Umoja
wa Wanawake Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania (UWASATA), umepinga
maandamano yasiyo na ukomo yaliyotanganzwa na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwa hayana tija kwa wananchi na Tifa kwa
ujumla.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa umoja
huo Cecilia Augustino, alisema maandamano hayo yanaashiria uvunjifu wa
amani ambayo ni urithi wa Taifa la Tanzania.
Alisema
wamefikisha tamko lao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis
Mutungi na kumtaka msajili kutoacha chokochocko hizo ziendelee kwani
zitasababisha kutoweka kwa amani nchini.
“Sisi
wanawake viongozi wa vyama vya Siasa Tanzania tunapinga azimio la
maandamano yasiyo na kikomo yanayoandaliwa na chama cha Chadema, hakika
maandamano hayo hayana tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla” alisema Hokororo na kuongeza:
“Mheshimiwa
Msajili, chokochocko hizi zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa
zikiachwa tu bila ya kukemewa tunaamini tunu yetu ya amani ambayo ni
urithi wetu tulioachiwa na waasisi wetu itatoweka”
Aliongeza
kuwa hatma ya maandamano hayo ni kuingia kwenye machafuko na hatimaye
mauaji na mateso kwa wanawake, watoto na walemavu, mambo ambayo
hawatakubali yatokee.
Alibainisha
kuwa wanawake viongozi wa vyama vya siasa wanaamini kuwa siasa ni
kushindana kwa hoja na si uvunjifu wa sheria kwa njia ya maandamano
yasiyo na tija kwa wananchi na Taifa.
Aliliomba
Baraza la Vyama vya Siasa kuhakikisha linawajibika katika kulinda
demokrasia, amani na ustawi wa jamii nzima ya Watanzania.
Katika
hatua nyingine, umoja huo unaojumuisha wanawake viongozi wa vyama 22
vya siasa nchini, umeomba kufanya kongamano la amani lenye lengo la
kuhamasisha amani na utulivu nchini.
Hivyo,
Hokororo aliwaomba viongozi wakuu wa nchi kuanzia Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, wadau wa amani na
mashirika binafsi kushirikiana na umoja huo kufanikisha kongamano hilo.
“Hakika
tunaumia wanasiasa wanapokuwa chanzo cha migogoro na vurugu kwa Taifa
letu.Hivyo tunamuomba Rais wetu tunajua ni msikivu aweze kuona namna
nzuri ya kutafuta suluhu ya mgogoro huu wa kisiasa” alisema Mwenyekiti Cecilia Hokororo.
Msajili
wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, tayari ameitisha Baraza la
Vyama vya Siasa Agost 30, mwaka huu ili kutoa fursa kwa pande vyama
husika kukaa meza moja na kujadili tofauti zilizopo na kuzipatia
ufumbuzi.
Naye
Makamu Mwenyekiti wa umoja huo Ziada Athumani alisema wanaunga mkono
hatua hiyo kwani ndio njia muwafaka ya pande husika ili kufikia muwafaka
kwa njia ya amani.
Katika
mkutano huo na waandishi wa habari, wanawake viongozi wa vyama vya
siasa waliwakilishwa na wenzao kutoka vyama vya Demokrasi Makini, ADA
TADEA na Chama cha Umoja wa Demokrasi ya Vyama Vingi (UMD).
0 comments:
Post a Comment