Dar es salaam. Aliyewahi
kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kada wa Chama cha
Mapinduzi (CCM), Balozi Juma Mwapachu leo ametangaza kujivua uanachama
wa chama hicho kutokana na chama kupoteza dira.
Tamko
la Balozi Mwapachu ambalo Mwananchi imethibitisha kutoka kwake linasema
kuwa kuanzia kesho kada huyo wa CCM hatakuwa tena mwanachama wa chama
hicho tawala na kuongeza kuwa bado hajaamua kujiunga na chama kingine.
‘’Kuanzia
kesho mimi si mwana CCM tena. Nitarejesha rasmi kadi yangu kupitia
ofisi ya CCM ya kata yangu Mikocheni, Dar es Salaam. Kwa sasa sijaamua
kujiunga na chama kingine. Mwenyezi Mungu anilinde,” inasema sehemu ya
tamko hilo.
Mwanasiasa
huyo ambaye amekuwa ndani ya CCM kwa miaka 48 sasa amesema kuwa katika
mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama hicho, chama kilidhihirisha
kutokuwa chama kinachoendeshwa kwa misingi ya demokrasia kwa kumuengua
waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye anapendwa na wengi ndani ya
chama.
Mwapachu amesema kuwa Lowassa na wanachama wengine wa CCM waliojitoa ni sahihi hivyo naye anaungana nao.
‘’Kujitoa
kwake uanachama wa CCM hivi karibuni ni sahihi kabisa kwasababu CCM si
chama tena cha watu. Kimetekwa, na mimi nakubaliana na msimamo wa
Lowassa na hao waliyofuata kutoka ndani ya CCM,’’ alisema Mwapachu.
Mwapachu
ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho lakini pia amewahi
kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). CHANZO: MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment