- Pesa iliyopigwa na wajanja NSSF ni mara tatu ya pesa iliyopigwa na wajanja wa ESCROW!
- Katika miradi yote inayosimamiwa na NSSF ya Arumeru na Kigamboni serikali imeingia hasara ya Tshs Trillioni 1.3
- Mradi wa Kigamboni wasimama, kuna ufisadi wa zaidi ya Tshs Billioni 179
- Mikataba yasainiwa kimagumashi bila kufuata sheria, wajenzi ni Waturuki.
- Ardhi ya Kigamboni ilinunuliwa kwa Tshs millioni 800 kwa ekari wakati ilitakiwa inunuliwe kwa Tshs Millioni 4.5 kwa ekari.
- Arumeru ardhi ilinunuliwa kwa Tsh Billioni 1.8 kwa ekari wakati thamani ya ekari moja ni Tshs laki 5 mpaka Millioni 1.
- Taratibu za ununuzi wa ardhi zilifanyika kimya kimya bila kumshirikisha mwanasheria wa serikali.
Mradi
mkubwa wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam uitwao
Dege Eco Village, ulioanzishwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii
(NSSF) umesimama huku ikiripotiwa kuwapo kwa ufisadi wa zaidi ya Sh179
bilioni katika mradi huo.
Mchoro
wa mradi huo ulioanzishwa mwaka 2014 kwa gharama ya Dola za Marekani
653 milioni (Sh1.3 trilioni) unaonyesha utakapokamilika utachangia
kubadili sura ya jiji la Dar es Salaam kwani kutakuwa na nyumba za
kifahari, majengo ya hoteli, maduka makubwa, eneo la wazi la mapumziko,
baa, shule, hospitali, kumbi za mikutano, nyumba za ibada na migahawa.
Hata
hivyo, mradi huo unaosimamiwa na kampuni ya Hifadhi Builders Limited
iliyoanzishwa na Bodi ya NSSF kwa ushirikiano na kampuni ya Azimio
Housing Estate Limited (Ahel), huku wajenzi wakiwa kampuni ya M/s
Mutluhan Construction Industry Company Limited kutoka Uturuki, huenda
usikamilike kwa muda uliopangwa kwani umesimama tangu Januari, ingawa
unadaiwa utaanza tena mwezi huu.
Ofisa
mmoja mwandamizi wa Serikali ameliambia gazeti la Mwananchi kwamba
ujenzi wa nyumba za Dege Eco Village ni miongoni mwa miradi ya kisasa
ambayo NSSF imekaguliwa na kubainika kufisadi fedha baada ya kuingia
mikataba bila kufuata taratibu, kanuni wala sheria za nchi.
Kwa
mujibu wa ofisa huyo, ripoti ya ukaguzi iliyoishia Juni 2015,
uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
akishirikiana na taasisi ya kimataifa ya ukaguzi ya Ernst and Young
imeanika ufisadi mkubwa unaotishia usalama wa fedha za wanachama wa
shirika hilo.
Mtoa
habari huyo amesema mradi wa nyumba za kisasa wa Kigamboni unaojengwa
katika ekari 300, unakabiliwa na kashfa baada ya kubainika kuwa NSSF
imenunua ekari hizo kutoka kwa mbia mwenzake Azimio Housing Estate
Limited kwa zaidi ya Sh800 milioni kwa ekari, wakati shirika hilo
linamiliki viwanja vingine maeneo hayo vyenye thamani ya Sh4.5 milioni
kwa ekari.
“Ukipata
ripoti hiyo ya ukaguzi utaweza kuona ilivyochambua miradi mbalimbali ya
ujenzi jijini Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Pwani na Mtwara. Kwa mfano
mradi wa Arumeru mkoani Arusha, NSSF imenunua viwanja kutoka Azimio kwa
Sh1.8 bilioni kwa kila ekari,” alieleza ofisa huyo.
Uchunguzi
unaonyesha kwamba Bodi ya NSSF na Azimio walitiliana saini Novemba 15,
2013, kuhusu uendeshaji wa miradi mbalimbali. Azimio walijieleza kuwa
wanamiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 20,000 Kigamboni, ekari 655.3
Arumeru, ekari 7,832.7 Pwani, ekari 200 Mwanza, ekari 5,723.6 Mtwara, na
kwamba maeneo hayo yanafaa kwa ujenzi wa miji ya kisasa.
