Soko
la hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa kupitia udhamini wa benki ya NMB
imezindua shindano la uwekezaji lijulikanalo kama ‘DSE Scholar
Investment Challenge’ linalowahusisha wanafunzi kutoka vyuo vikuu ambapo
washindi wanatarajia kuibuka na kitita cha shilingi milioni 2 na nafasi
ya kufanya mafunzo kwa vitendo.
Shindano
hilo ambalo litadumu kwa miezi mitatu, litawakutanisha wanafunzi wa
vyuo vikuu ambao watapewa mitaji ya kielectroniki (Virtual Capital) ya
shilingi milioni moja na wao kufanya uwekezaji kwa njia ya kununua hisa
kwenye soko la hisa la Dar es Salaam.
Washindi
watatu watakaopatikana, watagawana kitita cha shilingi milioni 2 ambapo
mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 1, mshindi wa pili laki 6 na
mshindi wa tatu atapata shilingi laki nne. Washindi watapatikana
kutokana na faida watayoipata katika uwekezaji wao kwenye soko la hisa
na ushiriki wao kwenye majadiriano yanayoonyesha njia walizotumia
kufikia faida walizopata. Shindano hili litafanyika kwa njia ya mtandao
wa simu.
Hii ni
mara ya pili kufanyika kwa shindano hili kuendelea kupata udhamini
mzuri kutoka benki ya NMB, Lengo la shindano hili ni kuwahamasisha
wanafunzi kujenga utamaduni wa kuwekeza na kutunza akiba katika taasisi
za fedha.
Afisa
kutoka DSE – Aleck Ngoshani akiwasilisha mada kwa wanafunzi wa CBE
wakati wa semina za kuwahamasisha wanafunzi kushiriki shindano la DSE na
jinsi watakavyoweza kufanya uwekezaji kwenye soko la hisa la Dar es
Salaam.
Wanafunzi
wa chuo cha biashara cha CBE wakisikiliza mada kutoka kwa maafisa wa
DSE jinsi ya kushiriki shindano la DSE Scholar Investment Challenge.
Meneja
Mradi na Biashara wa soko la hisa la Dar es Salaam – Magabe Maasa
akitoa mada juu ya nafasi ya wanafunzi katika uwekezaji.


