Dar es SalaamYALE mambo ya kudhalilishana sasa yanaonekana kuendelea kushika kasi baada ya mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe kunaswa na kamera ‘noumaa’ za gazeti la Championi akimdhalilisha beki wa Simba, Juuko Murshid.
Tambwe raia wa Burundi amenaswa akimvuta kwa makusudi sehemu za siri beki huyo ambaye alipambana naye vilivyo katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyozikutanisha timu zao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wikiendi iliyopita na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Picha inamuonyesha Tambwe akifanya kitendo hicho ikiwa siku 53 tu baada ya yeye kukabwa na beki George Michael wa Ruvu Shooting na gazeti hili kuweka mambo hadharani.
Katika suala hilo, lililotokea katika mechi hiyo ya Yanga na Shooting Januari 17, mwaka huu Tambwe alilalamika kudhalilishwa na beki huyo huku akidai kuna mpango wa kuwavunja nguvu wageni wanaocheza soka nchini, lakini safari hii amenaswa akimdhalilisha mgeni mwenzake kwa kuwa Murshid ni raia wa Uganda.
Tambwe alielezwa kuhusiana na kitendo hicho cha unyanyasaji tena akikifanya ikiwa ni siku chache baada ya kulalamika anaonewa, akasema:
“Kwa kweli sijafanya hivyo, labda kama nilimshika kwa bahati mbaya.”
Alipoelezwa kuwa inaonekana alikusudia kwa mujibu wa picha, akajibu: “Mimi naona kama Simba wananifuatafuata, maana hata (Zacharia) Hans Poppe (Mwenyekiti wa Kamati ya usajili Simba), nimesikia akinishambulia redioni.
“Wao ndiyo wameniacha, basi waachane na mimi hasa Hans Poppe kwa kuwa sasa niko Yanga sipendi ugomvi. Mbona mimi siwatangazi wakati ninawadai dola elfu saba?
“Sasa nimeamua kulifikisha suala hili Fifa wanilipe tu fedha zangu. Naona kama si wastaarabu.”
Wakati Tambwe anasema hayo, Murshid wa Simba alipotafutwa, yeye alionekana kuwa mwoga kujieleza, lakini baadaye alifunguka.
“Kweli, alikuwa akijaribu kunishika mara kadhaa. Lakini niliendelea kupambana kwa kuwa mpira una mbinu nyingi.“Si jambo zuri lakini mpira naujua, kila fowadi ana mbinu zake, mimi nilichohakikisha ni kufanya vizuri.”
Tukio jingine la unyanyasaji alifanyiwa mshambuliaji wa Simba, Elius Maguri na gazeti hili likamnasa Juma Nyosso wa Mbeya City ambaye amefungiwa mechi nane sambamba na Michael aliyemkaba shingoni Tambwe aliyefungiwa mechi tatu.