Mamilioni
ya Wamarekani jana waliadhimisha Siku Ya Shukrani (Thanksgiving). Hii
ni moja kati ya Siku Kuu rasmi nchini humu inayoadhimishwa kila Akhamis
ya nne ya mwezi wa Novemba.
Asili yake:
Rais wa Marekani Barack Obama akimuachia huru Bata. Photo na CARLOS BARRIA/REUTERS
Vyanzo
vya kihistoria vinatofautiana kuhusu asili ya Siku Kuu hii. Lakini
maelezo yanayosadikiwa na wengi ni kuwa chimbuko lake linarejea mwaka
1621.
Walowezi
kutoka Ulaya walipokuwa wakiwasili katika Mabara ya Amerika walipata
matatizo ya kuanzisha maisha mapya. Mnamo mwaka 1620 meli iliyopewa
jina la Mayflower ilitia nanga nchini Marekani ikiwa na abiria 102
kutoka Uingereza. Miongoni mwao walikuwemo Wakristo waliokuwa wakitafuta
sehemu watakayokuwa huru kufanya ibada zao, na pia walikuwemo
waliohajiri kwa ajili ya tamaa ya kumiliki ardhi.
Walipowasili
Marekani walikumbana na matatizo mbalimbali yakiwemo ukosefu wa uzoefu
wa mazingira mapya, na nusu yao walifariki dunia kutokana maradhi na
mengineyo.
Baada
ya kutimiza mwaka mmoja, mnao mwezi November 1621, Walowezi waliobakia
hai kwa msaada wa wenyeji ambao waliwapa jina la "Wahindi Wekundu",
walifanikiwa kupata vuno la mwanzo la mahindi.
Kwa
hivyo waliwaalika wenyeji wao na kufanya karamu maalum kwa ajili ya
kumshukuru Mungu kwa kuwapa neema zake, na kuwashukuru wenyeji wao kwa
kuwasaidia mbinu za maisha katika ulimwengu uliokuwa mpya kwao.
Inaarifiwa kuwa yakula vingi katika karamu hiyo iliyodumu kwa muda wa
siku tatu vilitokana na mapisi ya wenyeji wa asili hapa Marekani.
Kutoka
hapo siku hiyo ikawa inaadhimishwa katika makoloni mengine katika Bara
la Amerika, kila koloni likiiadhimisha kwa aina yake tofauti. Mnamo
mwaka 1863, Rais Abraham Lincolin akaitangaza kuwa Siku Kuu rasmi
kitaifa.
Katika enzi za leo:
Siku
Kuu Ya Shukrani au Siku Ya Kutoa Shukrani, imekuwa ni miongoni mwa Siku
Kuu kubwa kabisa za kitaifa nchini Marekani ambayo huwakutanisha pamoja
watu wa aila. Kwa vile inakuja siku ya Alkhamis, sehemu nyingi za kazi
hutoa mapumziko siku ya Ijumaa pia, na hivyo kuwawezesha watu kusafiri
kutoka sehemu mbalimbali kwenda kujumuika na aila zao, wakiongezea pia
Jumamosi na Jumapili ambazo kwa kawaida huwa ni siku za mapumziko katika
wiki.
Kwa
hali hiyo, biashara katika sekta za usafiri na nishati nazo pia
huchangamka kutokana na wingi wa watu wanaosafiri kutoka sehemu moja au
nyengine. Sekta ya biashara inayokumbwa na mkosi siku hii ni mikahawa,
kwa vile watu hula majumbani.
Kwa
jina la utani siku hii huitwa "Turkey Day", kwa vile mlo mkuu katika
karamu huwa ni bata mzinga, yakiwepo pia machopochopo mengine. Ikiwa
siku hii ni faraja kwa wafanyakazi wanaopata mapumziko ya siku nne
mfululizo na neema kwa wafugaji wa bata mzinga kwa vile biashara yao
hungezeka, kwa viumbe bata hao hii inakuwa ni siku ya nakama kutokana na
kuchinjwa kwa wingi.
Sehemu
nyingi za kazi hutoa mabata wa bure kwa wafanyakazi wao au kadi za
malipo ili kwenda kunua sehemu wanazotaka. Kwa kawaida karamu hii
hufanyika wakati wa jioni, ingawaje baadhi ya watu huifanya majira ya
mchana.
Wakati
mabata wengi huonja uchungu wa visu kwa ajili ya Siku Ya Shukrani,
angalau bata mmoja husalimika. Hii ni kutokana na ada ya kila mwaka ya
Ikulu ya Marekani kumwachia huru bata kama sehemu ya maadhimisho ya siku
hiyo. Siku ya Jumatano, Rais Barack Obama aliwaachia huru mabata
wawili. Sherehe hizi hufanyika rasmi wakiwepo pia waandishi wa habari.
Miongoni
mwa ada za Siku Kuu Ya Shukrani, ni mchezo wa kabumbu la Kimarekani
(American Football). Jioni, wakati watu wakiwa wanawararua mabata
majumbani, halkadhalika hupata nafsi ya kuburudika kwa kuangalia pambano
la mchezo huo unaopendwa zaidi nchini humu, ambalo aghalabu huwa la
kukata na shoka. Timu zinazopata nafasi ya kucheza siku hiyo hujisikia
heshima kubwa.
Changamoto zake:
Ingawaje
Siku Ya Shukrani ni katika Siku Kuu kubwa nchini Marekani, hata hivyo
pia inakabiliwa na changamoto zake. Kuna zile za watu wanaopigania haki
za wanyama na kuwahurumia mabata wanaochinjwa kwa wingi katika siku hii.
Aidha kuna changamoto za kihistoria.
Baadhi
ya watu wanaipinga Siku Kuu hii kwa vile kusherehekea kwake ni sawa na
kuhalalisha Ulowezi na Ukoloni na Ubeberu wa Wazungu katika Mabara ya
Amerika. Itakumbukwa kwamba, leo hii tunapoitaja Marekani akilini mwetu
zinatujia sura za Wazungu, na wenyeji wa asili takriban hawajulikani
kabisa.
0 comments:
Post a Comment