Polisi wakiwatuliza wafuasi wa Chadema waliokuwa wakipinga Mbunge wao John Mnyika asijibu swali lililoulizwa na Mkazi wa Kibamba.Picha ya maktaba.
Jeshi la polisi mkoani Geita limelazamika kuingilia kati kuwanusuru viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya wafuasi wa chama hicho zaidi ya 400 kuvamia viwanja vya ukumbi wa kanisa Katoliki ulipofanyika mkutano wa kura za maoni za nafasi ya ubunge jimbo la Geita, wakidai mgombea aliyekuwa akipendwa na wengi, Rogers Luhega, kuhujumiwa.
Hata hivyo, polisi baada ya kuitwa na kufika eneo la tukio wakiwa na silaha za moto, waliamua kutumia busara kwa kuamua kuwatorosha viongozi pamoja na wagombea wengine kwa kutumia gari dogo.
Akithibitisha kuwapo kwa tukio hilo, Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alisema hali hiyo ilitokana na wafuasi wengi kukutana na matokeo wasiyotarajia baada ya mgombea aliyekuwa akiungwa mkono na wengi kutoongoza kura za uteuzi huo hivyo kukosa uvumilivu.
Akizungumzia matokeo hayo mmoja wa viongozi walioshiriki mchakato huo (jina tunalo), alisema matokeo yaliyotangazwa yalifanyika ndani kwa kuhofia kushambuliwa katika mchakato huo uliokuwa na wagombea sita huku majina matatu yakitarajiwa kufikishwa ngazi ya taifa kwa uteuzi.
Walioshiriki kinyang’anyiro hicho ni Upendo Peneza kura 12, Muta Robert (19), Fabian Mahenge (26), Luhega (35) huku Paschal Kimisha na William Misalaba wote wakifungana kwa kura 44.
MEATU
Uchaguzi wa nafasi ya ubunge kwa kura za maoni wilaya ya Meatu katika majimbo ya Meatu na Kisesa, ulifanyika jana huku jimbo la Kisesa likiwa na wagombea saba, Masanja Manani, alishinda kwa kura 229 na kuwazidi Zidiya Nila (16) na aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, Erasto Tumbo (2).
Jimbo la Meatu walijitokeza wagombea watatu huku Meshack Opulukwa, mbunge anayetetea tena jimbo hilo akipata kura 171 dhidi ya 17 za Johnson Luzubuka na Dionizi Kalekwa (8).
TARIME
John Heche amefanikiwa kushinda kura za maoni katika jimbo la Tarime vijijini kwa kura 310 kati ya 521 zilizopigwa.
Heche aliwashinda Peter Busene (kura 117), Johanes Manko (52), Moses Yomami Misiwa (18), Phabian Mwita (13) na Prosper Nyamhanga kura 2.
TARIME MJINI
Mbunge wa Viti Maalum aliyemaliza muda wake, Esther Matiko, alifanikiwa kupata kura 106 katika jimbo la Tarime Mjini, huku nafasi ya Viti Maalum ikienda kwa Mary Nyagabona.
Matiko aliwazidi mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Tarime, Lucas Ngoto (24), Joseph Martinus (4), Christopher Chomete (2) na Charles Werema aliyepata kura 2.
RORYA
Jimbo la Rorya kura zilimwangukia Stephen Owawa kwa kufanikiwa kuzoa kura 279, Ezekel Kachare (35), Emmanuel Samara (33), Mtatiro Sanya (31), Kevin Robart (30), Herman Odemba (14), Thomas Risa (14) na Evenger Odea (11).
Opiyo Nalo (7), Matiko Saruka (6), Odera Charles (4), Emmanuel Werema (3) na Ochora Ondira (kura 2).
SERENGETI
Katika jimbo la Serengeti, Ryoba Marwa, alifanikiwa kuzoa kura 280 na kuwapita Ramson Rutiginga (160), Manguye Manguye (8), Makoro Rugatiri (4) na John Mrema (1) na nafasi ya Viti Maalum jimbo hilo imeenda kwa Catherine Ruge.
Imeandikwa: Renatus Masuguliko (Geita); Rose Jacob (Meatu) na Samson Chacha (Tarime) CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment