Dar/Dodoma. Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano ambalo uhai wake unaisha Julai 9, linaonekana dhahiri kwenda mrama baada ya wabunge 23 kumlazimisha Spika kuwatimua kikaoni wakipinga kuwasilishwa kwa miswada mitatu kwa hati ya dharura.
Kwa siku tatu mfululizo, Spika Anne Makinda
amekuwa akipata shida kuendesha chombo hicho cha kutunga sheria kutokana
na mbinu waliyogundua wapinzani ya kupiga kelele kukwamisha shughuli za
Bunge.
Juzi, kiongozi huyo wa Bunge aliamua kuwapeleka
wabunge 11 mbele ya Kamati ya Maadili kwa makosa ya kudharau kiti chake
na chombo hicho kikaibuka na adhabu ya kuwafungia wabunge wanne
kutohudhuria vikao vyote vilivyosalia, wengine wawili kufungiwa vikao
viwili.
Jana, hali iliendelea kuwa ya mapambano baada ya
wabunge hao kuhoji uhalali wa adhabu hiyo, huku wakihoji sababu ya
miswada hiyo kuwasilishwa kwa dharura.
Ezekia Wenje, mbunge wa Nyamagana, aliendelea
kubishana na Spika na kusababisha atangaze kumzuia kushiriki vikao
vitano, uamuzi uliosababisha wabunge wengine wa upinzani kusimama na
kupiga kelele wakitaka nao waadhibiwe.
Spika Makinda alisema kuwa ametumia kanuni ya 74(i) kuwatimua wabunge hao kwa kushindwa kuheshimu kiti kwa kupiga kelele.
Wakati wabunge waliopewa adhabu wakiongezeka,
wenzao ambao hawakuwapo sasa wamehamasishwa kwenda mjini Dodoma
kuendelea na walichokiita mapambano, hali inayoweza kusababisha Bunge
hilo likavunjwa likiwa limepukutika wabunge wa upinzani.
Sakata lilivyoanza
Kabla ya kikao kuanza jana asubuhi, Wenje aliomba
mwongozo wa Spika na baada ya kupewa nafasi, alipinga adhabu waliyopewa
wabunge saba juzi akisema wameonewa na kuhoji sababu za mbunge wa Mbozi,
David Silinde kuzuiwa kuingia wakati hakutajwa kwenye taarifa ya Kamati
ya Maadili iliyopendekeza adhabu hizo juzi.
Hata hivyo, Spika Makinda alimjibu kuwa hilo
lilitokana na makosa ya uchapaji, lakini Silinde alimtaja na ni miongoni
mwa waliokuwa wakifanya vurugu juzi na aliitwa kuhojiwa kwenye maadili.
Wenje aliendelea kupinga huku akibishana na Spika,
ndipo zogo likaibuka upya na Spika akaagiza atolewe nje ya Ukumbi wa
Bunge na asihudhurie vikao vitano kuanzia jana.
0 comments:
Post a Comment