Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia
Kamati yake ya Nidhamu hatimaye imemaliza kesi iliyochukua takribani
wiki tatu kusaka maamuzi ya madai ya mechi za ligi daraja la kwanza
baada ya , kuzishusha daraja timu zote,
Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Kanembwa na JKT Oljoro baada ya kuzikuta
na hatia ya kupanga matokeo katika mechi za mwisho za Ligi Daraja la
Kwanza Bara.
Maamuzi hayo yaliyotangazwa leo na makamu
mwenyekiti wa kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa yamezishusha JKT
Kanembwa iliyoshushwa hadi Ligi ya Mkoa, wakati Geita, Polisi Tabora na
JKT Oljoro zimeshushwa hadi Daraja la Pili.
Msemwa amesema aliyekuwa kipa wa Simba ambaye anaitumikia kwa
mkopo Geita, Dennis Richard amefungiwa miaka 10 kujihusisha na soka
pamoja na faini ya Sh. Milioni 10 baada ya kushikwa na hatia kuwa katika
mpango wa upangaji matokeo adhabu ambayo pia imemkumba kipa wa JKT
Kanembwa Mohamed Mohamed.
Naye kocha msaidizi wa Geita Choki Abeid
ameshushiwa rungu la adhabu kali kwa kufungiwa maisha baada ya kushikwa
na hatia na kamati hiyo.
“Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu
mkoa wa Geita (GEREFA), Salum Kurunge, Mwenyekiti wa klabu ya Geita
Gold, Cosntantine Moladi na Katibu wa klabu ya JKT Kanembwa Basil Matei
wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu baada ya kutokutwa na hatia katika
shauri hilo,”alisema Msemwa.
Aidha Msemwa amesema Wengine waliofungiwa
miaka 10 na faini ya Sh. Milioni 10 ni Refa na refa wa akiba wa mechi
kati ya Polisi na Oljoro ambazo nazo zilishikwa na hatia mbalimbali
kutokana na maelezo waliyoyatoa kwa kamati yake.
Refa wa mchezo kati ya Kanembwa na Geita
Gold, naye amefungiwa maisha sawa na Kamisaa wa mchezo huo na Kocha
Msaidizi wa Geita, Mwenyekiti Yussuf Kitumbo na Katibu, Alex Kataya wa
Chama cha Soka Tabora (TAREFA), Kocha msaidizi Polisi Tabora na
Mwenyekiti Oljoro.
Kwa upande wa Katibu wa klabu ya Polisi
Tabora, Alex Kataya, Katibu wa klabu ya JKT Oljoro, Hussein Nalinja,
mtunza vifaa wa klabu ya Polisi Tabora, Boniface Komba, na Meneja wa
timu ya Polisi Tabora, Mrisho Seleman, wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu ya baada ya kutokutwa na hatia.
Hata hivyo Kamati hiyo imefungua milango
kwa wahukumiwa kukata rufaa endapo watabaini maamuzi hayo hayakuwatendea
haki ambapo sasa kwa mujibu wa matokeo hayo ni wazi kwa mujibu wa
kanuni Mbao FC ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya nne ndiyo inayoweza
kuchukua nafasi ya kupanda Ligi Kuu.
0 comments:
Post a Comment