Kwa mujibu wa Ngwilizi aliyesoma hukumu hiyo Bungeni, wabunge wanne wamepata adhabu ya kutohudhuria vikao vyote vilivyosalia katika mkutano huu wa 20, wawili vikao vikao viwili na wengine watapata hukumu yao leo baada ya kusikilizwa na Kamati hiyo.
Amesema waliofungiwa vikao vyote vilivyosalia na kutopata fursa ya kumshuhudia Rais Jakaya Kikwete akivunja Bunge Julai tisa mwaka huu, waligoma kutoa utetezi wao, wakitaka wapate fursa ya kuja na mawakili wao kujitetea.
Brigedia Ngwilizi aliwataja waliofungiwa vikao vyote vya mkutano huu wa 20 ni John Mnyika (Ubungo), Paulin Gekul, (Viti Maalum), Tundu Lissu (Singida Mashariki) Felix Mkosamali (Muhambwe) na Moses Machali (Kasulu Mjini).
Waliofungiwa kuhudhuria vikao viwili ni Peter Msingwa (Iringa Mjini), Mbarouk Mohamed Mbarouk (Ole). Mwenyekiti huyo aliwataja watakapata adhabu baada ya kuhojiwa leo ni pamoja na Joseph Selasini (Rombo), Khalifa Suleman Khalifa (Gando), Rashid Ali Abdallal (Tumbi)
Akichangia hoja ya kuwafungia wabunge hao, Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Maadili, amesema walikubaliana kuwaruhusu watuhumiwa waje na mawakili wao kama walivyoomba, lakini ameshangazwa na hukumu iliyosomwa na Ngwilizi amesema wabunge hao hawakujitetea, hivyo hawakutendewa haki.
Mbunge wa Chake chake, Mussa Haji Kombo alihoji kwanini Kamati hiyo imeamua kutoa adhabu jana wakati bado kuna watuhumiwa wanaopaswa kuhojiwa leo.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, Lissu amesema watu wenye hatia siku zote ni waoga na Bunge hili ni la watu waoga.
Amesema wabunge walioitwa kwenye Kamati hawakujitetea kwani waliomba kuja na mawikili wao na ndio utaratibu na kanuni za Bunge.
“Kwenye Kamati wote tulitaka tuje na mawakili wetu, ndani ya Bunge hatukupata fursa ya kujitetea. Mnakumbuka hivi karibuni Mbunge wetu, Joseph Mbilinyi, alipelekwa kwenye Kamati hii, akaomba kwenda na wakili wake. Leo sisi tumepata adhabu hiyo bila kujitetea.” Amesema Lissu.
Lissu alirejea hoja ya aliyekuwa Mbunge wa Chadema, Zitto Kabwe kwamba mwaka 2007 alihukumiwa na Kamati hiyo, alipata muda wa kujitetea kwenye Kamati na ndani ya Bunge, hivyo alishangazwa na adhabu waliyopata.
Mbunge huyo amesema wamepata adhabu hiyo ili kuwapisha wabunge wa CCM kupitisha miswada ya kuliibia gesi taifa, dhambi ambayo amesema wao hawako tayari kushiriki.
Akizungumzia kilichotokea asubuhi, Lissu amesema wote waliosimama asubuhi wakati Waziri wa Nishati na Madini akilazimisha kusoma miswada hiyo, walitaka kuomba mwongozo, utaratibu na kutoa taarifa, lakini Spika Makinda alikataa na ndio chanzo cha vurugu.
Juzi Spika aliahirisha kikao cha 41 cha Bunge, baada ya wabunge wa kambi rasmi ya upinzani inayoundwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupinga Serikali kuleta miswada mitatu nyeti kwa hati ya dharula kwa madai kuwa wabunge hawajaisoma na wadau hawajapata muda zaidi wa kuijadili.
Miswada hiyo ambayo ni mwiba mchungu Bungeni ni pamoja na muswada wa Sheria ya Petroli, Muswada wa Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika taasisi za uchimbaji Tanzania wa mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment