KAMPUNI
ya Simu nchini Tanzania (TTCL) leo imezinduwa mtandao unaotumia
teknolojia ya 4G LTE unaoanza kutoa huduma jijini Dar es Salaam. Mtandao
huo wenye teknolojia mpya na ya kisasa wenye kasi kubwa utatoa huduma
katika maeneo 11 ambayo ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Mwalimu J.K.
Nyerere, Pugu Road, Posta Mpya, Upanga, Kinondoni, Ubungo, Oysterbay,
Mwenge, Mbezi Tangibovu, Mbezi Exchange, Kunduchi Salasala, na Wazi
Tegeta.
Akizungumza
leo jijini Dar es Salaam wakati akizinduwa rasmi teknolojia hiyo, Ofisa
Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura alisema licha ya kuzinduwa
huduma hiyo katika maeneo 11 kwa sasa mafundi wa kampuni hiyo wapo
kazini wakiendelea na awamu ya pili ya kufunga mitambo ili huduma hiyo
itolewe pia katika maeneo mengine 14 ya jiji la Dar es Salaam.
Aliyataja
maeneo mengine ambayo mitambo inaendelea kufungwa kwa sasa kuwa ni
pamoja na Kigamboni, Masaki, Temeke, Kimara, Jangwani, Kariakoo, Chuo
Kikuu, Kurasini, Mbezi Chini Gongo la Mboto, Tabata, Kibamba, Kongowe na
Bunju.
"...Awamu
ya pili ya mradi huu itakuwa imekamilisha maeneo yaliyobaki ya mkoa wa
Dar es Salaam na pia kupeleka mawasiliano hayo katika mikoa mingine
ikiwa ni pamoja na Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na kwingineko," alisema
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kazaura.
Alisema
uzinduzi wa teknolojia ya 4G LTE unakuwa umekamilisha nia ya siku
nyingi ya kampuni ya TTCL ya kuwahudumia wateja katika nyanja zote za
mawasiliano (Fixed-mobile convergence) kwa kutumia teknolojia ya simu za
mezani na simu za mkononi.
Akifafanua
zaidi Dk. Kazaura alisema uzinduzi wa teknolojia ya 4G LTE utakuwa na
mchango mkubwa katika kukuza na kuongeza kasi ya shughuli za maendeleo
ya kijamii na kiuchumi, kuchangia katika kukuza teknolojia ya habari na
mawasiliano na pia kuongeza uzalishaji kwenye sekta mbalimbali za
maendeleo.
Aidha
aliongeza kuwa TTCL inaamini mtandao wa 4G LTE utafungua fursa pekee
katika kukuza sekta ya elimu nchini kwa njia ya mtandao (E education).
Na pia ubora wa huduma hiyo ya intaneti utatoa fursa kwa wanafunzi,
wakufunzi, wataalam, wanazuoni na walimu kutumia teknolojia katika
kujifunza mambo mbalimbali ya kitaaluma na nje ya taaluma.
Kwa
upande wake Ofisa Mkuu wa Mauzo na Masoko wa Kampuni ya TTCL, Peter
Ngota akifafanua zaidi kwa wanahabari alisema mtandao wa 4G LTE
utaongeza fursa katika sekta ya afya ambapo hospitali, vituo vya afya,
vyuo vya afya na wadau mbalimbali wataweza kutumia mtandao huo katika
kuongeza ufanisi wa kutoa huduma bora za afya kwa wananchi tena kwa
haraka zaidi.
Alisema
mtandao huo pia utazinufaisha sekta nyingine za kiuchumi kama vile
sekta ya biashara, viwanda, kilimo na nyinginezo. "...Wafanyabiashara na
wazalishaji wa bidhaa wanahitaji mawasiliano ya uhakika katika shughuli
zao. Mtandao huu wa 4G LTE utakuwa mkombozi wao na utaleta mageuzi
katika kuongeza uzalishaji, kupanua wigo wa masoko ya bidhaa kwa
wakulima, masoko kwa wajasiliamali, masoko kwa makampuni ndani na nje ya
mipaka ya Tanzania," alisema Peter Ngota.
Hata
hivyo, Ngota aliongeza kuwa uzinduzi huo unaenda sambamba na uboreshaji
vifurushi rafiki vya intaneti kwa wananchi hivyo kuwaomba wananchi
kuiunga mkono kampuni ya kizalendo ya TTCL katika kuboresha huduma za
mawasiliano nchini.
|
0 comments:
Post a Comment