Taharuki imetanda kwa wamiliki wa shule nchini baada ya kupokea waraka unaowakataza kuongeza ada kwa shule zisizo za serikali katika mwaka wa masomo unaoanza mwezi ujao.
Kwa
mujibu wa tangazo hilo lililotolewa Desemba 3, mwaka huu na Katibu Mkuu
wa wizara hiyo, Sifuni Mchome, shule zinatakiwa kutoongeza ada mwaka wa
masomo 2016 hadi zitakapopata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu.
Tangazo
hilo pia lilieleza kuwa kwa shule ambazo zimeongeza ada bila kupata
kibali cha Wizara, kamwe hazitatambuliwa kwani ni batili na kwamba
zimefutwa kwavile hazina nguvu kisheria.
Kadhalika,
tangazo hilo lilieleza kuwa ada zote kwa shule zisizo za serikali
zitabaki kama zilivyoidhishwa na kamishna ambapo waraka wa Elimu Na. 4
wa mwaka 2008 umeelekeza ada zinazotozwa shule za msingi na sekondari
pamoja na zisizo za serikali.
Ada iliyowekwa kwa shule za kutwa zisizo za serikali ni Sh. 150,000 na shule za bweni Sh. 380,000 kwa mwaka kila mwanafunzi.
Wamiliki wa Shule Waivaa Serikali
Mkuu
wa Shule ya Mtakatifu Florence ya Mikocheni, Willison Mwabwuke, alisema
wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hiyo kutoka kwa serikali.
Alisema wao hutumia gharama kubwa kuendesha shule hiyo ikiwamo kuwalipa mishahara walimu na kununua vitendea kazi.
Alisema hutoza ada Sh. 2,055,000 kwa wanafunzi wa kutwa na Sh. 2,970,000 kwa wanafunzi wa bweni.
“Tunagharamia
usafiri, chakula, ulinzi, maji na usafi pia tunawalipa walimu mishahara
mikubwa, sidhani kama serikali watakuwa wanatutendea haki,” alisema Mwabwuke.
Alisema serikali inatakiwa kuboresha huduma katika shule za umma na siyo kuzibana shule binafsi.
Aliongeza kuwa ni mapema kwa serikali kuanzisha utaratibu huo.
Naye
mmiliki wa Shule za Green Acres, Julian Bujugo, alisema suala hilo
haliwezekani kwa sababu wahusika waliopanga kiwango hicho hawakuangalia
gharama wanazozitumia shule binafsi.
Alisema shule binafsi zina magari ambayo yanatumika kuwabeba wanafunzi kutoka majumbani hadi shuleni.
Alisema
kama serikali inataka kuanzisha utaratibu huo, ni dhahiri watahamia
katika hospitali kwa kuwa nako zinamilikiwa na watu binafsi na
kuwapangia bei.
“Hili
suala sisi wamiliki wa shule binafsi tunalipinga moja kwa moja na
serikali inatakiwa kufanya utafiti kwanza kabla haijaanza kutekeleza,” alisema Bujugo.
Alisema shule za Green Acres hutoza Sh. 400,000 kwa wanafunzi wa kutwa na Sh. 550,000 kwa wanafunzi wa bweni.
Alisema endapo serikali wakiendelea kusisitiza kuwapo kwa bei hizo, Green Acres hawataweza kuendelea kutoa elimu.
Alisema
walimu katika shule zake wanalipwa kuanzia Sh. 700,000 hadi Sh. milioni
moja kwa mwalimu wa daraja la juu na Sh. 450,000 hadi Sh. 500,000 kwa
walimu wa daraja la chini.
Mkuu
wa Shule ya Sahara iliyopo Mabibo, Pili Odinga, alisema ni vyema
serikali ikatoa mchanganuo wa gharama hizo walizozielekeza kwa wamiliki
wa shule binafsi.
Alisema Shule ya Sahara inajiendesha na haipati ruzuku kutoka serikalini.
Alisema
ada ya mwanafunzi kwa shule ya msingi ni Sh. milioni moja kwa kutwa na
Sh. milioni 2.2 kwa wanafunzi wa bweni kwa mwaka na kwamba ina walimu 15
wanaolipwa mishahara.
Kwa
upande wake, mmiliki wa shule ya sekondari na Chuo cha Ufundi Mong’are,
Joseph Mong’are alisema suala hilo haliwezekani na litakuwa gumu
kutekelezwa.
Alisema kwa mfano, darasa moja lenye wanafunzi 40 kila mwanafunzi akilipa Sh. 150,000, itakuwa Sh. milioni sita kwa mwaka.
Alisema
Sh. milioni sita ikigawanywa kwa miezi 12 ya kuwapa mishahara walimu
itapatikana Sh. 500,000, ambayo haitaajiri walimu wala kujenga majengo,
vitendea kazi, maktaba, maabara, vitabu havitanunuliwa.
Serikali Yakanusha
Ofisa
Habari wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Oliva Kato, alisema
serikali haijatoa waraka wa ada elekezi yoyote kwa shule zisizo za
serikali kama ilivyoripotiwa, badala yake imetoa tangazo la katazo la
kuongeza ada kwa mwaka masomo 2016 kwa shule hizo.
Alisema
hadi sasa hakuna waraka uliotolewa na serikali ukizitaka shule hizo
kutoza ada elekezi, badala yake limetoka tangazo linalozitaka kutotoza
ada mpya bila kuwasiliana na Kamishna wa Elimu.
“Hakuna
ada elekezi yoyote iliyotolewa na serikali kwa mwaka wa masomo 2016
limetolewa tangazo la kuzikataza shule kutotoza ada mpya mpaka zipate
maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu,” alisisitiza Kato.
Alisema
wamiliki wa shule hizo wamepewa wiki mbili kuwasilisha ada walizotoza
mwaka huu na vibali vya kutoza pamoja na zitakazotozwa mwaka ujao wa
masomo kwa ajili ya kupatiwa vibali na Kamishna.
Alisema
kwa sasa bado wataalam wa wizara wanafanya utafiti za kuandaa mfumo wa
kielektroniki wa kutambua gharama za kumsomesha mwanafunzi katika elimu
ya awali, msingi na sekondari.
0 comments:
Post a Comment