Kikosi cha timu ya Yanga
kimeondoka usiku huu kuelekea Tunisia kwa ajili ya mchezo wake wa
marudiano wa kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Etoile du Sahel
utakaopigwa nchini humo siku ya Jumamosi.
Kikosi cha Yanga kimeondoka na
msafara wa watu 50 wakiwemo wachezaji, viongozi, benchi la ufundi pamoja
na wanachama na wapenzi wa timu hiyo. Msafara huo wa Yanga unaongozwa
na mjumbe wa kamati ya utendaji ya TFF Ayubu Nyezi, wameondoka kwa ndege
ya shirika la Emirates kupitia Dubai hatimaye kutua Tunisia.
Kocha mkuu wa timu hiyo Hans
van der Pluijm amesema, hawana cha kupoteza kwenye mchezo huo hivyo
wanahitaji kuibuka na ushindi ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya
pili kwa ukubwa kwa ngazi ya vilabu barani Afrika.
“Hatuna cha kupoteza kwenye
mchezo huo, tulitoka sare ya kufungana goli 1-1 tukiwa nyumbani hivyo
tunahitaji kupata ushindi au sare ya magoli kuanzia mawili ili tuweze
kusonga mbele. Tumejipanga vizuri kwa hili na wachezaji wote tunaokwenda
nao wanatambua umuhimu wa mchezo huo”, amesema Pluijm.
“Etoile ni timu nzuri na
inauzoefu mkubwa kwenye michuano ya Afrika na kila mtu aliona aina ya
soka walilocheza hapa, tunawaheshimu na tumejipanga ili kukabiliana nao
na kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo”, aliongeza Pluijm.
“Ni lazima tucheze soka la
kushambulia na kupata magoli ya mapema lakini wakati huohuo tunatakiwa
kuwa makini sana kuhakikisha haturuhusu kufungwa goli, nimezungumza na
wachezaji na kila mtu anajua majukumu yake. Najua kwenye soka lolote
linaweza kutokea na tukasonga mbele kwa hatua inayofuata”, alimaliza
Pluijm.