Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amewaasa raia wanaokimbia nchi zao na kupata
hifadhi Tanzania kutobeba silaha wanapoingia nchini kuja kuishi kwenye
kambi za wakimbizi.
Ametoa
onyo hilo jana wakati akizungumza na mamia ya wakimbizi wanaoishi
kwenye kambi za Nyarugusu na Nduta zilizoko wilayani Kasulu na Kibondo,
mkoani Kigoma waliofika kumsikiliza kwenye mikutano ya hadhara
iliyofanyika kwenye kambi hizo.
“Ninawasihi
mjitambue kuwa mmehama kutoka DRC na Burundi, na mnapoingia hapa
inabidi mbadilike muwe na tabia za hapa. Hatuhitaji mje na silaha au
vifaa hatarishi kwa sababu tunataka mkae kwa usalama,” alisema.
Alisema
suala la usalama ni muhimu miongoni mwao, ni muhimu zaidi kwa majirani
zao lakini pia ni muhimu sana kwa watoa huduma wanaowahangaikia.
“Tunataka kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake ili siku mkiondoka mrudi nyumbani mkiwa salama,” alisema.
“Ninyi
mko hapa mnatunzwa kwa hiyo hamruhusiwi kutoka kambini na kutembea
hovyo huko nje. Hii ni kwa usalama wenu. Hatumruhusu kuingia na bunduki
au mabomu na yeyote atakayemuona mwenzie ana silaha au ameificha mahali
aje atuambie ili tumchukulie hatua na ninyi wengine mbakie salama,” alisisitiza.
Kuhusu
maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), Waziri Mkuu aliwataka wakimbizi
hao wajiepushe na ngono zembe kwa sababu kiwango cha maambukizi
kimeongezeka kwa asilimia moja ikilinganishwa na mwaka jana
“Nimetembelea
hospitali yenu hapa kambini na kuelezwa kuwa maambukizi ya VVU hapa
yapo na mwaka huu yamefikia asilimia mbili ya watu waliopimwa
ikilinganishwa na mwaka ambapo ilikuwa ni asilimia moja tu,”
“Kutokana
na uwingi wenu, naomba niwasihi sana mjizuie kufanya ngono zembe na
kama mtu atashindwa kabisa kujizuia ni vema atumie kinga. La sivyo
mtaleta maambukizi ya juu sana na wote mtakwisha,” alisema.
“Suala
lenyewe siyo jambo la dharura, kawaida huwa kuna maandalizi baina ya
wahusika, watu wanakubaliana juu ya muda na mahali pa kukutana ndiyo
maana nasema siyo jambo la dharura. Ndugu zangu tujihadhari sana kwa
sababu kasi ya maambukizi mahali hapa iko juu sana,” alisisitiza.
Mapema,
Mkuu wa kambi ya Nyarugusu, Bw. Sospeter Boyo alimweleza Waziri Mkuu
kwamba kambi hiyo ilifunguliwa Novemba 1996 kwa lengo la kuwahifadhi
wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo waliokuwa wakikimbia
vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Alisema
kambi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 28, ina uwezo wa kuhifadhi
wakimbizi 50,000 lakini kwa sasa inao wakimbizi 151,032 ambao ni mara
tatu zaidi ya uwezo halisi wa kambi hiyo.
“Tangu
Aprili mwaka huu, idadi ya wakimbizi imeongezeka hadi kufikia 151,032
miongoni mwao ni wakongo 61,313, warundi 89,619, Wanyarwanda 75, Waganda
12, Wasudan kusini wane,Wakenya wane, Msomali mmoja, Mzimbabwe mmoja na
raia wa Ivory Coast mmoja,” alisema Bw. Boyo.
Alisema wanakabiliwa na changamoto za uhaba wa maji safi, ufinyu wa huduma za afya na elimu na uharibifu wa mazingira.
Waziri
Mkuu bado anatembelea pia kambi ya JKT ya Mtabila wilayani Kasulu na
kesho asubuhi ( leo) anatarajiwa kufanya majumuisho ya ziara yake.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, DESEMBA 29, 2015
0 comments:
Post a Comment