https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    Nyaraka Feki za Serikali Zazagaa Kila Kona.....Mpigachapa, Polisi Watoa Onyo kwa Wanaozimiliki


    MPIGACHAPA Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo amekiri kuwepo kwa nyaraka bandia za serikali katika sekta mbalimbali, nyingi zikiwa za ukusanyaji wa mapato ya serikali, vyeti vya kitaaluma, ndoa na nyinginezo.

    Kutokana na hali hiyo, amewaasa wananchi wanaofanya shughuli hizo za kutengeneza nyaraka hizo bandia ambazo ni hatari kwa usalama wa nchi, kuacha kwani wanaendesha oparesheni ya kudumu itakayowabaini na kuchukuliwa hatua kali, ikiwemo kifungo cha miaka 20 jela.

    Hivyo amewataka watendaji na wasimamizi katika idara mbalimbali kufanya uhakiki upya wa nyaraka za serikali, kwani zimezagaa sehemu mbalimbali nchini hususan katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), vyuoni na katika maeneo ya kazi.

    Akizungumza Dar es Salaam jana, Mpigachapa Mkuu Chibogoyo alisema nyaraka hizo bandia ni pamoja na stakabadhi za malipo, vibali mbalimbali, hati za makontena, leseni za magari pamoja na bima.

    Alisema katika oparesheni iliyofanyika mwaka jana ya ‘Okoa Pato la Taifa‘ katika kutafuta nyaraka bandia za serikali, walibaini kuwepo kwa nyaraka za vyeti vya ukaazi au kuzaliwa vinavyomilikiwa na raia wa kigeni, stakabadhi za mapato, leseni za biashara, vyeti bandia vya kitaaluma na vinginevyo.

    Alisema nyaraka hizo walizikuta katika vituo vyao vya mauzo na wengine kwenye nyumba zao za kutengenezea uhalifu huo na kubaini kuwa uhalifu huo ni zaidi ya ujambazi kutokana na madhara yake kwa nchi.

    Alisema katika oparesheni hiyo walibaini kiwanda cha kutengeneza bidhaa hizo maeneo ya Buguruni katika Manispaa ya llala, Dar es Salaam pamoja na vyeti feki vya Chuo Kikuu cha Kampala (KIU), vitambulisho vya ukaazi ambako kuna raia wa kigeni amepewa cha ukazi akiishi Kariakoo, risiti za usalama barabarani pamoja na shahada za ndoa za Kanisa Katoliki la Mtakatifu Maria Magomeni jijini Dar es Salaam.

    Alisema pia walikamata boksi tatu za stika za bima zinazowekwa kwenye magari zikiwa tayari kusafirishwa kwenda mkoani Tanga zikiwa zimewekwa kwenye jokofu bovu lililochakaa karibu na mama ntilie katika maeneo ya Salamander.

    “Wananchi wasio waaminifu wanaotaka kupoteza maisha ya wananchi wema na usalama wa nchi ikiwemo kurudisha nyuma maendeleo na uchumi wa nchi, nawapa salamu zangu kuwa mimi na timu yangu tumejipanga kutokomeza vitendo hivyo na tutapigania nchi,” alisema Chibogoyo.

    Alieleza kuwa makatazo ya udhibiti wa nyaraka yapo katika Sheria ya Makosa ya Jinai, Sheria ya Ngao ya Taifa, Sheria ya Ushahidi na Sheria ya Usalama wa Taifa, hivyo ukikamatwa na katatasi inayokusudia kutumika kwa udanganyifu, adhabu ni kufungwa miaka saba.

    Aidha, alifafanua kuwa Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 inakataza kuwa na nyaraka, mihuri, karatasi maalumu na kumiliki taarifa za serikali isivyo halali na sheria inasema kuwa ni mhalifu na adhabu yake ni miaka 20 jela.

    Chibogoyo aliwataka wananchi wema kutoa taarifa pale wanapowabaini watu hao wanaotengeneza nyaraka bandia za serikali pale wanapohitaji nyaraka hizo kwa haraka na ofisi yake itampatia nyaraka halali kwa haraka.

    Akizungumzia nyaraka hizo bandia za serikali, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alisema hali ya nyaraka hizo inatisha kwani ni kubwa kwani nyaraka hizo zote muhimu zipo na zinatumika katika maeneo mbalimbali. 

    Kamanda Sirro alisema kuna watu wamenufaika kwa nyaraka hizo kama vyeti kutumika kupata ajira hivyo watafuatilia na watawachukulia hata za kisheria wanufaika wote wa nyaraka hizo bandia.

    Alisema katika oparesheni waliyoshirikiana na Mpigachapa Mkuu wa Serikali walikamata watu watatu ambao inaonekaan ndiyo mabosi au wakurugenzi wa kutengeneza nyaraka hizo huku wakiwa na mawakala wao katika mikoa mbalimbali kama Mwanza na kwingineko. 

    Alisema wataendelea kufanya oparesheni ili kuhakikisha suala hilo linakoma kwa kuwakamata wahusika wote.
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Nyaraka Feki za Serikali Zazagaa Kila Kona.....Mpigachapa, Polisi Watoa Onyo kwa Wanaozimiliki Rating: 5 Reviewed By: news
    Scroll to Top