Nyasa. Safari
ya mwisho ya mbunge wa Mbinga Magharibi jana ilihitimishwa saa 9.25
alasiri wakati mwili wake ulipofunikwa na mfuniko mkubwa wa zege
uliobebwa na gari maarufu kwa jina la “kijiko”.
Haikuwa
kitu cha kawaida wakati gari hilo kubwa likishusha mfuniko huo wa zege
kwenye kaburi la mwimbaji huyo maarufu wa nyimbo za uhamasishaji za CCM
na kiongozi wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT), lakini majonzi
yaliwafanya waombolezaji kulichukulia tukio hilo kuwa la kawaida.
Safari
ya Komba, iliyoanza miaka 61 iliyopita kwenye kijiji cha Lituhi ambako
aliazikwa jana, ilikamilishwa kwa salamu mbalimbali ambazo zilielezea
ushupavu wa kapteni huyo mstaafu wa jeshi.
Mazishi
hayo yaliyohudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi
mbalimbaliwakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete na mkewe Salma, yalifanyika
katika makaburi ya Misheni,katika Kijiji cha Lituhi (Bundi) wilayani
Nyasa mkoani Ruvuma.
Nyuso
za majonzi zilitawala kwa waombolezaji waliojitokeza nyumbani kwa
marehemu, takriban mita 500 kutoka katika makaburi hayo na baadaye
katika misa iliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Lituhi,
ikiongozwa na Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki la Mbinga.
Kaimu
katibu wa Bunge, John Joel, akisoma wasifu wa marehemu, alisema Kapteni
Komba aliyefariki dunia Februari 28, mwaka huu akiwa njiani kupelekwa
Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, alikuwa anasumbuliwa na maradhi
ya shinikizo la damu na mara kadhaa Ofisi ya Bunge ilimpeleka India kwa
matibabu. Pia alikuwa na tatizo la kisukari ambalo ndilo lililochukua
maisha yake.
Mazishi
hayo yalishuhudiwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Edward Lowassa,
ambaye alikuwa Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Steven Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Utaratibu na
Bunge), Jenister Mhagama na mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi.
Wengine
ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Naibu Spika wa Baraza la
Wawakilishi, Ali Abdallah Ali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Uwanja wa ndege
Kwenye
Uwanja wa Ndege wa Songea, viongozi mbalimbali waliwasili kwa ndege za
kukodi na Lowassa ndiye aliyefungua mlango kwa ndege iliyotua saa 2:33
asubuhi akiambatana na mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani.
Haikupita
muda mrefu, ndege nyingine ilitua saa 2:50 ikiwa na Spika Makinda na
msafara wake uliomjumuisha mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe.
Saa
3:22 ilitua ndege iliyobeba ujumbe wa CCM ukiongozwa na Kinana. Wengine
waliokuwamo ni naibu katibu mkuu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba, katibu wa itikadi na uenezi, Nape Nnauye na mwimbaji wa
kikundi cha TOT, Khadija Kopa. Pia baadaye Rais Kikwete alitua na ndege
ya Serikali
MWANANCHI