Waziri mkuu Mh Kassim Majaliwa amemtaka mtendaji mkuu wa wakala wa
vipimo Tanzania kumpa maelezo kwa maandishi ya sababu za kuzuia
utumiwaji wa mita za kupima kiwango cha mafuta kinachopakuliwa bandarini
kutoka melini (flow meter) kwa kipindi cha miaka mitano jambo
lililosababisha serikali kupata hasara ya mamilioni ya shilingi huku
mita hizo zikianza kufanya kazi siku moja tu kabla ya kufanya ziara hiyo
bandarini hapo.
Waziri mkuu Mh. Kassim Majaliwa ameifanya ziara hiyo ya kushtukiza
katika bandari ya Dar es Salaam ili kujionea namna shughuli za upakuaji
wa mafuta kutoka melini zinavyofanyika bila ya uwepo wa mwanya wa
ukwepaji wa kodi kwa kutembelea maeneo yenye mita za kupimia mafuta hayo
yaani flow meters na kubaini kuwa mita hizo licha ya kununuliwa kwa
fedha nyingi hazijafanya kazi kwa kipindi cha miaka mitano baada ya
uwepo wa zuio kutoka kwa wakala wa vipimo Tanzania na kuanza kufanya
kazi siku moja kabla ya ziara hiyo ya waziri mkuu na kutaka maelezo.
Mtendaji mkuu wa wakala wa vipimo nchini Magdalena Chuwa nae
akapata fursa ya kutoa maelezo ya sababu za kuzuia kutumika kwa mita
hizo jambo lililoisababishia serikali hasara.
Mara baada ya maelezo hayo waziri mkuu Kassim Majaliwa anatoa
maagizo kadhaa mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali bandarini hapo
ambapo kwanza anamwagiza mtendaji mkuu wa wakala wa vipimo nchini
kumwandikia barua yenye maelezo ya sababu za kuzuia utumiwaji wa mita
hizo.
Pia waziri mkuu anatoa muda wa mwezi mmoja kung`olewa kwa mabomba
yote ya mafuta yaliyounganishwa bila idhini ya mamlaka ya bandari nchini
jambo linalotoa mwanya wa uwepo wa wizi wa mafuta kutokana na
kukosekana kwa ufuatiliaji.
Aidha waziri mkuu anamuagiza msajili wa hazina kwa kushirikiana na
mwanasheria mkuu kuangalia namna ya kuvunja mkataba na kampuni ya Oryx
Energys inayomiliki matanki ya kuhifadhia mafuta kwa asilimia 50 kwa 50
na serikali.
Waziri mkuu huyo anataka uwepo wa mfumo maalum utakaodhibiti mianya
ya upitishwaji wa mafuta katika bandari ya Dar es Salaam bila ya
ukwepaji wa kodi ili kuliwezesha taifa kukusanya mapato ya kutosha
kutoka bandarini kabla ya serikali kuanza kujielekeza katika kuimarisha
sekta ya reli nchini
0 comments:
Post a Comment