Na Hemed Kivuyo
Nilisoma na mtu mmoja anaitwa Bakari kule Arusha, huyo jamaa alikuwa mjeuri sana na msumbufu darasani. Mara nyingi tunapokuwa mstarini yeye hayupo hujificha chooni. Tunapoingia darasani yeye huingia kwa dirishani au huingia kwa kujificha akiwa mchafu asiyeweza kufua hata shati lake.
Mara kadhaa alikuwa haandiki na akiulizwa hujibu kwakukaa kimya mpaka mwalimu hutumia fimbo pamoja nahayo huwa ‘sugu’ tu.
Panapotokea kelele darasani mwalimu anapoingia tu kuanza kumuangalia Bakari alipokaa na kisha humwita mbele na kumuadhibu hata kama Bakari hakuwa mleta fujo kwa wakati huo.
Siku moja tulikuwa mstarini na Bakari alikuwepo, siku hiyo hata mimi nilishangaa kwanini Bakari yupo mstarini tena alikuwa kafua nguo zake na zilionekana kupigwa pasi alikuwa nadhifu ‘barobaro’.
Viatu vilionekana kung’aa barabara huku akinukia manukato, hakika alikuwa Bakari halisi tofauti na siku zote nilizomjua.
Wakati tumeshakaguliwa na kuingia darasani, Bakari alikuwa wa mwisho kuingia darasani, mwalimu mmoja hivi simkumbuki jina akamuona Bakari akiwa wa mwisho. Mwalimu yule haraka alimwamuru Bakari ashike chini kisha akamnyuka ‘viboko’ vitatu vya nguvu kisha akaanza kumtajia makosa yake.
Kwanza alimwambia amechelewa na hakukaa mstarini na tatu alikuwa mchafu jambo ambalo kwa siku hiyo halikuwa kweli. Bakari alikuwa msafi na aliwahi ila alikuwa wa mwisho katika mstari na alipolala chini kuchapwa mwalimu hakuona mavazi yake kuwa ni masafi.
Baada ya kipigo kile mwalimu alipewa taarifa kuwa makosa yote aliyomsomea Bakari hayakuwa sahihi alimuomba radhi ingawa Bakari alishapata maumivu.
Ndugu zangu hiyo ni hadithi fupi na yakweli ambayo ninaifananisha na haya yanayotokea kwa sasa baina ya msemaji wa Yanga Jerry Muro na msemaji wa Simba Haji Manara.
Binafsi nilikuwepo siku ile Muro anaongea nasi (waandishi wa habari) aliongea mengi ya klabu hiyo lakini pia alimshukia Haji Manara yeye mwenyewe akiita ‘kutumbua majipu’.
Kumekuwepo na maneno kuwa Muro ametoa maneno yakibaguzi dhidi ya Hadji Manara lakini maneno yenyewe hayatajwi ni yapi na ambayo mimi sikuyasikia siku hiyo.
Nilimsikia Jerry akisema Haji amemtaja kuwa yeye ni mtu kutoka Kilimanjaro na hajui soka, pia akaseka Yanga inapendelewa na Shirikisho la Soka nchini TFF, hayo ni kwa mujibu wa Jerry.
Jery akasema kwakuwa Haji alimtaja moja kwa moja katika chombo cha Habari kuwa yeye hajui soka kwakuwa ametoka Kilimanjaro na yeye anamtaja na kumjibu kwa jina lake kwakuwa mwiba hutokea pale ulipoingilia.
Kwa mujibu wa Jery, Manara alimtaja kwa jina kuwa ametoka huko wasipojua soka.
Kama tukiamua kuzama katika Kiswahili na kupata maana halisi ya ubaguzi, basi Haji Manara na Jerry Muro wamebaguana wenyewe. Ukisikiliza kwa makini maneno ya Muro utaona ametamka maneno yale kiufundi mkubwa, ametamka kwa mfumo wa kujibu.
Naamini kabisa kama watapelekwa katika mahakama zetu zakiraia mfano Kisutu hakutokuwa na ushahidi wa moja kwa moja wa kumkuta Jerry Muro na hatia.
Nasema hivyo kwasababu Mahakama huhitaji ushahidi wa moja kwa moja na usiyokuwa na shaka hata kidogo.
Jerry ametoa shutuma hizo kwa ufundi mkubwa ambao haumuingizi hatiani labda kwa kamati ‘zakisiasa’ lakini kisheria hawezi kukutwa na hatia.
Mfano mimi nimelaumiwa na rafiki yangu Issa na akanitupia shutuma kali na maneno yasovikwa nguo, nami nikamjibu na katika kumjibu nikamjibu kama ifuatavyo.
“Mimi siwezi kutishwa na mtu hohehahe kama Issa, eti mtu anasema mimi sijasoma basi aende kushtaki, sibabaishwi na paka anayehitaji hisani kupata mlo”, mwisho.
Tukienda Mahakamani Issa kanishtaki mimi nimemuita yeye ni ‘Paka’ hawezi kushinda hiyo kesi.
Hata kama kuna ushahidi wa sauti na picha nikitamka maneno hayo kwasababu nyingi zakisheria Issa hawezi kushinda kesi.
Hilo ni suala moja, lakini suala la pili kama kweli Haji Manara alianza kutoa maneno hayo yakibaguzi dhidi ya Muro hata kama hakusema katika chombo cha habari ni dhambi katika soka. Ukiua mtu haijalishi ulimuua wapi msingi ni kwamba umeua.
Miaka ile ya 1890 na kuendelea alikuwepo Mwanadada aliyeitwa Mtumwa, lakini jina lake halisi ni Siti binti Saady. Alililewa katika mazingira ya wakati huo mwanamke hapewi nafasi ya kwanza na kulijaa ubaguzi wa hali ya juu.
Alibaguliwa na kulikuwa na ubaguzi wa rangi kutoka kwa jamii ya waarabu. Kulitokea uhasama baina ya waarabu na weusi. Siti alikuwa mweusi. Siti alikuwa mwimbaji mzuri na umma ulimpenda, alikuwa na sauti muruwa na kuwavuta wengi.
Katika moja ya majibizano hayo, wabaya wa Siti wakamwambia Siti..‘Siti kawa mtu lini kaja mjini na kaniki chini, kama si sauti angekula nini.
Siti akawajibu kupitia wimbo wake akisema “hasara ya mtu kukosa akili”.
Kimsingi ukiangalia vyema na kusikiliza vyema majibu ya Siti huwezi kumuhukumu moja kwa moja kuwa aliwatusi wabaya wake.
Muro kusema Haji akahangike na yake yanayomshinda siyo ubaguzi, kusema hana gari siyo ubaguzi, kusema anaishi kwao siyo ubaguzi na kama kweli alisema hivyo.
Kuna ukweli na kuna urongo. Kama ni kweli basini uhalisia hakuna unafiki hapo. Yawezekana ni maneno ya kuudhi lakini siyo yakibaguzi na hapa najadili maneno ya kibaguzi kwakuwa ndiyo Jerry analaumiwa nayo lakini naona ni maneno ya kuudhi siyo kibaguzi.
Majibu hayo makali pia hutegemea mtoa kauli wa awali aliyatoa kwa ukali kiasi gani.
Jery alitumia lugha za kuudhi wakati akijibu mapigo kwa hasimu wake kisoka ingawa hawapaswi kuwa mahasimu kama zilivyo timu zao.
Binafsi siungi mkono mameno ‘machafu’ na yenye ubaguzi ndani yake miongoni mwa jamii lakini lazima tuangalie haki ilipo kwakuwa haki huwa inanyooka.Haji Manara naye ni mkosefu ila ni mkosefu anayelindwa na wengi na hapo ndipo anapoficha makucha yake.
Shirikisho la kandanda limetajwa na Haji Manara kuwa linaipendelea Yanga, shirikisho halijakanusha wala halijamchukulia hatua Hadji Manara.
Bali shirikisho limesherehesha kauli ya Manara kwakudhamiria kumchukulia hatua msemaji wa timu wanayoipendelea, kwa mujibu wa Haji.
Kama Jerry muro atakuwa na tuhuma za kutoa lugha zakibaguzi basi nitashangaa sana kama tuhuma hizo hatokutwa nazo Haji Manara.
Haji Manara mwenye sifa ya upole wa Twiga lakini mwenye maneno makali ambayo yaliwahi kuwajeruhi hata waandishi wa Habari kwa kuwaita ni wenye ‘kuingiza ndimi zao puani’.
Tutoe hukumu za haki ingawa mara nyingi chini ya Juha hamna haki, tusimuhukumu Jery kama Bakari aliyezoeleka kuvunja kanuni za shule lakini siyo alipopewa adhabu hakuvunja kanuni hizo.
Wahukumiwe kwa kutoa lugha za kuudhi kwakuwa hata Haji hayupo salama.
0752 250157 au 0655 250157
0 comments:
Post a Comment