TFF inapaswa kutuambia mchakato wa kuwapata wanao wania tuzo ulifanyikaje, vigezo gani vilizingatiwa kupendekeza majina ya watu wanaowania tuzo hizo. Kwasababu ulimwenguni kote waandishi wa habari za michezo ndio wanatumiwa kupendekeza majina na baade wao ndio wanapiga kura kuchagua nani anastahili kupewa tuzo.
Kwa nini waandishi wa habari za michezo ndio wanaotumiwa kupiga kura ya kuchagua mshindi wa tuzo? Waandishi ndiyo pekee wanye kumbukumbu ya kilakitu ambacho kimeendelea viwanjani nani amefanya nini nanani amefanya vile. Lakini unapoibuka na kutoa majina yako ya watu wanaowania tuzo bila kutuambia umezingatia vigezo gani unakuwa hututendei haki.
Shida ya tuzo hizi siyo waliochukua tuzo, bali waliopendekeza majina ya wawania tuzo hizo. Tukiwalaumu waliochukua tuzo tunakuwa tunawaonea maana wao waliwekwa tu kama ambavyo hata wewe au mimi ningewekwa. Havikutumika vigezo madhubuti vya kuwapata hawa washindania tuzo ndiyo maana wengi wao wamelalamikiwa baada ya kushinda tuzo hizo.
Makosa yalianza tangu hatua ya kupendekeza majina ya watu wanaowania tuzo hizo, hapa ndipo madudu yote yalianzia. Watu wamekutana wameshasahau namna ambavyo mechi zilichezwa na viwango vilivyooneshwa na wachezaji, hawana data wala facts waka teua tu majina ili kujaza nafasi. Na hapo ndipo makosa yote yalipofanyika lakini kilichotokea siku ya ugawaji tuzo ilikuwa ni mwisho lakini makosa yalikuwa huku mwanzo.
Haya ni matokeo ya kutokuwa na watu makini kwenye bodi ya ligi ambao wangekaa chini na kuangalia ni utaratibu gani utumike ili kuwapata watu sahihi wanao stahili kuwania tuzo hizo. Hata TFF ambao ndiyo dira ya soka la Tanzania hakukuwa na umakini juu ya hili kawasababu wao ndio wenye mamlaka ya mwisho, kwanini wasiombe ufafanuzi wa vigezo vilivyotumiwa kuwapata hawa watu, kukosa watu makini wa kufanya hivyo ndio maana haya yote yanatokea.
Tukianza na golikipa bora wa msimu ambaye ni Shabani Kado, tunahitaji kuambiwa idadi ya mechi ambazo amecheza, aliokoa michomo mingapi ambayo ilikuwa inaelekea langoni, na vitu vingine siyo kutuwekea tu pale Kado anawania nafasi ya golikipa bora bila kutuambia kwanini yupo pale kuwania tuzo ya golikipa bora wakati haujatueleza ubora wake ni upi.
Kwasababu hata timu yake (Coastal Union) aliyokuwa anaitumikia hadi kufikia hatua anatajwa kwenye orodha ya kuwania tuzo tayari hayupo pale kwasababu amenyimwa mkataba mpya. Sasa kwa akili ya kawaida tu, ulishawahi kuona wapi mchezaji bora anaachwa na timu yake atimke kikosi bure? Kumbuka huyu ndiye mshindi wa tuzo ya golikipa bora lakini timu yake ambayo ameitumikia kwa muda mrefu na wanafahamu vyema kiwango chake lakini hawana hata mpango wa kumuongezea mkataba na anaondoka bure.
Ukija kwenye upande wa makocha, kulikuwa na makocha wawili wa kigeni ambao ni Goran Kopunovic (Simba SC) na Hans van der Pluijm (Yanga), sasa kama mpango ulikuwa ni kuwafanya makocha wazawa kuwa bora kwa kuwapa tuzo ambazo hawastahili sidhani kama tunawasaidia. Na kwa hili kama makocha wa kigeni pia hatuoni mchango wao, tunaona kwamba hawastahili kupata tuzo kama hii basi hakuna sababu ya kuwaweka kwenye kipengele hiki kwasababu tunawadhalilisha bure tu.
Nchi nzima ya wapenda michezo ilikuwa inajua nani anastahili kuchukuwa tuzo hii ya kama kocha bora wa msimu ukiangalia takwimu zinavyoonesha, na ndio maana nikasema mapema kuwa, waandishi wa habari za michezo wanajua vizuri takwimu za kila kinachoendelea kwenye soka kwa kila mchezo. Sasa mkikutana barazani mkaanza kujadiliana nani achukue tuzo wakati hamna takwimu matokeo yake ndio haya tunayoyaona.
Ili tuwe waungwana hebu tuchukue takwimu za makocha wote watatu, Makata, Van Pluijm na Kopunovic tuziweke mezani halafu tuziache zizungumze tuone takwimu za nani zitaibuka kidedea. Van Pluijm aliiongoza Yanga kwa jumla ya mechi 19 za ligi kuu, Kopunovic akaichukua Simba na kuiongoza kucheza mechi 18 za ligi wakati Mkata yeye alikuwa kocha wa Tanzania Preisons kwa mechi nane. Hapa sitaki kusema nani alishinda mechi ngapi, akatoka sare mara ngapi na alipoteza mechi ngapi maana nahisi aibu.
Ukiachilia mechi za ligi ambazo ndio zimetumika kupima ubora wa makocha hawa, kuna makocha wawili kati ya hao walishiriki michuano mingine tofauti na hiyo ya ligi kuu Tanzania bara. Hawa ni Van Pluijm na Kopunovic ambao walishiriki Mapinduzi Cup kule Zanzibar. Lakini Van Pluijm yeye timu yake ilishiriki michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika, sasa tunapopima ubora wa kocha tunaangalia nini? Tulipaswa kuambiwa maana inawezekana kuna vitu vingine ambavyo sisi hatuvijui.
Ukiangalia majina yote ambayo yalikuwa yakiwania tuzo kwa nafasi za wachezaji hakukuwa na jina hata moja la mchezaji wa kigeni, hivi hili linawezekanaje? Basi kama tuliona watawafunika wachezaji wetu na lengo letu sisi ni kuhakikisha wachezaji wetu wanapata tuzo basi ingekuwa ni busara kama kingekuwepo kipengele cha wachezaji wakigeni ili wapambane wao wenyewe. Lakini kutowapa nafasi kabisa tunakuwa hatuwatendei haki kwasababu na wao ni sehemu ya soka la Tanzania na wanamchango wao.
Unawezaje kuwa na makocha wa kigeni kwenye kipengele kimoja na makocha wakizalendo halafu wakati huohuo kwenye vipengele vya wachezaji unawanyima fursa wachezaji wa kigeni? Hili nalo halikubaliki, kwa staili hii hatuwajengi wachezaji wetu bali tunawabeba.
Kitu cha kufurahisha ni pale wanaposema kwamba, katika kuwapata waliokuwa wakiwania tuzo suala la nidhamu pia lilizingatiwa, sawa wala sina ubishi na hilo lakini nadhani kikubwa ni uwezo wa mchezaji au timu. Huwezi ukatuletea mchezaji, kocha au mwamuzi ukasema ni bora wakati tunajua fika anauwezo mdogo halafu ukatuambia amepewa tuzo kwasababu ananidhamu hapo hatuwezi kukubali hata kidogo.
Mimi ninaona kuna haja ya ushirikishwaji wa wadau wa soka kwenye ugawaji wa tuzo hizi. Maana yangu ni kwamba ikiwezekana washindi wa tuzo hizi wapatikane kwa kura za wadau hasa waandishi wa habari za michezo ili haki itendeke kwasababu hakuna haja ya kuwaweka watu watatu kwenye kipengele kimoja halafu mwisho wa siku wewe mwenyewe tena unachagua mshindi bila kutuambia umempataje huyo mshindi wako. Kama ni hivyo bora umuweke mmoja ili asubiri siku ya kuchua tuzo awe akijua tuzo ni yakwake na hakuna mwingine anayeiwania.
Kwa hili TFF mnalipaka matope soka la Tanzania badala ya kulisaidia, hebu ifikie mahala twende kama dunia inavyotaka. Tumeshuhudia mara nyingi ugawaji wa tuzo za wachezaji mbalimbali na kwenye mashindano makubwa, tunajua utaratibu unaotumika. Msitupelekepele tu ilimradi siku zisogee na maisha yaende.