MOROGORO: Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni! Kijana Said Ally
Mwinyimvua anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro akidaiwa
kumuua kwa kumcharanga mapanga mama yake mzazi, Sikuzani Said (70), kisa
kikidaiwa kuwa ni kunyimwa wali (ubwabwa) na kupewa mdogo wake, Abass
ambaye ni mziwanda, Uwazi linakupasha.
Tukio hilo lililoacha majonzi, lilijiri wiki iliyopita nyumbani kwa
familia hiyo, Kijiji cha Kungwe, Kata ya Tomondo, Wilaya ya Morogoro
Vijijini.
Uwazi lilifika eneo la tukio na kuwakuta viongozi wa kijiji hicho kwa
kushirikiana na mgambo wakimpeleka mtuhumiwa huyo kwenye Kituo cha
Polisi Mkuyuni ambako anashikiliwa hadi sasa.
Kwa upande wake, mume wa marehemu, Ally Mwinyimvua Dugulu ‘Mzee
Kisauti’ (80), alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alikuwa na haya ya
kusema:
”Mimi na mke wangu tumejaliwa kuzaa watoto tisa, wa kike wanne na wa
kiume watano. Wakike wote wameolewa huko mijini na wa kiume watatu
wameoa pia hukohuko mjini. Hapa nyumbani tumebaki na watoto wawili, Said
na Abass ambaye ndiye mtoto wa mwisho.
“Kwa muda mrefu Said amekuwa akitulalamikia sisi wazazi kwamba
tunampenda zaidi mdogo wake kuliko yeye, jambo ambalo si la kweli.
“Hawa watoto waliwekewa zamu ya kupika. Siku ya tukio ilikuwa zamu ya
Said, alipika ubwabwa, akaubeba wakaenda shamba. Ubwabwa mwingine
waliubakisha kwa ajili ya jioni. Mimi kutokana na kazi zangu nilibaki
hapa nyumbani, wakaniwekea ubwabwa wangu.
Saa 11 jioni, Abass na mama yake walirudi huku wakimuacha Said shambani.
“Saa moja usiku, Said alirudi, akaenda kwenye kabati na kukuta ubwabwa umekwisha. Alimuuliza mama yake, akamjibu kwamba mdogo wake amekula wote hivyo yeye ale kiporo cha jana, jambo ambalo lilimkera sana. Alichukua panga alilotoka nalo shamba na kuanza kumcharanga mama yake mwili mzima.
“Mimi kutokana na uzee, nilishindwa kumsaidia mke wangu mpaka anakata
roho alikuwa akipiga kelele,” alisema Mzee Kisauti.Kwa upande wake,
Abass alipohojiwa, alisema alijaribu kumsaidia mama yake bila mafanikio
kwani kaka yake alitishia kumuua na yeye.
“lshu kama ni ubwabwa angeniambia ningemuachia ale kuliko kumuua
mama. Nilijitahidi sana kumtetea mama lakini kaka alitaka kunikata na
panga hivyo nilikwenda kuita majirani ambapo walipofika tulikuta mama
ameshafariki dunia huku kaka akikimbia,” alisema Abass.
Alipoulizwa kama kaka yake anakunywa pombe au kuvuta bangi, Abass
alisema hatumii vitu hivyo.Alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, diwani wa
kata hiyo, Hamis lssa Msangale alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na
kusema:
“Mtuhumiwa baada ya kumuua mama yake kwa kumcharanga mapanga zaidi ya
20 mwilini, usiku huohuo alitoweka nyumbani na kwenda kujificha huku
wananchi wenye hasira wakimsaka kijiji kizima kwa lengo la kulipa
kisasi.
“Kwa bahati nzuri alfajiri, raia wema walitujulisha kwamba Said
amepitiwa na usingizi amelala chini ya mwembe. Nilimjulisha mwenyekiti
wa kijiji, tukachukua mgambo tukaenda kumkamata na kupita naye vichakani
mpaka Kituo cha Polisi Mkuyuni tukiwakwepa wananchi wenye hasira,”
alisema kiongozi huyo.
0 comments:
Post a Comment