Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora kuwakamata viongozi wanne wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU) pamoja na kufunga ofisi za chama hicho kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu.
Pia Waziri Mkuu amevunja Bodi ya WETCU pamoja na Bodi ya Tumbaku Tanzania - TTB kwa sababu ya kushindwa kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo jioni katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Isike Mwanakiyungi mkoani Tabora, ambapo amesema Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa TTB, Bw. Vita Kawawa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo Bw. Wilfred Mushi.
Viongozi wa WETCU ambao Waziri Mkuu ameagiza wakamatwe ni Mwenyekiti Bw. Mkandara Mkandara, Makamu Mwenyekiti Bw. Msafiri Kassim, Mkaguzi wa Ndani na Mhasibu Mkuu. Pia amewasimamisha kazi watumishi wa kitengo cha uhasibu wa chama hicho hadi uchunguzi utakapokamilika.
“Kuanzia sasa watumishi wote wa kitengo cha uhasibu pamoja menejimenti nimewasimamisha kazi pamoja na Mrajisi wa mkoa wa Tabora Deogratius Rugangila. Kamanda hakikisha ofisi hazifunguliwi kuanzia sasa hadi hapo timu ya ukaguzi itakapokamilisha kazi yake,”amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema kwa muda mrefu wakulima wameteseka na zao hilo kukosa tija kwa sababu ya usimamizi mbovu wa viongozi wa ushirika na Bodi ya Tumbaku Tanzania jambo ambalo Serikali haiwezi kulivumilia.
Amesema “Hatuwezi kuwa na ushirika ambao hauwasaidii wanachama. WETCU walipokea sh. bilioni 15 ambazo walizikatia risiti na hazijaonekana. Pia waliwalipa wazabuni sh, bilioni 10 ambazo hawajazikatia risiti,”.
“Wakati wanachama ambao ni wakulima wakiendelea kutesema WETCU walinunua gari la sh. milioni 269 kinyume na maelekezo ya Mkutano Mkuu wa wadau ambao ulipitisha zitumike Shilingi milioni 40 tu,” amesema.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa chama hicho kimesababisha kupungua kwa uzalishaji kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwa na menejimemti mbovu jambo ambalo limechangia wakulima wa tumbaku kukosa tija.
Amesema WETCU kimekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha ambapo alitolea mfano suala la ukarabati wa ofisi tatu ikiwemo ya makao makuu ambayo ilipangwa ikarabatiwe kwa sh. milioni 33 wakatumia sh. milioni 170 na ofisi za Tabora na Urambo zilipangiwa sh. milioni tano kila moja na hazikukarabatiwa.
Pia Waziri Mkuu amepiga marufuku ununuzi wa mbolea kutoka nje ya nchi wakati ikiwa inazalishwa hapa nchini.
Aidha, alimepiga marufuku matumizi ya kwa dola katika sekta ya tumbaku na badala yake zitumike fedha ya Kitanzania kwa sababu kitendo hicho kimekuwa kiwanyonya wakulima.
0 comments:
Post a Comment