Wakati
Jeshi la Polisi likisisitiza kupiga marufuku mikutano na maandamano ya
Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Kupinga Udikteta nchini (Ukuta),
chama hicho kimepinga katazo hilo nakudai kuwa liko kinyume na Katiba ya nchi.
Kauli
hiyo imetolewa leo na Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema katika
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Makao Makuu ya chama
hicho Mtaa wa Ufipa, jijini Dar es Salaam.
Kwenye
mkutano huo akiwa na Lawrance Masha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani
(2005-2010) Lissu amesema, rais anayo nafasi ya kuzuia mikutano ya
hadhara kwa sharti la kupeleka hoja bungeni na kisha kujadiliwa na si
vinginevyo.
“Ipo
sheria ya kutangaza hali ya dharura, iliyotungwa mwaka 1995, hii
inamruhusu rais kupeleka hoja bungeni ya kutaka kutangaza hali ya
dharura kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu na kama Bunge likiridhia,
basi rais anatangaza, namshauri Magufuli afanye hivyo.
“Aitangazie
Tanzania na dunia kwa ujumla kuwa, nchi hii ipo katika hali ya hatari
na katika hali ya dharura, na kwamba mikutano yote itakuwa marufuku.
“Na
miezi mitatu ikiisha aende tena bungeni kuomba aongeze mingine.
Akifanya hivyo atakuwa hajavunja sheria na hata sisi tutamtii,” amesema Lissu.
Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki amelitaka Jeshi la Polisi
kuacha kutoa matamko yanayoiingiza nchi katika utawala wa kidikteta.
Kauli
hiyo inakuja ikiwa ni siku moja tu, tangu jeshi hilo kupitia Nsato
Marijani, Kamishina wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, litangaze kupiga
marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa nchini, ikiwemo vikao vya
ndani vya vyama.
Katika
mkutano na wanahabari, makao makuu ya chama hicho, akiwa ameambatana na
Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa chama hicho, Profesa Mwesiga
Baregu, Mjumbe wa Kamati Kuu, pamoja na Masha amesema, Lissu amesema,
kamwe Chadema hakiwezi kuruhusu ukiukwaji wa katiba na sheria za nchi.
“Amri
ya jana ya polisi, wakipiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa
ikiwemo vikao vya ndani ni muendelezo wa amri haramu na kitendo hicho
cha jana na vingine vilivyopita, ni mfano hai ya kwamba, nchi yetu
imeingia katika mfumo wa udikteta.
"Kwani,
kwa mujibu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1967;
udikteta ni utawala wa mtu mmoja au kikundi cha watu wachache
wanaofikiria kwamba, amri zao ndiyo sheria na wote wanaowapinga, hukiona
cha mtema kuni,” amesema Lissu.
Lissu
amesema kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya sasa pamoja na sheria zote
ikiwemo Sheria Na. 5 ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa, Sheria ya Maadili
ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2007 pia sheria za Jeshi la Polisi, hakuna
mahali ambapo polisi au rais anaruhusiwa kupiga marufuku mikutano ya
kisiasa.
“Anayetakiwa
kujulishwa kuhusu uwepo wa maandamano na mikutano ya hadhara ni Mkuu wa
Polisi Wilaya (OCD) na kama kuna tatizo kwa muda huo, anaweza kuelekeza
isifanyike kwa muda fulani lakini siyo Rais Magufuli wala Nsato,” amesema.
Wakati Lissu akisema hayo, Masha amesema,
“nimekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa miaka mitano, lakini sikuwahi
kupiga marufuku mikutano ya hadhara wala ile ya ndani. Nilifahamu kuwa,
kuna umuhimu wa watu kuzungumza, kukosoana na kuelimishana.
"Ni
vyema Rais Magufuli akajua, hii ni nchi ya kidemokrasia na kuna Katiba
na sheria ambazo kila mtu ni lazima afuate akiwemo yeye, matamko ya
kibabe ya Rais, Waziri wa Mambo ya Ndani na Jeshi la polisi ni kinyume
na sheria pamoja na Katiba yetu.”
Dk.
Mashinji, amesisitiza kuwa, Chadema kipo tayari kwa mazungumzo na
mamlaka yoyote ya serikali juu ya azma ya kufanya mikutano na
maandamano, ili mradi tu sheria na katiba ya nchi izingatiwe katika
mazungumzo hayo.
“Hatujafunga
milango ya mazungumzo na serikali, tunachosisitiza sisi ni kuwa hata
kama kuna mazungumzo yatafanyika, Katiba na sheria za nchi yetu lazima
zizingatiwe,” amesema Dk. Mashinji.
0 comments:
Post a Comment