Leo Azam inacheza mchezo wa nusu
fainali ya Kagame kwa mwaka 2015 ikikutana na timu ya KCCA ya Uganda
kwenye mchezo ambao utaamua ni timu gani kati ya hizo itaingia fainali
ya mashindano hayo kwa mwaka huu.
Mpaka sasahivi Azam haijaruhusu
wavu wake kutikiswa na timu yoyote ndani ya dakika 90, hii imekuwa timu
pekee kwenye mashindano ya mwaka huu kuingia kwenye hatua ya nusu
fainali ikiwa haijafungwa goli hata moja mpaka sasa na kujiwekea rekodi
kwenye michuano hii. Lakiki kwa upande mwingine Azam inaungana na Gor
Mahia kuwa timu mbili pekee ambazo zimeingia kwenye nusu fainali zikiwa
hazijapoteza mchezo hata mmoja tangu ngazi ya makundi.
Azam iliyoiondosha Yanga kwenye
michuano hii zilipokutana kwenye hatua ya robo fainali na kuitupa timu
hiyo nje ya mashindano kwa changamoto ya mikwaju ya penati 5-3
imefanikiwa kufunga magoli tisa mpaka sasa ikianza kwa kuifunga KCCA
goli 1-0, ikapata ushindi mwingine wa goli 3-0 dhidi ya Malakia FC kisha
kuifumua Adama City kwa goli 5-0 na kutinga hatua ya robo fainali na
kuitoa Yanga kwa penati.
Azam ilikuwa kundi moja na KCCA
ya Uganda zote zikiwa zimepangwa kundi C na Azam walishinda mchezo wao
dhidi ya KCCA kwa goli 1-0 goli lililofungwa na John Bocco ‘Adebayor’.
Hivyo mchezo wa leo utakuwa ni wa kisasi au ubabe, KCCA wakitaka kulipa
kisasi kwa kuifunga Azam iliyowafunga kwenye mchezo wa kwanza wakati
Azam itakuwa inataka kuendeleza ubabe wa kuifunga tena KCCA.
Mchezo mwingine utakuwa ni kati
ya Gor Mahia dhidi ya Khartoum ambazo pia zilikuwa kwenye kundi moja la A
na timu hizo zilipokutana zilitoka sare ya kufungana kwa goli 1-1. Gor
Mahia haijapoteza mchezo hadi sasa, imefika nusu fainali kwa kuisukuma
nje ya mashindano timu ya Malakia kwa kuifunga goli 2-1 kwenye mchezo wa
robo fainali. Khartoum yenyewe imepoteza mchezo mmoja ambapo ilifungwa
na Yanga kwa goli 1-0 kwenye hatua ya makundi.
Khartoum imetinga hatua ya nusu
fainali kwa kuiondosha timu ngumu na kongwe kwenye michuano ya Kagame
APR FC ya Rwanda kwa kuipa kichapo cha mbwa mwizi kwa kuibugiza goli 4-0
na kuwa timu ambayo imefunga magoli mengi hadi sasa ikiwa imefunga
magoli 12. Mechi ya kwanza ilianza kwa ushindi wa goli 5-0 mbele ya
Adana City, 2-1 dhidi ya KMKM, 1-1 dhidi ya Gor Mahia na 4-0 ilipochuana
na APR.
Mchezo kati ya Gor Mahia dhidi ya
Khartoum unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na walimu wote kutumia mbinu
mbalimbali ambazo zimekuwa zikitoa matokeo wanayo yataka. Kwesi Appiah
kocha wa Khartoum amekuwa na mbinu nyingi sana za kupata matokeo licha
ya timu yake kuwa haipewi nafasi ya kufanya vizuri kwenye mashindano
haya.
Ni kocha mwenye uzoefu wa hali ya
juu na ameshakutana na mechi kubwa na ngumu nyingi kuliko ilivyo kwa
Kagame.Wakati kocha wa Gor Mahia Frank Nuttal anajivunia rekodi yake ya
kutopoteza mcheo na Gor Mahia.


0 comments:
Post a Comment