NIPASHE
Serikali imeondoa Muswada wa Sheria ya Haki ya upatikanaji habari wa mwaka 2015 Bungeni huku ikiahidi kwamba Muswada huo utasomwa katika Bunge la kwanza la Serikali ijayo.
Akitoa taarifa ya kuondolewa kwa Muswada huo Waziri Prof. Mark Mwandosya alisema Muswada huo
“Serikali imetafakari maoni ya kamati na kuafiki muswada uendelee kufanyiwa kazi hadi hapo kamati itakapokamilisha kazi yake ipasavyo na kuwakilisha maoni yake Bungeni,“alisema Prof. Mark Mwandosya.
Juni 22 2015, wadau mbalimbali wa habari waliokutana Dar kupinga muswada huo, kwa kile kinachoelezwa kuwa unakiuka Sheria za Kimataifa, Katiba ya nchi na unawanyima haki raia kupata taarifa.
NIPASHE
Jitihada za Mbunge Andrew Chenge kutaka asihojiwe na Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma ‘zimekwaa kisiki’ baada ya shauri la pingamizi lake alilofungua Mahakama Kuu kutupwa.
Chenge ni miongoni mwa watumishi wa Umma waliotajwa katika kashfa ya mgawo wa fedha za akaunti ya Tegeta ESCROW zilizotolewa na mfanyabiashara James Rugemalira.
Februari 25, mwaka huu Chenge baada ya kusomewa mashtaka tisa na baraza kabla ya kuhojiwa aliwasilisha pingamizi la amri ya Mahakama linalodai kuzuia Mamlaka zozote kujadili au kufanya kazi ya suala lolote la ESCROW.
Siku iliyofuatia Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Mstaafu Hamisi Msumi alitupilia mbali pingamizi hilo na kueleza kuwa Baraza lina haki ya kumhoji Chenge, lakini hakukubaliana na uamuzi huo na kusema anakata rufaa Mahakama Kuu kuomba mwongozo wa Mahakama kuhusu kuendelea kujadiliwa suala hilo au la.
Jana Jopo la Majaji wa Mahakama hiyo jijini Dar es Salaam, Gadi Mjema, Fauthi Twaibuna Rose Teemba walisikiliza mapingamizi yaliyowekwa na Chenge na washtakiwa Juni 1 na 2, mwaka huu, na maamuzi yakatolewa kwamba kesi hiyo imetupiliwa mbali Baraza hilo lina uwezo wa kuendelea na shauri dhidi ya Chenge.
“Nimetendewa haki, huo ndio uamuzi wa Mahakama nimeridhika nao sina la kusema,” alisema Chenge huku akicheka.
Ofisa Habari wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Johanither Barongo amesema wamepata taarifa za maamuzi ya Mahakama na watatoa taarifa zaidi Jumatatu.
MWANANCHI
Jana ilikuwa siku ya aina yake kwa msanii Faiza Ally na mzazi mwenzake, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’. Wakati Faiza akimwaga chozi katika chumba cha habari katika gazeti la Mwananchi alipofika kutoa ujumbe wa kuomba radhi kutokana na vazi la kitenge lenye kambakamba alilovaa siku ya KTMA 2015, Sugu alimwaga chozi bungeni Dodoma alipowataka wabunge wasijadili mambo yake ya faragha.
Faiza akiwa amevaa baibui na kufunika kichwa kwa hijabu, alieleza kwamba anajutia kutokana na kuvaa vazi lililoonyesha sehemu kubwa ya makalio yake alilodhani ulikuwa ubunifu.
“Siwezi kurudia kosa, nitakuwa makini zaidi katika mavazi yangu, Wasanii wengi ni wabunifu na hufanya mambo kwa nia ya kufurahisha mashabiki kama ambavyo amekuwa akifanya Joti kuvaa nguo za kike na kupaka rangi ya mdomo, hivyo mavazi yangu yalikuwa na lengo la kutoka tofauti mbele za mashabiki wangu, lakini kwa yaliyonikuta hasa kwenye vazi la Kili niliomba msamaha kwa jamii na bado naomba wanisamehe”, alisema Faiza Ally akiwa kwenye Ofisi za Gazeti la Mwananchi huku akitokwa machozi.
Mbunge Sugu aliongea Bungeni kwa uzito akieleza suala lote; “Kwa taarifa tu pamoja na Mahakama kunipa haki, mtoto bado yuko kwa mama yake kwa sababu mimi ni mstaarabu, nimetoa nafasi ili majadiliano ya kifamilia yafanyike. Naomba mjadala huu usiendelee zaidi ya hapa,” alisema Sugu ambaye alionekana akifuta machozi akisikitishwa suala hilo kuzua mjadala bungeni.
MWANANCHI
Prof. Mark Mwandosya ambaye anawania kuteuliwa na CCM kugombea urais amemtakaEdward Lowassa kujiunga na kambi yake kwa kuwa makada wengine wanne kwenye mbio hizo wanamuunga mkono japo wawili kati ya makada hao wanne wamekana kumuunga mkono.
Mwandosya aliwataja Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri Steven Wasira, Samuel Sittana Bernard Membe kwamba wanamuunga mkono na hivyo kumshauri Lowassa kujiunga na kambi yake.
“Kama wengi wananiunga mkono, aliyebakia basi atakuwa ni ndugu yangu, rafiki yangu, Edward Lowassa. Naye angesema hivyo ingerahisisha sana kazi ya Chama, ingepunguza sana kazi, makundi yangekuwa yameisha,” alisema Mwandosya baada ya kurejesha fomu za kuomba CCM impitishe kugombea urais.
Prof. Mwandosya alisema mchakato huo umewafanya wanaoomba Urais kuwa marafiki zaidi licha ya kupigana vijembe, huku akisema ingekuwa nchi nyingine wangefanyiana vurugu.
“Namshukuru Benard Membe ambaye ametangaza kwamba yeye ameona katika orodha yote ya watu 40, kama si yeye basi ataniunga mkono.. Mheshimiwa Pinda, amelizungumzia hili katika vituo kama si kimoja viwili kuwa moyo wake utakuwa na furaha kama Profesa Mwandosya anaweza kuteuliwa na chama”—Prof. Mwandosya.
HABARI LEO
Mbunge David Kafulila amemwandikia barua Spika Anne Makinda kumwomba aitake Serikali iwasilishe hoja juu ya sakata la mabehewa feki ya Shirika la Reli Tanzania ili ijadiliwe na Wabunge.
“Kwa kuzingatia taarifa iliyotolewa na Mamlaka inayosimamia Udhibiti na Manunuzi , ununuzi wa mabehewa uliofanywa na Kampuni ya India ulikuwa na mapungufu… kwa sababu Waziri wa Uchukuzi alikiri kupokea Ripoti hiyo, tunaomba iletwe Bungeni”—David Kafulila.
Katika barua hiyo Mbunge huyo alisema mapungufu mengine ilikuwa ni Kampuni hiyo kulipwa pesa kabla haijayafikisha Mabehewa hapa nchini.
Kafulila alisema sakata hilo linahusisha sh. Bilioni 230 na halipaswi kukaliwa kimya