Nikiamini hali yako ni njema, karibu sana kwenye ukurasa huu ili kuweza kuburudika na habari moto moto za kimichezo ambazo pengine unaweza kuzikosa sehemu nyingine. Binafsi mwenyezi Mungu amenijalia afya tele na hata jana nilifanikiwa kuwaona Waholanzi wakifundishwa adabu na Waturuki na hata yale niliyo yaandika kwenye makala iliyopita kuhusu uwezekano wa Uholanzi kutazama michuano ya Euro kwenye Luninga huenda yakatimia. Pia Mwenyezi Mungu alinipa afya kuona kiwango matata cha Shomari Kapombe na Saidi Ndemla. Umati mkubwa wa watu pale Tabora na Morogoro pia nilijaaliwa kuuona. Namshukuru Mungu kwa hili.
Pep Guardiola ni miongoni mwa maocha bora kabisa duniani ambaye anasubiri tu kuifundisha timu ya taifa ili achukue ubingwa wa dunia, mabara na ule ubingwa wa Ulaya ili aweze kutimiza rekodi ya kuchukua kila kitu kwenye medani ya soka. Kutokana na umaridadi wa kocha huyu, leo hii nimekuletea wanandinga ambao wamepata majina makubwa chini ya kocha huyu ambaye anaheshimika sana pale Camp Nou. Kuwaona wanandinga hawa ungana nami mwanzo hadi mwisho hapa chni. Karibu sana..
SERGIO BUSQUETS
Akiwa na miaka 20, Guardiola alimuamini sana kwa kumpa majukumu ya kucheza kama Deep-lying midfielder. Baada ya kutekeleza majukumu haya, hatimaye Sergio alianza kuchezeshwa na Pep kama Defensive midfielder na hapa ndipo alipowafanya akina Yaya Toure na Seydou Keita kuikimbia Barcelona. Uwezo wake ulimfanya Alex Song arudi EPL baada ya kukosa nafasi kabisa Nou Camp. Uwezo wake wa kuusoma mchezo ulimfanya kupewa nafasi na Pep na kwa sasa amekuwa nyota mkubwa kabisa duniani. Ana akili ya kupiga pasi zenye uhakika na amejawa na nidhamu ya kukaba bila kupata kadi hatarishi.
GERALD PIQUE
Japokuwa alikaa Manchester kwa miaka 4 ila aliamua kumfuata Pep baada ya kuona hana nafasi kwenye kikosi cha Fergurson. Msimu wake wa kwanza pale Nou camp alicheza mechi 45, idadi ambayo hakuifikia kwa kipindi cha miaka 4 aliyokaa Old Trafford. Guardiola alionekana kuvutiwa na uchezaji wa Pique hasa kutokana na ukweli kuwa Gerald ni Ball playing defender na wala sio mtu wa kubutua mipira ovyo kama akina fulani wa pale London. Akiwa chini ya Guardiola, Gerald alitajwa kama miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha mwaka cha UEFA mara mbili, mwaka 2010 na 2012.
THIAGO ALCANTARA
Akiwa na miaka 19 pekee, Pep alimpa nafasi kijana huyu mwenye asili ya Brazili na Italy. Tangu mwaka 2009 Pep alimuamini mchezaji huyu na alicheza takribani mechi 45 chini ya Guardiola licha ya Xavi kuwa na kiwango bora kwa kipindi hiki. Thiago ni kiungo anayeweza kukupa vitu vingi katikati ya uwanja. Uwezo wake umemfanya Pep aende nae pale Munich. Akiwa Bayern, Thiago aliweka rekodi ya kugusa mpira mara 185 na kuweka rekodi kwenye Bundesliga. Pep ana uwezo wa kumchezesha Thiago kama Deep-lying playmaker au pia kama kiungo mshambuliaji.
PEDRO RODRIGUEZ
Akiwa Barcelona B, Pedro alipandishwa na Pep kwenye timu ya wakubwa na hapa ndipo alianza kufanya makubwa katika anga ya soka. Msimu wake wa kwanza alipewa nafasi mara 14 na kuonesha kiwango cha juu kitu ambacho baadae kilimfanya kuwa mchezaji wa kwanza kucheza kwenye mashindano 6 tofauti. Pia msimu uliofuata chini ya Pep, Pedro alifunga magoli 23 na msimu uliofuata pia aliweka kambani magoli 22. Pedro alifanya makubwa sana baada ya kuaminiwa na Pep hali iliyomfanya kuwa Super star na kumtambulisha kama winga hatari duniani.
LIONEL MESSI
Japokuwa alianza kucheza chini ya Frank Rijkaard ila Messi tunayemjua leo alitengenezwa na kuaminiwa chini ya Pep Guardiola. Pep alimpa Messi majukumu ya kucheza kama namba tisa muongo muongo, hapa Messi alifunga magoli 47 na jina lake kuanza kutajwa sana miongoni mwa wanasoka duniani. Akiwa chini ya Pep, Messi alifunga magoli 211 katika mechi 219. Magoli haya ni mengi sana hasa kutokana mfumo wa Guardiola ambao ulimfanya Messi kuwa wa mwisho kumalizia mipira ya akina Xavi na Iniesta. Uwezo wa Messi kukabwa na mchezaji zaidi ya mmoja uliwapa nafasi ya kuonekana akina Pedro na Sanchez.


0 comments:
Post a Comment