliitaka Serikali na wadau waliangalie suala la vifo vya akinamama na watoto kwa jicho la tofauti na kulipigia kelele zaidi ili uwekezaji kwenye fani ya ukunga na uuguzi uweze kuongezwa.
Bw. Ferla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Utepe Mweupe wa Muungano wa Uzazi Salama Tanzania, alisema Serikali na wadau mbalimbali wamekuwa wakipigia kelele idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani lakini hakuna mtu anayesema chochote kuhusu vifo vya wanawake na watoto wachanga.
“Watu wanapiga kelele kuwa Taifa limepoteza watu 972 kati ya Januari na Aprili mwaka huu, lakini hatujui kwamba katika kipindi hicho hicho Taifa limepoteza wanawake na watoto 15,000 kutokana na matatizo ya uzazi na hii ni mara 15 zaidi lakini hakuna anayepiga kelele,” alifafanua.
Alisema wanawake 8,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na uzazi wakati watoto 40,000 hupoteza maisha wakiwa katika mwezi wao wa kwanza duniani. “Vifo vya ebola tangu ianze vimefikia 10,000 lakini dunia nzima imeitikia lakini hivi vya akinamama hakuna anayesema chochote.”
“Kuna tatizo jingine ambalo linakwenda kimyakimya nalo ni la vifo vya watoto wanaozaliwa wafu. Hawa wanafikia 47,000 kwa mwaka ambao ni karibu watoto 15,000 kwa miezi minne lakini nalo pia hakuna anayelisemea licha ya kuwa ni janga kubwa kitaifa,” aliongeza.
“Ninaiomba Serikali na wadau wawekeze zaidi katika kada ya wakunga ili tuweze kuokoa maisha ya akinamama na watoto,” alisema Mkurugenzi huyo ambaye kwa muda wote alitumia Kiswahili fasaha na kuufanya mkutano mzima umshangilie kwa nguvu.