Taratibu
ziliitaka NSSF kujiridhisha kuhusu uwepo wa ardhi hiyo, uhalali wa
kisheria wa Azimio kumiliki eneo hilo pamoja na thamani halisi ya ardhi
hiyo kutoka mamlaka zinazohusika. NSSF hawakufanya hivyo na wala
hawakumshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Napenda
kukuthibitishia kwamba NSSF waliridhia bila ya kujiridhisha kuhusu
uwapo wa ardhi hiyo bali walitiliana saini miradi ya pamoja kujenga
nyumba Kigamboni na Arumeru bila kujiridhisha,” alisema ofisa huyo.
Mradi
wa Kigamboni una thamani ya Dola za Marekani 653,436,675 (Sh1.3
trilioni), na mradi wa Arumeru thamani yake ni Dola 3,340,589,543 hadi
utakapokamilika.
Tatizo
jingine kubwa ni kuhusu umiliki wa mradi. Uchunguzi unaonyesha mkataba
wa mradi huo uliitaka Azimio kuchangia asilimia 55 zikiwamo ekari 300
ambazo ni sawa na asilimia 20 ya mradi, huku NSSF ikichangia asilimia
45. Uchambuzi unaonyesha Azimio imetoa ekari 300 za Kigamboni kwa Dola
108,906,113, na ekari 655.3 za Arumeru kwa Dola 556,764,924.
Kwa hiyo kwa miradi miwili hiyo, NSSF ‘imenunua’ ardhi yenye thamani ya Dola 665,671,037 (Sh1.33 trilioni) kutoka Azimio.
Uchunguzi
unaonyesha kuwa Serikali imekasirishwa na hatua ya taasisi hiyo ya umma
‘kununua’ ekari moja ya ardhi kwa zaidi ya Sh800 milioni huko
Kigamboni, wakati bei halisi ya ardhi iliyotangazwa na Halmashauri ya
Manispaa ya Temeke mwaka 2012 wakati ikiuza viwanja vyake ilikuwa Sh8,
000 kwa mita za mraba, kwa hiyo ekari moja ilikuwa Sh39 milioni.
Vilevile,
NSSF yenyewe ilikuwa inamiliki ekari 267 Kigamboni ilizonunua kutoka
kampuni ya Georgia Homes (T) Ltd kila moja kwa Sh4.5 milioni, hivyo
hatua ya shirika hilo ‘kununua’ ekari moja kwa Sh800 milioni kutoka
Azimio haikubaliki.
Hata
mradi wa Arumeru, NSSF pia imebainika kufuja fedha kutokana na kukubali
kununua ekari moja kwa Sh1.8 bilioni, kinyume na thamani halisi ya
viwanja kwenye eneo ambalo lipo kilometa 30 kutoka Jiji la Arusha.
Uchunguzi umebaini wenyeji wa eneo hilo wanauza ekari moja kwa bei kati
ya Sh500, 000 na Sh1 milioni.
Hatua
ya NSSF ‘kununua’ ekari 300 Kigamboni kila moja kwa Sh800 milioni
imesababisha hasara ya Sh179 bilioni na ekari 655.3 Arumeru kununuliwa
kila moja kwa Sh1.8 bilioni imeingiza hasara ya Sh1.165 trilioni. Kwa
hiyo, miradi miwili hiyo imeingiza hasara ya Sh1.3 trilioni.
“Tusubiri,
lakini nina uhakika watu ambao kwa uzembe, walilishauri shirika kuingia
kwenye matatizo haya na kuhatarisha fedha za wanachama lazima
watawajibishwa ili kuepusha matatizo mengine yajayo kwa fedha za
wanachama wa mfuko,” alisema ofisa huyo.
Ofisa
huyo alisema kwamba hadi ukaguzi ulipofanyika shughuli zote hata
manunuzi ya vitu muhimu kwa ajili ya mkandarasi zilikuwa zinafanywa na
NSSF pamoja na mawasiliano na wasambazaji wa huduma. Hadi wakati wa
ukaguzi, NSSF ilikuwa imeingiza kwenye mradi Sh205.141 bilioni na
hazikuwapo nyaraka zilizoonyesha mchango wa Azimio mbali ya ardhi.
