MHASIBU wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Imani Abduli Nyamangaro (44) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida akikabiliwa na tuhuma za mashitaka 57 ya wizi wa mishahara hewa yenye jumla ya shilingi 29,418,642/=.
Mapema Mwendesha Mashtaka,Wakili wa serikali, Michael Lucas Ng’hoboko alidai kwamba kati ya april , 29 mwaka 2013 na machi, 27 mwaka 2014 mshitakiwa Nyamangaro ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Utemini, mjini Singida kwa makusudi aliiba mishahara hewa ya zaidi ya shilingi milioni 29.4 huku akijua wazi kwamba kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Joyce Minde, Ng’hoboko alidai kwamba mshitakiwa huyo alikuwa akijipatia mishahara hiyo ambayo wahusika waliisha staahafu kazi kwa kipindi cha muda mrefu, kupitia akaunti yake no. 50802503513 iliyopo katika Benki ya NMB Tawi la Singida.
Hata hivyo mshitakiwa Nyamangaro alikana kutenda makosa hayo yote 57 na hivyo kesi yake imeahirishwa hadi apr, 27 mwaka huu itakapotajwa tena.
Hakimu wa Mahakama hiyo,Minde alisema dhamana ya mshitakiwa ipo wazi na kwamba atapaswa kutoa fedha taslimu shilingi 14,709,321/= Mahakamani au awe na mali isiyohamishika yenye thamani inayolingana na kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo hadi Mwandishi wa Habari hizi anaondoka katika Mahakama hiyo,mshitakiwa alikuwa bado hajatekeleza masharti ya dhamana hiyo.
0 comments:
Post a Comment