Rafa Benitez ameanza kazi yake kwa ‘ sare ya kuchukiza’, Estadio El Molinon dhidi ya Sporting Gijon. Gareth Bale alibeba majukumu ya mshambulizi wa kati, Cristiano Ronaldo, Jesse, Isco, Ton Kroos na Luka Modrid kwa pamoja walianza kama wachezaji sita wa nafasi za kiungo na ile ya mashambulizi lakini walikutana na timu iliyocheza kwa ku-jihami muda wote na kushindwa kufunga.
MWELEKEO MBAYA…
Mara baada ya kuchukua nafasi ya Mtaliano, Carlo Ancelotti, Benitez alisema wazi kuwa, Bale ndiye atayecheza katika eneo la kati katika safu ya mashambulizi na si Cristiano Ronaldo ( mfungaji bora wa klabu kwa miaka mitano mfululizo). Timu hiyo ilishindwa kufunga magoli ya kutosha katika michezo ya maandalizi.
C.Ronaldo amekuwa mbali na nafasi iliyompandisha ‘ chati’ na jambo litaendelea kuisumbua Real ya Benitez kwa kuwa ushindani binafsi kati ya Leonel Messi na Cristiano ndiyo huchangia mafanikio ya ndani ya uwanja ya klabu za FC Barcelona na Real Madrid. Benitez anajaribu kumuweka Bale katika daraja moja na kina C.Ronaldo na Messi kwa kuamini kuwa kama Bale atafunga mfululizo atakuwa ‘ levo’ ya Messi.
Hakika mwalimu huyo wa zamani wa Valencia, Liverpool, Chelsea na SS Napoli atakuwa anajipeleka kama ‘ mwelekeo mbaya’ yeye mwenyewe. Cristiano hajawahi kulalamika kuhusu nafasi yake mpya lakini kama mpinzani wake binafsi, Messi atafunga magoli mfululizo bila shaka zitaanza tetesi za kuwepo kwa ‘ bifu’ kati ya Rafa na mwanasoka huyo bora wa dunia mara tatu.
Real ilipiga jumla ya mashuti 27 kwa muda wote wa mchezo lakini, ni mashuti 8 tu yalikuwa ya hatari. Benitez alimuanzia nje, James Rodriguez na hakuwa na mshambulizi majeruhi, Karim Benzema na timu yake ikamiliki mchezo kwa asilimia 67.
Unaweza kushawishika na kusema ni mapema mno kumnyoshea kidole mwalimu huyu mshindi wa mataji ya ligi ya mabingwa ulaya na michuano ya Europa League lakini rekodi yake kimahusiano na wachezaji nyota si nzuri na Cristiano ni mchezaji asiyehofu kusema chochote Real inapofanya vibaya ama yeye mwenyewe kupangwa katika nafasi itakayo mnyima magoli.
Bale ni ‘mtambo wa mabao’ aliwahi kubeba majukumu ya mshambulizi wa kati na katika timu ya Tottenham Hospur na kukaribia kushinda tuzo ya ufungaji bora wa ligi kuu England msimu wa 2011/12. Anaweza kubeba majukumu hayo ya ufungaji katika timu hiyo ya Santiago Bernabeu. Kuzungukwa na viungo wenye ‘ macho makali’ kama, Isco, Modrid, James na Kroos ni jambo linaloweza kumpatia magoli mengi.
Lakini, je, Cristiano atatoa ushirikiano kwa Bale na kumsaidia kufunga?. Messi ameweza kuwanyanyua, Neymar Jr na Luis Suarez katika timu ya Barcelona. Sababu kubwa ni kujishusha kwa mastaa wa Brazil na Uruguay na kuamua kucheza vile anavyotaka Muargentina huyo.
Mwanzoni kabisa mwa msimu uliopita, Luis Enrique aliingia katika mzozo na Messi kwa uamuzi wa mwalimu huyo kumpanga Suarez katika nafasi ya mshambulizi wa kati. Enrique akamrudisha Messi katika eneo alilozoea na akapata msimu wa kwanza wenye mafanikio makubwa kwa kutwaa mataji matatu kwa mpigo ‘ treble’.
Lugha ya Mwili’ kutoka kwa Cristiano Ronaldo wa sasa pale Real inazungumza bado anahitaji kubeba majukumu ya mshambulizi wa kati. Benitez anapaswa kurudia baadhi ya nyakati zake nzuri pale Liverpool, 2004/05 alipochukua timu ‘ kabambe’ iliyoandaliwa na Mfaransa, Gerlad Houllier na kuipata ubingwa wa Mabingwa ulaya.
Carlo, ameacha timu nzuri Santiago Bernabeu. Aliweza kuwapanga, C.Ronaldo, Bale, Benzema, James, Isco/Modric na Kroos na timu ilicheza bila matatizo hata katika gemu kubwa. Wakati fulani, Cristiano na Bale walitajwa kuwa na mahusiano mabaya uwanjani-kutopeana pasi, na jambo hilo limewahi kujitokeza ila Carlo aliweza kuwatuliza na kucheza kwa ushirikiano mkubwa.
Kumnyima uhuru Cristiano Ronaldo ni sawa na kuinyima mabao Real Madrid na hili litakuwa jambo la kwanza ku-yumbisha mahusiano ya Benitez na mchezaji huyo na pengine hadi kwa mashabiki wanazi wa timu na rais wa klabu, Florentino Perez. Makundi yote matatu ( Cristiano, wanazi wa klabu na Perez) hawana ‘ aibu’.
Kama, Bale hatafunga na Real kupata magoli ya kutosha bila shaka, Benitez atasemwa kuwa hana mbinu bora. Atakuwa amejipeleka mwenyewe katika mlango wa kutokea. Kama, Bale atafunga litakuwa jambo la sifa kubwa kwake kwani atakuwa amemtengeza mchezaji bora wa dunia, wote wawili ( Bale na Benitez) watatembea ‘ vifua mbele’ wakati Cristiano akiinamisha uso wake chini.


0 comments:
Post a Comment