WAKATI
wapinzani wakipinga uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, waziri huyo amewasihi wananchi kumvumilia kidogo, ili
baada ya muda mfupi atoe mpango wa maendeleo ya wizara hiyo, ambao
pamoja na mambo mengine, utaelezea bei ya nishati hiyo itakavyoshuka.
Akizungumza
na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuapishwa kushika wadhifa
huo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Profesa Muhongo alisema mbali na
mkakati wa kushusha bei ya umeme, kasi ya kusambaza umeme vijijini
kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), itarejea palepale.
“Nimepokea
uteuzi huo, kinachofuata ni kuwatumikia wananchi, niwaombe tu
wanivumilie kidogo nitawapa mpango wangu wa maendeleo wa muda mfupi na
mrefu, lakini nisisitize tu nishati sio siasa, ni suala la utaalamu,
liachwe lifanywe kitaalamu,” alisema Profesa Muhongo.
Akizungumzia
bei ya umeme na upatikanaji wake, Profesa Muhongo alisema kupunguza bei
hiyo ni ajenda muhimu itakayozingatiwa na kusema ili umeme uwe wa
uhakika, ni lazima kuwe na mipango ya kuwa na nishati hiyo ya uhakika
ifikapo mwaka 2025.
“Umeme
wa uhakika utapatikana na matarajio yetu ni Tanzania kuwa nchi ya
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ambapo tunatarajia uzalishaji wa
nishati hiyo ufike Megawati 10,000 hadi 15,000,” alisema Profesa Muhongo.
Alisisitiza
kwamba wizara yake haitategemea chanzo kimoja cha nishati bali
wataangalia vyanzo vingine ikiwemo nishati jadidifu, upepo, gesi, makaa
ya mawe, maji huku akisema vyanzo hivyo vikitumika kuzalisha nishati, ni
wazi bei ya umeme itashuka na kushusha gharama nyingine za maisha na za
uwekezaji.
Aliongeza
katika kuendeleza sekta ya nishati suala la uwekezaji ni muhimu hivyo
wizara yake inakaribisha wawekezaji wenye sifa, watakaowekeza kwenye
sekta hiyo ili kuja na matokeo bora zaidi, wananchi wanufaike na
rasilimali za nchi yao.
Pamoja
na nia yake hiyo kwa wananchi, Profesa Muhongo anakabiliwa na pingamizi
kutoka kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani, akiwemo Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba.
Lissu
na Profesa Lipumba, wamekaririwa wakikosoa uteuzi wa Profesa Muhongo
kwa madai kuwa wizara aliyopewa kuiongoza, ilikumbwa na kashfa ya
Akaunti ya Tegeta Escrow wakati wa uongozi wake, ikasababisha ajiuzulu.
Hata
hivyo, Profesa Lipumba na Lissu katika kukosoa huko, hawakutaka kutumia
kumbukumbu zilizo wazi kuwa uchunguzi dhidi ya Profesa Muhongo,
ulibaini kuwa hakukiuka maadili yoyote katika sakata la utoaji wa karibu
Sh bilioni 300 zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa
Benki Kuu (BoT).
Matokeo
ya uchunguzi huo yalitangazwa Mei mwaka huu na Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue, ambapo alisema Tume ya Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, ndiyo ilifanya uchunguzi kama Profesa Muhongo
alistahili kwenda kwenye Baraza la Maadili kujibu mashitaka, lakini
hawakuona tatizo lake na kufunga shauri lake.
Balozi
Sefue aliweka wazi kuwa Profesa Muhongo alijiuzulu kwa sababu za
kisiasa, lakini kimaadili hakuhusika kwa namna yoyote, kutokana na
uchunguzi wa Sekretarieti ndiyo sababu hakufikishwa katika Baraza la
Maadili.
Kitu
kingine ambacho Lissu na Profesa Lipumba, hawakutaka kuzungumzia ni
utendaji wa Profesa Muhongo alipokuwa katika wizara wakati wa uongozi wa
Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Kumbukumbu
zinaonesha kuwa katika miaka miwili ya uongozi wake katika Wizara ya
Nishati na Madini, Profesa Muhongo alisimamia kwa umahiri usambazaji wa
umeme vijijini.
Kabla
ya kuteuliwa kwa Profesa Muhongo, Watanzania asilimia 14 tu ndio
waliokuwa wakitumia nishati ya umeme, kati yao asilimia 12 walikuwa
watumiaji wa mijini na asilimia mbili ndio walikuwa watumiaji wa
vijijini.
Kwa
mujibu wa takwimu za Serikali, kati ya mwaka 2007 na mwaka 2010,
kulikuwa na ongezeko la asilimia nne la watumiaji wa umeme, hali
iliyoonesha kuwa ongezeko la Watanzania waliokuwa wakipata umeme,
lilikuwa asilimia moja kwa mwaka.
Lakini
baada ya kuteuliwa kwa Profesa Muhongo katika nafasi hiyo, katika muda
mfupi wa uongozi wake, idadi ya Watanzania wanaotumia umeme iliongezeka
na kufikia asilimia 36 katikati ya mwaka jana.
Kwa
hatua hiyo, uongozi wa Profesa Muhongo ulivuka malengo ya Ilani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo ndio msingi wa utekelezaji wa malengo
ya Serikali, iliyotaka Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2015, asilimia
30 ya Watanzania wawe wanapata umeme.
Katika
kutimiza malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010, uongozi wa
Profesa Muhongo, ulitangaza punguzo la gharama za kuunganisha umeme
majumbani kutoka Sh 177,000 za awali hadi Sh 27,000 vijijini.
Awali,
punguzo hilo lilitolewa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, ambako bomba la
kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam limeanzia na limepita, lakini
baada ya muda gharama hizo zilishushwa kwa vijiji vyote nchi nzima.
Profesa
Muhongo mwenyewe alikaririwa akisema gharama hizo zitahusu miradi
inayosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), katika kipindi ambacho
makandarasi watakuwa wakiendelea na awamu ya pili ya miradi iliyoanza
Machi mwaka huu na kutarajiwa kukamilika katikati ya mwakani.
0 comments:
Post a Comment