Kauli ya NSSF
Mwananchi
lilifanya juhudi kupata ufafanuzi kutoka NSSF kwa zaidi ya mwezi moja
lakini majibu hayakuridhisha. Kwanza liliambiwa shirika hilo halikuwa na
Mkurugenzi Mkuu tangu Februari 15 baada ya Dk Dau kuteuliwa kuwa
balozi.
Alipofuatwa
Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Miradi wa NSSF, Yacoub Kidula
alitaka apelekewe maswali ili ajibu kwa maandishi. Alipopelekewa maswali
kwa maandishi alitaka yaandikwe kwenye karatasi yenye jina la kampuni
na namba ya kumbukumbu. Baada ya kukamilisha takwa hilo, Kidula
aliipeleka barua hiyo kwa Mhandisi Julius Nyamhokya ambaye ni Mkurugenzi
wa Hifadhi Builders.
Baada
ya wiki kadhaa za kufuatilia majibu, baadaye barua ilipelekwa kwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, Eunice Chiume ambaye alisema hawezi kuijibu
kwa kuwa bado ofisi hiyo haikuwa na mkurugenzi mkuu.
“Endeleeni
kuwa wavumilivu kwa sababu sisi hatuwezi kuzungumza chochote bila kuwa
na mkurugenzi mkuu. Tukimpata atajibu kwa sababu taratibu za ofisi zetu
ni kuwa mkurugenzi mkuu ndiye mwenye majibu ya kila kitu,” alisema
Chiume.
Rais
John Magufuli alipomteua, Profesa Godius Kahyarara kuwa Mkurugenzi Mkuu
wa NSSF, bado majibu hayakutolewa. Chiume alisema Profesa Kahyarara
bado anajifunza mazingira ya shirika.
Mkurugenzi
wa Mradi wa Kampuni ya Azimio, Vital Dege alisema mradi unaendelea na
mpaka sasa nyumba 300 tayari zimekamilika. “Mradi haujasimama, bado
unaendelea na sasa tupo kwenye hatua za mwisho,” alisema Dege.
Lakini
Mwananchi lilipotembelea eneo la mradi huo hivi karibuni, lilishuhudia
shughuli zikiwa zimesimama; walikuwapo wafanyakazi wachache, wengi wao
walinzi kutoka kampuni ya Usalama Corps na wajenzi kadhaa wa kampuni ya
Uturuki ya M/s Mutluhan. Vibarua wote, mafundi na wataalamu mbalimbali
hawakuwapo.
Walinzi
wawili walionekana kwenye vibanda vya juu wakilinda majengo yaliyobaki
kama magofu. Pia, walionekana walinzi wengine wanne ambapo wawili
walikuwa kwenye lango kuu la kuingilia eneo lenye ofisi, mashine za
kutengenezea nondo na kokoto huku wengine wawili wakiwa kwenye lango la
kuingilia kwenye mradi.
“Ujenzi
umesimama, kama ungekuwa unafanya kazi, nisingeweza hata kuzungumza na
wewe, ningekuwa na kazi kubwa ya kupekua watu na kukagua magari
yanayotoka nje na kuruhusu yanayoingia. Hapa pote pangekuwa vurugu tupu,
hawa wanaingia hawa wanatoka. Kule (anaonyesha kwa kidole) kungekuwa na
kelele za mashine za kokoto na nondo,” alisema mmoja wa walinzi wawili
katika lango kuu la kuingia kwenye eneo la ofisi.
“Tumebaki walinzi tu na wasimamizi wachache. Wapo wajenzi wachache Waturuki, naona nao wanasubiri kuondoka.”
Ofisa
masoko wa kampuni ya Hifadhi Builders, Alphonce Kayombo aliyekutwa eneo
la mradi alisema mradi huo ulioko katika hatua ya pili ya ujenzi,
umesimama kwa muda kutokana na alichodai wajenzi kwenda likizo.
“Mradi
kwa sasa umesimama kwa sababu Waturuki waliopewa kazi ya ujenzi
wamekwenda likizo. Watakaporudi wataendelea na ujenzi mwezi wa nne
kumalizia hatua ya tatu na ya mwisho ili mradi uwe umekamilika ifikapo
mwaka 2018,” alisema Kayombo.
0 comments:
Post a Comment