Pichani Kulia ni Mgombea Urais wa CCM Dkt John Pombe Magufuli akimnadi aliyekuwa Mgombea Ubunge wa jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe (enzi za uhai wake),wakati Dkt Mgufuli alipopita kwenye jimbo hilo wakati wa kampeni
Mgombea Urais wa Jamhuri
ya muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko
na huzuni nyingi taarifa za vifo vya Mbunge wa Jimbo la Ludewa, mkoani
Njombe Ndugu Deo Filikunjombe Haule, Kepteni William Silaa pamoja na
abiria wengine wawili ambao wameaga dunia jana, Alhamisi, Oktoba 15,
2015 kwa ajali ya helkopta iliyotokea katika eneo la Hifadhi ya Selous
mkoani Morogoro.
Katika salamu za
rambirambi ambazo amewatumia Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe Ndugu Deo
Sanga, na Meya wa Manispaa ya Ilala Mstahiki Jerry Silaa, Dkt. Magufuli
amesema: “Kwa hakika, nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za
vifo vya Ndugu Filikunjombe na Ndugu Silaa ambavyo nimetaarifiwa kuwa
vimetokea kwa ajali ya helkopta aliyokuwa akiitumia Ndugu Filikunjombe
kwa Kampeni zake za Ubunge katika jimbo hilo la Ludewa.
Katika salamu zake hizo
za rambirambi Dkt. Magufuli ameongeza kuwa: “Kama unavyojua, namfahamu
vizuri Ndugu Filikunjombe. Alikuwa Mbunge mwenzangu katika Bunge
lililomaliza muda wake mwaka huu. Nimefanya kazi naye kwa karibu na kwa
miaka mitano ndani ya bunge letu.
Alikuwa mtumishi hodari, mtumishi
mwaminifu na mwadilifu kwa wananchi wa Tanzania, na hasa wananchi wa
Jimbo la Ludewa, ambao aliwawakilisha kwa miaka mitano iliyopita akiwa
Mbunge wao. Hata nilipofanya ziara ya kampeni katika jimbo lake la
Ludewa mwezi uliopita nililala nyumbani kwake, hiyo inaonesha
nilivyokuwa karibu naye. Tutakosa utumishi wake mahiri sana.”
Salamu zake za
rambirambi kwa Mstahiki Meya Jerry Silaa, Dkt. Magufuli amesema:
“Nimesikitishwa sana na taarifa ya kifo cha Baba yako Kepteni William
Silaa, kwani ni tukio lisilozoeleka. Ni jana tu nimeshiriki nawe katika
kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 katika jimbo unalogombea
Ubunge, jimbo la Ukonga, naungana nawe katika kipindi hiki kigumu cha
msiba mkubwa. Nakupa pole wewe binafsi, familia yenu, ndugu, jamaa na
marafiki wote”.
Aidha aliongeza
“Nakutumia wewe Ndugu Sanga, Mwenyekiti wetu wa CCM mkoa wa Njombe
salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Ndugu
Filikunjombe na abiria hao wengine. Aidha, kupitia kwako namtumia
rambirambi nyingi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Anna Semamba Makinda na Wabunge wote kwa kuondokewa na
mwenzao.”
Dkt. Magufuli ameongeza
“Nakuomba pia unifikishe salamu zangu za rambirambi kwa wananchi wa
Jimbo na Wilaya ya Ludewa ambao wamepoteza Mbunge wao aliyewatumikia kwa
ustadi mkubwa kwa kipindi chote. Aliwawakilisha vizuri na kujali sana
maslahi yao. “Ametuma pia salamu za
rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Ndugu Filikunjombe
kwa kuondokewa na mhimili wa familia na rafiki yao mpenzi.
Amewaombea kwa Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu ya
uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi. Pia naungana nao
kumwomba Mwenyezi Mungu aziweke pema peponi roho ya Deo Filikunjombe
Haule”. Amen.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
CCM Ofisi Ndogo, Lumumba
DAR ES SALAAM.
16 Oktoba, 2015
Kitengo cha Mawasiliano
CCM Ofisi Ndogo, Lumumba
DAR ES SALAAM.
16 Oktoba, 2015
0 comments:
Post a Comment