Dar es Salaam. Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa amesema kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow imekijengea chama hicho chuki kwa wananchi na hivyo kinahitaji mgombea anayekubalika ili kishinde kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Msekwa, ambaye ni mmoja wa viongozi wa zamani wanaotarajiwa kutoa mapendekezo yatakayokuwa msingi wa kupata mgombea wa urais wa CCM, alisema hayo kwenye kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa kila Jumatatu na Kituo cha Televisheni cha ITV.
CCM imeshaanza mchakato wa mwisho wa kumpata mgombea wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 kwa ajili ya kuwania kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano na pia mrithi wa Jakaya Kikwete kwenye nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho. Mchakato huo utakamilika Jumapili wiki hii wakati Mkutano Mkuu utakapochagua mgombea wa nafasi hiyo ya juu ya kisiasa nchini.
Akizungumza kwenye kipindi hicho, Msekwa alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ushindi wa mgombea urais wa CCM, Rais Kikwete, uliporomoka kutoka asilimia 82 hadi 61 kwa sababu kulikuwa na matukio mengi yaliyowafanya wananchi wajenge chuki dhidi ya chama hicho.
“Lakini uchaguzi wa mwaka huu, kuna jambo moja tu la escrow,” alisema Msekwa.
Msekwa, ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Nane, alisema sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow limejenga chuki na hasira mpya kwa wananchi, hivyo CCM lazima iwe na wagombea wanaokubalika katika jamii.
Msekwa alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa kama matukio ya aina mbalimbali yaliyotokea miaka ya nyuma yanaweza kuwa sababu ya wananchi kuwa na chuki na CCM, kukifanya chama hicho kuwa na wakati mgumu katika chaguzi mbalimbali.
“Hayo ni maamuzi ya wananchi. Mimi siwezi kutabiri chuki hiyo ni kubwa kiasi gani. Wakati ule chuki ilikuwa kubwa sana na tuliiona hata viongozi wa dini walikasirishwa sana. Hiyo ndiyo ilifanya CCM ipate ushindi wa asilimia 61,” alisema.
“Sasa hivi suala lililopo mbele yetu ni escrow tu, hivyo siwezi kupima ukubwa wake ukoje na itatupa ushindi kwa asilimia gani. Ila nina imani kuwa tutashinda lakini sijui ni asilimia ngapi maana inategemea ukubwa wa chuki dhidi ya CCM.”
Katika sakata hilo, zaidi ya Sh306 bilioni zilichotwa kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na fedha hizo zilionekana zikiingia kwenye akaunti za baadhi ya mawaziri, wabunge, majaji na watendaji waandamizi serikalini.
Sakata hilo lilimlazimu Rais Kikwete kumwengua Profesa Anna Tibaijuka katika wadhifa wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi huku Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini sambamba na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, wakilazimika kuachia ngazi.
Wizi wa mabilioni hayo uliwekwa wazi katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo iliibua mjadala mkubwa bungen
0 comments:
Post a Comment