Timu ya Mbeya City bado ipo njia panda kuhusu kushiriki au kuto shiriki michuano ya Kagame Cup ambayo inatarajia kuanza kutimua vumbi hivi klaribuni jiji Dar es Salaam, lakini mpaka kufikia wakati huu timu ya timu hiyo bado haina taarifa rasmi ya mwaliko kutoka CECAFA juu ya ushiriki wao kwenye michuano hiyo.
Afisa habari wa Mbeya City Dismas Ten amethibitisha kutopokea taarifa rasmi kutoka CECAFA ya kualikwa kushiriki michuano hiyo inayoshirikisha vilabu bingwa Afrika Mashariki na Kati.
“Kama unavyofahamu mashindano ya Kagame yanataka timu tatu kwahiyo sisi bado hatujapata taarifa na kama ikitokea tukapata basi tutatangaza na tutakuwa tayari kwa kile ambacho wao watakuwa wamekisema kwetu sisi”, amesema Ten.
“Huwezi kushiriki mashindano ya Kagame kama hujapewa taarifa rasmi kutoka Shirikisho la vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwahiyo sisi tunasubiri taarifa yao, kama watatuletea sisi tutashiriki”, ameeleza.
“Haya ni mashindano na yana watu ambao wanayasimamia na wanajua ni timu zipi zinapaswa kushiriki lakini sisi kama tunajua hilo huwezi kwenda kwenye mashindano hujapata mwaliko rasmi. Unaweza ukaenda na ukageuka mtazamaji, kwahiyo ni vizuri kwenda na taratibu na kanuni zilizopo kwasababu soka linahitaji pia uende na kanuni na taratibu ili kuweza kufanikisha kile ambacho kinakuwa kipo mbele yako. Sisi tunawasubiri ila timu yetu iko sawa”, amefafanua.
Nchi mwenyeji wa michuano ya Kagame hupewa nafasi ya kutoa timu tatu kushiriki michuano hiyo na kwa maana hiyo, Mbeya City ndiyo timu inayopewa nafasi ya kushiriki mashindano hayo kwasababu ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimu wa ligi wa 2013-2014 ambao ndio unaotumiwa kama kigezo cha kuwapata washiriki wa michuano hiyo.
Timu nyingine ambazo zinanafasi ya kushiriki michuano hiyo kutoka Tanzania ni pamoja na Azam FC ambayo ndio ilikuwa bingwa wa msimu huo na Yanga iliyomailiza nafasi ya pili.