Nani asiyemkumbuka Michael Jordan? Wapo wanaomfahamu pasipo kumwona na hawajui anafananaje lakini jina lake wanalifahamu. Nani asiyemkumbuka Scottie Pippen na ni nani asiyekuwa na kumbukumbu ya Dennis Rodman, mwanaume mwenye visa ndani na nje ya uwanja. Usisahau kumtaja kocha wa sasa hivi wa Golden State Warriors Stev Kerr.
Hawa wote walitengeneza kikosi bora kabisa cha msimu wa mwaka 1995-96 ambacho kilienda kuweka rekodi ya kushinda michezo 72 huku wakipoteza 10 peke yake. Ijapokuwa historia huwekwa ili zivunjwe lakini hakuwapo aliyetabiri ama kuwaza kabla ya kuanza kwa msimu huu kuwa Warriors wangeweza kuifikia na kuvunja rekodi ya wababe hawa.
Lakini wazungu wanasema Never Say Never… Warriors walianza msimu kwa kasi, Curry akifanya makubwa na kuanza kunyanyua kope na masikio ya watu kuhusiana na namna ambavyo wanaweza kumaliza msimu huu.
Mpaka kubakia kwa michezo minne ya mwisho, Warriors walikuwa wameshapoteza michezo 9, hali iliyofanya watu kuamini wasingeweza kuifikia rekodi ama kuivunja na sababu kubw ilikuwa michezo miwili dhidi ya klabu ya pili kwa ubora ama ambayo wengi wanaamini ndiyo iliyotimia zaidi ya San Antonio Spurs. Walitakiwa kushinda 3 ili kufikia rekodi na kushinda yote ili kuvunja.
Lakini Warriors walishinda michezo yote 3 kabla ya huu wa leo na kuifikia rekodi ya Chicago Bulls ya 95-96 huku pia wakiondoa uteja uliodumu katika uwanja wa San Antonio Spurs wa AT&T Center kwa miaka 19 iliyoshuhudia wakipoteza michezo 33 ya ligi.
Warriors walimaliza mchezo wao wa mwisho alfajiri ya leo dhidi ya Memphis Grizzlies, siku ambayo ilipewa jina la mamba day kutokana na Kobe Bryant kuwa anacheza mchezo wake wa mwisho wa ligi hiyo na klabu ya Los Angeles Lakers.
Warriors walimaliza mchezo kwa ushindi wa pointi 125-104 na kuweka rekodi mpya huku wakivunja rekodi ya Bulls iliyodumu kwa miaka 20 na ambayo hakuna aliyetegemea ingeweza kuvunjwa na wengi wakiangazia kile kikosi kama kilichokuwa kimetimia barabara.
Stephen Curry alimaliza mchezo huo akiwa na pointi 46 huku akicheza kwa dakika 30 pekee. Curry alikuwa akishikilia rekodi ya kufunga pointi 3 nyingi zaidi katika historia ya NBA akiwa amefunga pointi 3 286 msimu uliopita. Hivyo aliingia katika mchezo huu akiwa na pointi 3 392 na hivyo kutakiwa kufunga pointi 3 nane ili kufikia jumla ya pointi 3 400 katika msimu mmoja bila kuhesabu playoff.
Curry alipata mitupo 10 ya pointi tatu hivyo kumfanya afikishe pointi 3 402 katika msimu mmoja bila playoff. Hii inamfanya Stephen Curry, mtoto wa mchezaji wa zamani Dell Curry, mume wa Ayesha Curry na baba wa mabinti wawili Riley na Ryan Curry kuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya NBA kufikia mitupo 300 ya pointi 3 na pia kuivuka kwa zaidi ya mitupo 100 na kufikia mitupo 400 katika msimu mmoja.
Steve Kerr, kocha wa sasa wa Warriors ambaye pia alikuwa mchezaji katika kikosi cha Bulls kilichoweka rekodi hakusita kukubali anachokiona na kusema ” nimekuwa nikiwaambia watu wangu wa karibu kuwa sikuwahi kufikiri kama rekodi hii iliyowekwa miaka 20 iliyopita ingeweza kuvunjwa sikuwa sahihi na sasa nimeamini”.
Akaendelea “Lakini siamini kama hii tuliyoweka inaweza kuvunjwa tena, yaani timu ishinde 74-8, hapana na hata mashabiki wa Warriors najua wanaamini kama mimi na hawawazi kama mwakani tutafika hapo”.
Michael Jordan hakusita kuwasifia Golden State Warriors na kukiri kuwa rekodi zipo ili zivunjwe na anawapongeza sana katika hilo kwani mchezo wa mpira wa kikapu una rekodi na mambo mengi ambayo inabidi yatokee. Akamalizia kwa kutamani kuwaona nini watakifanya katika hatua ya mtoano yaani Playoffs.
Mara baada ya mchezo kumalizika, Rais wa Marekani Barrack Obama alitweet na kuandika “nawapongeza sana Warriors kwa kuvunja rekodi. Ni watu safi ndani na nje ya uwanja, na kama kuna timu niliamini itavunja rekodi ya Bulls (hii ndiyo timu anayoshabikia Obama) basi ni wao.
Kamishna wa NBA, Adam Silver pia aliwapongeza Warriors kwa rekodi na mafanikio waliyojiandikia.
HIGHLIGHTS
0 comments:
Post a Comment