………………………………………..
Joto la ubunge katika jimbo la Arusha
mjini limezidi kupanda mara baada ya Kada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)
mkoani Arusha,Kim Fute kutangaza rasmi kuwania ubunge katika jimbo hilo
endapo akipewa ridhaa na chama chake kugombea.
Kim,amejitokeza kutangaza azma hiyo
ikiwa ni siku chache baada ya makada wengine wa CCM ambao ni Phillemon
Mollel,Victor Njau,Thomas Munisi,Deo Mtui,Godfrey Mwalusamba kutangaza
nia ya kuwania jimbo hilo linashikiliwa na mbunge wake,Godbless Lema
ambaye tayari ametangaza kugombea tena.
Akizungumza na gazeti hili jijini
hapa,Fute alisema kuwa amesukumwa na dhamira ya kuwania ubunge katika
jimbo hilo mara baada ya kutathmini na kubaini ya kwamba jimbo hilo
linakabiliwa na tatizo la ombwe la uongozi.
Alisema kwamba amejipima vya kutosha
na kubaini ya kwamba ana sifa za kutosha za kuwawakilishi wakazi wa
jimbo la Arusha mjini ambao alidai kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa
viongozi bora wa kuwawakilisha.
Kada huyo alisisitiza kwamba miongoni
mwa mambo ambayo atakwenda kuyafanyia kazi pindi akifanikiwa kuwa
mwakilishi wa jimbo hilo ni pamoja na kushughulikia suala la usalama wa
mji wa Arusha ambalo alidai tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka
2005 mji huo umeandamwa na matukio mbalimbali kama maandamano,vurugu na
mambomu.
Alisema kuwa mji wa Arusha ni mji wa
kimataifa na pia una fursa nyingi kama kitovu cha utalii hapa nchini na
duniani hivyo atajikita kuhakikisha anasimamia hali ya kurejea kwa
usalama ili biashara hiyo iweze kufanyika kwa uwepesi kwa kuwa
inachangia pato kubwa la taifa.
“Arusha ni mji wa kimataifa na una
fursa nyingi kama biashara ya utalii ambayo inachangia pato kubwa la
taifa lakini usalama ni hafifu na unaharibu kwa kiasi kikubwa hivyo
nitajikita kuhakikisha hali ya usalama inarejea”alisema Kim
Hatahivyo,alibainisha kwamba mbali na
usalama pia atahakikisha anakutana na makundi mbalimbali ya viongozi wa
dini zote,waandishi wa habari pamoja na wadau wa maendeleo jijini hapa
ili kuangalia namna ya kuuweka mji wa Arusha katika hali ya utulivu.