Mwezi Juni hadi Agosti ni miezi nyeti katika soka na hususan kwa wale mashabiki wa ligi kubwa tano duniani. Miezi hii ni kipindi ambacho timu, mashabiki pamoja na vyombo vya habari huwa macho kujua nani anakwenda wapi na nani wanamhitaji.
Lakini swali hapa ni kwamba, kwanini ni ngumu kukuta katika picha za nje za magazeti kipindi hiki cha usajili kuna sura za mabeki?
Mfano angalia ambavyo jina la Raheem Sterling, Harry Kane, Paul Pogba na washambuliaji wengine yalivyotawala katika magazeti ya michezo? Kwanini hatuoni mabeki? Ukiachilia mbali mlinzi wa Real Madrid, Sergio Ramos na golikipa David de Gea wa Manchester United, bado hata bei zao hazitajwi kuwa kubwa.
Sio kwamba walinzi hawasajiliwi, la hasha! Ila hawana thamani hii wanayopewa akina Paul Pogba na Raheem Sterling.
Kumbe mwisho wa haya yote tunapata jibu kwamba kumbe soka ni mchezo wa matokeo. Ndio maana Liverpool wamemsajili mlinzi chipukizi wa Southampton Nathael Clyne kwa pauni 12m huku wakimsajili mshambuliaji wa brazil Roberto Firmino kwa pauni 29m.
Leo hii klabu ya Manchester United hawako tayari kutoa zaidi ya pauni 35m kwa mlinzi wa kati wa Real Madrid, Sergio Ramos lakini usishangazwe wakitoa pauni 75m kwa mshambuliaji Gareth Bale wa klabu hiyo hiyo ya Madrid.
Mpira ni mchezo wa ushindi, yaani magoli. Ndio maana sijashtushwa na usajili wa pauni 12m wa mlinzi mbrazil kutoka Atletico Madrid, Miranda wa kwenda Inter lakini nitashangaa kuona mshambuliaji wao Arda Turan akiuzwa kwa pungufu ya pauni 25m.
Kimsingi hapa ni namna mfumo wa mpira unavyobadilika, katika ‘modern game’ walinzi wamebadilishiwa majukumu na kwamba siku hizi mashambulizi ya timu huanzia kwa mabeki. Walinzi wa pembeni siku hizi wamekuwa na kazi ndogo zaidi ya ulinzi kuliko kushambulia kutokea pembeni.
Mlinzi Dany Alvez ameonekana mara nyingi katika nusu ya pili ya eneo pinzani awapo uwanjani, lakini hali hiyo utaikuta pia kwa Philip Lahm wa Ujerumani. Mpira ni magoli, ni ushindi. Ndio maana Barcelona walitoa pauni 75m kumsajili Luis Suarez lakini kamwe hawawezi kutoa hata pauni 50m kumsajili mlinzi Diego Godin ama Vicent Kompany.
Hizo pamoja na sababu nyingine za matangazo ya kibiashara hufanya timu kutoa macho zaidi kuwanunua wachezaji wa kiungo na ushambuliaji kwa ada kubwa zaidi ya mabeki.
Thamani ya watu wa ulinzi inashuka na pengine ndio maana Sepp Blatter alimpa tuzo ya mchezaji bora wa dunia Cannavaro wa Italia mwaka 2006 ili kujaribu kuinua thamani yao katika mchezo wa soka.
Pengine watu watasema hii ni Ulaya tu? Hapana ni kila sehemu ya dunia hivi sasa. Kwani hatuoni magazeti yetu ya hapa bongo? Vichwa vya nje vimepambwa majina ya akina Kaseke, Okwi, Busungu na Niyonzima, lakini kwanini sio Oscar Joshua? Mpira ni magori, ushindi.
0 comments:
Post a Comment