Tanga. Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa dini nchini kuwahimiza waumini wao kuwachagua wanasiasa wasiokuwa waovu, wasiofanana na uovu au hata kuukaribia.
Amewataka kuepuka makundi ya kisiasa na wasiwape mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu katika kutafuta madaraka kwa thamani yoyote na wawakemee wale wanaotaka kupata madaraka kwa gharama yoyote.
Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 125 tangu kuingia kwa injili katika ukanda wa Pwani ya Tanga na Milima ya Usambara uliofanyika katika Viwanja vya Mbuyukenda jijini hapa.
“Wanasiasa wanaotaka madaraka kwa njia yoyote ile, muwanyanyapae, wakatalieni kwa macho makavu, hawa si watu wema watatufikisha pabaya,” alisema Rais Kikwete.
Alisema hayo baada ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga kumweleza kwamba akiwa mkuu wa nchi anao wajibu wa kuhakikisha Taifa linavuka kwa amani na usalama katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema katika kipindi hiki, viongozi wa madhehebu ya dini wasijiingize katika makundi ya wanasiasa kwa sababu mambo yakiharibika itakuwa hakuna pa kukimbilia.
Aliwataka viongozi wa dini watumie nyumba za ibada kuliombea Taifa livuke salama katika kipindi hiki kigumu badala ya kuwapangia vyama au viongozi wa kuwachagua.
“Tunawategemea kuwahimiza na kuwakumbusha kutumia haki na wajibu wao vizuri, muwahimize na kuwakumbusha kuwa watatakiwa kufanya mambo matatu muhimu; Kwanza, kujiandikisha, pili, kujitokeza kwenda kupiga kura na tatu kuchagua viongozi wazuri, wasiokuwa waovu, wasiofanana na uovu na kuukaribia uovu, watakaosukuma mbele gurudumu la maendeleo na kujali masilahi mapana ya jamii husika na nchi yetu.”
“Viongozi wa dini muwe kama mimi, nina wagombea wa urais 42, kama nitaonyesha kuwa upande wa mgombea yeyote kati yao, basi nitakuwa nimeharibu mchakato mzima wa uchaguzi.
“Tusiwape mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu kuwafarakanisha Watanzania. Tuendelee kukemea matumizi mabaya ya fedha, rushwa, hila, ghiliba na hujuma katika uchaguzi. Tunapaswa kufanya hivyo tena zaidi sasa, wakati wa michakato ya ndani ya vyama vya siasa na baadaye wakati wa uchaguzi,” alisema.
Alisema hiki ni kipindi nyeti na kwamba, viongozi wa dini pamoja na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kufahamu kuwa Tanzania haina kinga ya milele ya amani na utulivu, kama itavurugwa haitakuwa lulu ya Afrika tena kama ilivyo sifa yake.
“Tuwakemee wanasiasa wapenda madaraka kwa gharama yoyote, ambao watataka kutumia fedha kununua ushindi au ubaguzi wa rangi, kabila, dini na kadhalika, kuwabagua wapinzani wao na kujijenga kisiasa. Nawaomba msiwasikilize wala kuwaendekeza kwani mchezo wao ni mauti yetu. Wakatalieni kwa macho makavu na kwa kweli muwanyanyapae,” alisema.
0 comments:
Post a Comment