Timu
ya Gor Mahia ya Kenya imefanikiwa kutinga nusu fainali ya michuano ya
Kagame Cup baada ya kuitandika Malakia FC ya Sudan Kusini kwa goli 2-1
kwenye mchezo wa robo fainali uliopigwa jioni ya leo kwenye uwanja wa
Taifa.
Godfrey Walusimbi amefunga magoli
yote mawili ya Gor Mahia na kuivusha timu hiyo hadi kwenye hatua ya
nusu fainali. Ilichukua dakika mbili tu Gor Mahia kuandika goli la
kwanza lililofungwa na mshambuliaji raia wa Uganda Godfrey Walusimbi
kabla ya kufunga goli lingine dakika ya 27 kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili Malakia
walionekana kucheza kwa nguvu na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara
wakitafuta goli ambapo walifanikiwa kupata goli la kufutia machozi
kupitia kwa Thomas Jacob Mathew. Kipindi cha pili Gor Mahia ilionekana
kuridhika na matokeo ya kipindi cha kwanza kwa kucheza mpira wa taratibu
huku wachezaji wake wakionekana hawahitaji tena kufunga goli.
Matokeo hayo ya leo yanazifanya
Khartoum National Club na Gor Mahia kukutana kwenye mchezo wa nusu
fainali, ikumbukwe timu hizi zilikutana kwenye hatua ya makundi zote
zikiwa Kundi A na kutoka sare ya kufungana goli 1-1. Mchezo wao wa nusu
fainali utakuwa ni wa pili kwenye mashindano haya ya Kagame mwaka huu.
Kesho pia itapigwa michezo miwili
ya robo fainali , mchezo wa kwanza utakuwa saa 7:45 mchana kati ya KCCA
ya Uganda dhidi ya Al Shandy ya Sudan wakati mchezo unaosubiriwa kwa
hamu kubwa na wapenzi wengi wa soka ni ule wa Azam FC dhidi ya Yanga
mchezo utakaopigwa majira ya saa 10:00 jioni michezo yote ikipigwa
kwenye uwanja wa Taifa.
Michezo ya nusu fainali itapigwa
siku ya Ijumaa wakati mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu pamoja na
mechi ya fainali itachezwa siku ya Jumapili.
0 comments:
Post a Comment