WINGA wa Yanga SC, Simon Msuva ameondoka leo kwenda Afrika Kusni kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Orlando Pirates ya huko. Msuva aliomba ruhusa kwa uongozi wa Yanga jana wakamkatalia, lakini leo amepanda ndege kwenda Johannesburg. Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba Pirates walileta mwaliko wa majaribio kwa ajili ya Msuva, lakini wakamuambia asubiri amalize Ligi Kuu atakwenda. “Najua kuna hiyo safari, ila aliambiwa asuburi amalize Ligi atakwenda, kama amekwenda bila ruhusa atakuwa amefanya makosa,”amesema Muro.
Msuva aliyeibukia akademi ya Azam FC, ameondoka akiwa tayari ameipa Yanga SC ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, huku pia akiwa anaongoza kwa mabao, 17 akifuatiwa na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Amissi Tambwe mabao 14. Tangu ajiunge na Yanga SC mwaka 2012 akitokea Moro United, Msuva ameifungia timu hiyo mabao 35 jumla katika mechi 102 za mashindano yote.