TIMU za Yanga, Simba na Azam zilipewa nafasi ya kushiriki
michuano ya kombe la Kagame yalipofanyika kwa mara ya mwisho hapa nchini
mwaka 2012 kwasababu zilishika nafasi tatu za juu.
Lakini mwaka huu Tanzania ikitarajiwa kuwe mwenyeji, CECAFA
wametoa nafasi tatu kwa timu za Tanzania na kwa namna ligi ilivyoisha
msimu uliopita, Azam, Yanga na Mbeya City zinatakiwa kushiriki, lakini
Mbeya City fc licha ya kushika nafasi ya tatu msimu uliopita imepigwa
chini na nafasi yake wamechukua Simba walioshika nafasi ya nne.
Katibu mkuu wa Shirikisho la soka nchini, TFF, Selestine
Mwesigwa amesema timu yenye uhalali wa moja kwa moja ni Azam fc, lakini
unapokuwa mwenyeji unapewa nafasi mbili nyingine, kwahiyo mshindi wa
pili na watatu wanatakiwa kuingia, lakini Mbeya City hawatakuwepo.
“Mbeya City walistahili, lakini niseme ukweli, tumeamua
kumchukua Simba, kwanini? kwasababu ya rekodi yake. Amekuwa bingwa mara
nyingi wa mashindano haya, kwahiyo ana nafasi yake sio katika Tanzania
tu bali ukanda mzima, na huwezi kumuondoa”. Amesema Mwesigwa na
kuongeza: “Mwaka jana baada ya Azam kujitoa kushiriki mashindano mapya
ya kagame, tuliwapa Mbeya City nafasi”.
Hata hivyo ukiangalia kwa jicho la ndani, TFF na CECAFA hawawezi kuwanyima Simba kwasababu za kimaslahi.
Yanga na Simba zinaposhiriki michuano yoyote nchini watu
wengi wanajitokeza kutazama mpira, hivyo kuziweke timu hizi ni
kutengeneza namna bora ya kupata mapato.
Bahati nzuri pia hakuna kanuni inayobana kwamba lazima timu
tatu za juu zishiriki, nchi mwenyeji inaweza kuchagua timu yoyote kwa
vigezo itavyojiwekea.