TP Mazembe walinusa harufu ya ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa klabu ya USMA Alger kwa mabao 2-1 usiku wa kuamkia Jumapili katika uwanja wa Omar Hammadi, Algiers.
Bao la ushindi la TP Mazembe lilifungwa na Mbwana Samatta kwa mkwaju wa penati dakika 11 kabla ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi Ghead Grisha kutoka Misri.
Bao hilo la saba kwa Samatta limemfanya kuwa mfungaji bora sawa na Bakri wa Al Merriekh ya Sudan.
Kiuongo mshambuliaji wa Zambia Rainford Kalaba ‘Master’ aliifungia Mazembe bao la kwanza dakika ya 28 na baadae kutolewa nje kwa kadi nyekundu kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.
Wenyeji, USM Alger walijitutumua na kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Mohamed Segur dakika ya 89.
El Orfi wa USM Alger alilambwa kadi nyekundu kipindi cha pili kufanya timu zote mbili kumaliza pambano zikiwa na wachezaji kumi.
Kwa matokeo hayo, TP Mazembe itahitaji sare ya aina yoyote ili kutawazwa mabingwa wa Afrika kwa mara ya tano.
Mazembe itakuwa na faida ya kucheza kwenye uwanja wake wa nyumbani jijini Lubumbashi kwenye pambano la marudiano siku ya Jumapili.
0 comments:
Post a Comment