https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    Mkuu wa Wilaya Amzuia Waziri Nchemba Kwenda Kijijini Kusikiliza Kero za Wananchi


    Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, juzi alimzuia Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwigulu Nchemba kwenda kijiji cha Mikomario wilayani Bunda kutatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na mwekezaji kwa madai ya wasiwasi wa usalama kuwa mdogo. 

    Baada ya jitihada zake za kumzuia kugonga mwamba, Nyamubi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Bunda aliamua kujitenga na ziara hiyo kwani licha ya kufika eneo la mkutano, hakujihusisha na lolote kwa kuamua kukaa pembeni. 

    “Mheshimiwa waziri nakushauri usiende Kijiji cha Mikomario kwa muda huu ambao unakaribia usiku kwa sababu usalama utakuwa ni mdogo kutokana na ukorofi wa wananchi wa eneo lile,” alishauri Nyamubi wakati akizungumza na Nchemba ofisini kwake.

    Hata hivyo, waziri Nchemba alisisitiza kuwa lazima aende kuzungumza na wananchi hata kama atalazimika kuhutubia kwa kutumia taa za gari kwa sababu aliwaahidi kuwa angefika na kuzungumza nao na walikuwa wakimsubiri tangu mchana.

     “Mheshimiwa kaimu mkuu wa mkoa, bado sijashawishika kutotimiza ahadi ya kwenda kuzungumza na wananchi wale, wamenisubiri tangu asubuhi na nimepata taarifa wako uwanjani hadi jioni hii wakinusubiri. Kutokwenda ni kutowatendea haki,” alisisitiza Nchemba.

    Baada ya msimamo huo, ndipo Nyamubi alipotangaza kujitoa kwa lolote ambalo lingetokea, licha ya kuwamo kwenye msafara wa viongozi uliofika kijijini hapo saa 12.40 jioni, hakukaa meza kuu wala kujishughulisha na lolote hadi mkutano ulipomalizika kwa amani saa 1.10 usiku.

    Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho ambacho kimekuwa na mgogoro wa ardhi kwa miaka 30 sasa bila ufumbuzi, Waziri Nchemba aliahidi kuutafutia ufumbuzi, lakini akawasihi kuwa na subira kwa sababu lazima awasiliane na wizara nyingine zinazoguswa nao.

    “Suala hili ni la kisheria, hivyo linatakiwa kutatuliwa kisheria badala ya mapigano, nipeni fursa ili wizara yangu iwasiliane na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Tamisemi ili kwa pamoja tuutafutia ufumbuzi.

    “Wenye mamlaka ya kupanga na hata kubadili matumizi ya ardhi ya kijiji ni ninyi wananchi kupitia mikutano na Serikali yenu ya kijiji, viongozi na wataalamu kazi yetu ni kutoa ushauri kuhakikisha uamuzi wenu unakuwa halali,” alisema. 

    Wakiwa na mabango yenye ujumbe, wakazi hao walimpongeza waziri kwa kutimiza ahadi ya kuzungumza nao ili kutafutia ufumbuzi mgogoro huo unaohusu hekta 2, 500 zinazodaiwa kutolewa kwa mwekezaji bila ridhaa ya Serikali ya Kijiji. 
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Mkuu wa Wilaya Amzuia Waziri Nchemba Kwenda Kijijini Kusikiliza Kero za Wananchi Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top